Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Bandari mpya kujengwa Mbegani
Bandari mpya kujengwa Mbegani
By Habari Tanzania | Published  05/27/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dk. Asha-Rose Migiro, amesema serikali ina mpango wa kujenga bandari mpya kubwa katika eneo la Mbegani wilaya ya Bagamoyo, nje kabisa ya Jiji la Dar es Salaam
Hatua hiyo imechukuliwa kutokana na eneo la Mbegani, kuonekana kuwa lina kina kizuri na salama zaidi, hata kwa kipindi cha miaka 20 ijayo.

Pia, hatua hiyo imechukuliwa kwa sababu bandari ya sasa ya Dar es Salaam, imezidi kuwa finyu kutokana na kujaa tope.

Aidha, hatua hiyo itaiwezesha Tanzania kuwa na bandari kubwa ya kisasa, itakayoweza kuhimili ushindani wa bandari zingine barani Afrika, katika kipindi kirefu cha hata miaka 20 ijayo na itakayoweza kupokea mizigo mingi zaidi kutoka mataifa mbalimbali.

Dk. Migiro alieleza hayo jana, kwenye mkutano wake na waandishi wa habari alioutisha kuelezea taarifa ya ziara ya Rais Jakaya Kikwete, aliyofanya katika nchi za Falme za Kiarabu, Ufaransa, Marekani na Uingereza.

Rais alifanya ziara katika nchi hizo tangu Mei 12 hadi Mei 23, mwaka huu.

Awali, Dk. Migiro alieleza kuwa Rais alipokuwa katika nchi za Falme za Kiarabu (UAE), alionana na Kiongozi Mkuu wa Falme, ambaye pia ni Mtawala wa Dubai.

Pia, Rais alitoa mwaliko kwa wawekezaji wa nchi hizo za Uarabuni, kuja kuwekeza Tanzania katika nyanja za elimu, utalii na miundombinu.

Alifanya nao mazungumzo ya kina ya kuhusu ujenzi wa Chuo Kikuu kingine, kitakachochukua wanafunzi wengi zaidi na pia juu ya ujenzi wa bandari mpya huko Mbegani, wilayani Bagamoyo.

’Tanzania imetakiwa iandae upembuzi yakinifu wa Chuo Kikuu kipya na bandari hiyo ya Mbegani na upembuzi huo uwasilishwe haraka kwenye Mfuko wa Maendeleo ya Abu Dhabi,’ alisema Dk. Migiro.

Akielezea kuhusu hali ya sasa ya bandari ya Dar es Salaam, Dk Migiro alisema eneo lake limezidi kupungua na kujaa tope na kwamba meli moja ilishindwa kutia nanga na kunasa kwenye tope, jirani kabisa na bandari hiyo hivi karibuni.

Alisema hivi sasa meli zinapanga foleni, ili kutia nanga katika bandari ya Dar es Salaam na kwamba meli kubwa ndizo zinapata matatizo zaidi ya kutia nanga.

Dk Migiro aliongeza kuwa ’Kuna nchi kadhaa za jirani, kama vile Botswana, zinataka kutumia bandari ya Dar es Salaam, lakini haziwezi kuitumia ipasavyo kwa sasa kutokana na jinsi ilivyo.’

Waziri Migiro alisema akiwa Ufaransa, Rais Kikwete alikutana na Rais Jac Chirac na kufanya mazungumzo naye kuhusu masuala ya maji, elimu, uendelezaji wa sekta binafsi na michezo.

Akiwa nchini Marekani, Rais Kikwete alikutana na kufanya mazungumzo na Rais George W. Bush, Makamu wa Rais Dick Cheney, Waziri wa Mambo ya Nje Condoreza Rice, Rais wa Benki ya Dunia, Mkurugenzi Mkuu wa IMF, maseneta, wabunge na Naibu Katibu Mkuu wa UN.
 
SOURCE: Nipashe

How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.