Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Wamachinga ni wawekezaji wazalendo wenye mitaji midogo
Wamachinga ni wawekezaji wazalendo wenye mitaji midogo
By Habari Tanzania | Published  10/17/2006 | Habari za Kitaifa | Rating:

SIFA mojawapo ya kujenga ni ushirikishwaji wa jamii katika maamuzi yanayohusu maendeleo yao wenyewe, kinyume cha utaratibu huu ni sawa na kubomoa.

Wamachinga ni vijana wanaojishughulisha na biashara zisizo rasmi mijini.

Biashara hizi ni za kila aina, kuanzia mavazi mpaka vipuri vya magari.

Shughuli za kimachinga ndizo zinazotoa ajira kubwa kwa vijana kuliko nyingine ya aina yoyote nchini, na si hapa Tanzania peke yake, bali hata katika nchi zote zinazoendelea duniani.

Tatizo la wamachinga linaanzia kwenye mfumo au utaratibu unaotumika kufanya biashara.

Wamachinga wamekuwa kero kubwa kwa wakazi wa mijini, kwa utaratibu mbaya wa kibiashara wanaoutumia, hawana utaratibu unaojali shughuli za watu wengine zaidi ya kutizama biashara zao.

Wamekosa uelewa wa kiutendaji wa shughuli zao.Wamelea mabaya ambayo sasa ndiyo kigezo kinachotumika kuhamishwa kila mahali walipo.

Yanayo wakwaza ni ya kisheria na kijamii, lakini si ya kibiashara. Nina maana ya kusema kuwa wamachinga ni shughuli isiyo rasmi, hakuna sheria inayowalinda.

Pia ni maoni ya halmashauri za miji, manispaa na majiji mbalimbali kwamba ni kero kwa wakazi wao kuzingirwa na shughuli za umachinga usiokuwa na utaratibu wa kibiashara.

Wamachinga kwa ujumla wao hawana tatizo la mikopo au soko la bidhaa zao ambayo kimsingi ndiyo matatizo yanayodhoofisha biashara, hasa zenye mitaji midogo.

Mitaji yao ni utendaji wao wa kazi, na ukiona idadi yao imekua, basi ni ishara ya kukua kwa mitaji yao ambayo ndiyo sifa ya sekta isiyo rasmi, kwamba mtaji ni sawa na nguvu inayotumika.

Masuala hayo ya kisheria na kijamii, ndio upungufu wa biashara ya wamachinga uliopo.

Serikali imetenga maeneo ya wamachinga kufanyia biashara zao, kama suluhisho la upungufu huo uliojitokeza, suluhisho lililofikiwa bila ya kuwashirikisha wamachinga hao katika kutoa maamuzi hayo.

Kutoshirikishwa huko kunadhihirika katika namna mbili. Mosi unapowahamisha wamachinga, maana yake ni sawa na kuwaondosha katika soko la bidhaa zao, jambo ambalo si rahisi kwa mfanyabiashara yeyote kulitekeleza, na mpaka soko lizoeleke huko wanako elekezwa waende.

Mmachinga huyu atakua ameisha kula mtaji, na ili aendelee na biashara, basi atalazimika kubinafsisha nguvu zake mwenyewe, jambo ambalo si uamuzi unaoweza kufanywa naye.

Huu ni uamuzi wa mtu baki, kama ingekuwa amehusishwa, tungeona utaratibu uliowekwa kuhakikisha mitaji yao inalindwa.

Uamuzi wa kuwahamisha bila kushiriki kwao, haujali mahitaji yao, zaidi sana unataka utekelezaji tu wa kiimla, na ndivyo inavyojidhihirisha.

Pili, namna maamuzi hayo yalivyopokelewa kwa jazba na kutoeleweka kwa upande wa wamachinga, inaonyesha kutokubaliana na maamuzi hayo.

Inasikitisha kuona jinsi gani serikali inaweza ikasahau umuhimu wa vijana, hasa katika kuwajengea uwezo wa kujitengenezea ajira na wa kujiamulia mambo yanayo wahusu.

Ushirikishwaji wa jamii katika maamuzi ya kimaendeleo, ndio mtazamo wa kisasa katika kutoa maamuzi sahihi ya kimaendeleo yaliyo endelevu, kila utafiti uliofanyika kuhusu maendeleo ya kijamii, ulihimiza ushirikishwaji wa kijamii katika maamuzi ya mipango ya kimaendeleo

Kwa serikali kuwaacha wamachinga katika maamuzi yanayo wahusu si dalili nzuri, uamuzi huo usiokuwa na ushiriki wa kijamii,hauna nia ya kuwajenga wala kuwaendeleza, kwani katika maamuzi mengi ya kimaendeleo serikali imefuata utaratibu wa ushirikishwaji wa kijamii mpaka kuzaliwa kwa misamiati kama MKURABITA na MKUKUTA na mipango kama MMEM,MEMKWA na mengine.

Haya yote yana sifa ya ushiriki wa kijamii na lengo lake ni kuleta maendeleo. Sifa kama hizi hazipo katika maamuzi ya serikali hiyo hiyo inayoamini katika ushiriki wa kijamii katika maamuzi ya kimaendeleo, haikufanya hivyo katika suala la wamachinga, japo basi hata ushiriki wao (wamachinga) uishie kwenye kutunga msamiati mpya wa utekelezaji wa operesheni ‘Tawanya wamachinga’, ingesaidia japo kidogo, lakini kuwaacha nje kabisa ya maamuzi hayo, inaondoa uelewa muhimu wa uwepo wa wamachinga na kusababisha kuwapo maamuzi ya kubomoa badala ya kujenga.

Serikali inajipiga kifua kwamba kumetumika juhudi, busara na hekima ya hali ya juu katika kutoa maamuzi hayo, lakini inasahau mbinu rahisi yenye kuthaminisha busara na hekima iliyotumika ya kuona haja ya ushiriki wao na maamuzi yanayofanywa juu yao.

Wamachinga ndio wanaounda sekta isiyo rasmi (informal sector). Wataalamu wa mambo ya ajira wanasema sekta hii ni matokeo ya wimbi la watu wanaotoka kwenye sekta ya uzalishaji (production sector) kujiunga katika sekta ya huduma (Service Business Sector).

Wanataaluma hao wanasema wimbi hili ni matokeo ya soko la ajira duniani, tofauti ya mapato ni moja ya msukumo huo wa kiajira.

Sekta ya uzalishaji (production Sector), inahusisha kilimo na viwanda (agriculture & industry), nchi nyingi za Kiafrika, ukizungumzia sekta hii unazungumzia uzalishaji katika kilimo.

Katika nchi zilizoendelea, wimbi linalotoka viwandani linahusishwa pia na ukuaji wa teknolojia katika uzalishaji.

Katika nchi zilizoendelea, mapato si sababu kubwa ya wimbi hilo kama ilivyo kwa nchi zinazoendelea, lakini wanaotoka viwandani humo ni wasomi wa kutosha, kwa usomi wao wanaweza ama kuajiriwa katika sekta ya huduma au kujiajiri wenyewe katika sekta hiyo ya huduma, elimu waliyonayo na upatikanaji wa mitaji katika nchi hizo zilizoendelea ni tofauti na zinazoendelea.

Nchi zinazoendelea hazina viwanda vingi au wasomi au hutoa mtaji, badala yake nchi hizo zina kinyume cha hayo yote ya nchi zilizoendelea, matokeo yake hilo wimbi linawahusu vijana wanaoondoka vijijini kuja mijini bila mitaji, wala sifa za kuajiriwa kwa kisomo duni walichonacho, ila wanasukumwa kwa mvuto wa tofauti za kimapato uliopo kati ya sekta hizi mbili.

Hapa kwetu ndio wanaitwa wamachinga. Hata jina hilo tu linaashiria kuhama huko, kwani wamachinga asili yao ni kusini kabisa mwa Tanzania, lakini utawasikia kaskazini hadi Ziwa Victoria. Haina maana kuwa ni wamachinga wote, lakini wanafanana kwa ujio wao mijini, maana yake ni ile ile ya watoka mbali.

Vijana hawa sasa ndio kwa wingi wanaitwa wamachinga, wako wengine wazaliwa wa mijini lakini wana kisomo duni na mitaji midogo. wanajiingiza pia katika kundi la wamachinga (au sekta isiyo rasmi).

Ikumbukwe kuna zaidi ya asilimia 80 ya wananchi vijijini, kwa hiyo wimbi hili si la kwisha leo, kwa lugha sanifu, zoezi hili lina ‘uhai’.

Utafiti unaonyesha kuwa pia sekta hii isiyo rasmi ndiyo inayotoa ajira kwa wingi, hasa kwa vijana.

Vilevile utafiti umebaini kwamba sekta hii ina ujasiriamali ndani yake pamoja na upungufu iliyonao,ujasiriamali (enterpreneurship) huu unakwama kusajiliwa rasmi kwa sababu ya milolongo ya kisheria, kukosekana mikopo na gharama kubwa za usajili wake, hasa katika nchi zilizoendelea.

Hivyo wahusika kwa kuona ugumu huo huendelea kujiendesha katika hali hiyo hiyo ya kutokuwa rasmi ili waendelee na shughuli zao, vinginevyo watakwama waking’ang’ania usajili, ilhali pangekuwapo uelewa wa kiserikali, watu hawa wangeweza kuhamasishwa kuwa wajasiriamali timilifu na wangechangia zaidi uchumi kuliko kubakia katika sekta isiyo rasmi, isiyowapa fursa ya kukua kibiashara au kuchangia pato la taifa.

Na tatizo hili linaanzia kwa watendaji kutojua uwezo wa sekta hii, kama ambavyo wanawatunza wawekezaji wa nje wenye mitaji mikubwa kwa umakini mkubwa, umakini ambao unakosekana kwa wawekezaji wetu wa ndani (wamachinga), eti kwa kuwa wana mitaji midogo.

Nionavyo mimi, ndipo umakini mkubwa ungeelekezwa ili kuilinda mitaji hiyo isipotee, kwani kwa kufanya hivyo serikali inalinda ajira kwa vijana wake, au tuseme kwa kuwa IMF na Benki ya Dunia hawajatoa semina ya jinsi ya kuilinda mitaji midogo midogo kama ya wamachinga, basi hili haliwezekani kwa watendaji wetu wa kiserikali? Aibu.

Halafu watekelezaji hao wanataka tuamini ndio wenye uwezo wa kufanya maongezi ya kibiashara na wawekezaji wakubwa halafu watekelezaji hao hao wanashindwa kukaa na wamachinga, siamini hata chembe kama huo uwezo wa kukaa na wawekezaji wa nje wanao wao kweli hao wawakilishi wa serikali, kama si wanaazima uwezo kutoka Benki ya Dunia na IMF, na kwa sababu washauri hawa hawana wanalolijua kuhusu wamachinga wetu wa ndani, wanakosa la kuwashauri watendaji wetu wa serikali, basi nao wanakosa uelekezi sahihi wa kuilinda mitaji ya Watanzania, wawekezaji wenye mitaji midogo midogo.

Tanzania, Kenya na Uganda ni mojawapo ya nchi zinazoongoza kwa shughuli za sekta isiyo rasmi.

Nchi zote hizi inasadikiwa zina zaidi ya asilimia 50 ya uwiano wa kazi katika miji mikubwa, ni shughuli za sekta isiyo rasmi; na kwa Uganda inasadikiwa ni zaidi ya asilimia 70, uwiano ambao ndio mkubwa zaidi Afrika.

Hivi karibuni kumekuwapo na kutokubaliana na maamuzi ya serikali kuhusu masuala ya wamachinga, si kwa Tanzania tu, hali kama hii imejitokeza Kenya pia, lakini sivyo ilivyo Uganda pamoja na kuwa na ukubwa wa sekta isiyo rasmi.

Wengi wanayaona matunda yaliyofikiwa na Uganda na kudhania ni matokeo ya maamuzi ya kiserikali pekee.

Serikali ya Uganda ilijenga utaratibu wa kuishirikisha sekta isiyo rasmi katika maamuzi na pia ilijenga mazingira ya sekta hiyo kuanza kuchangia pato la taifa kwa kutambua uwezo wao wa kimapato, ufahamu uliowezekana pale ushiriki wa wanasekta isiyo rasmi ulipohusishwa kutoa maamuzi yanayoihusu sekta hiyo, pamoja na ukweli kwamba Uganda ina wasomi wengi zaidi ya Tanzania na Kenya, lakini bado umuhimu wa watu wa kawaida unaheshimika katika kujenga maamuzi yanayolinda uwepo wa jamii na maendeleo yake.

Kinachoonekana sasa ni jinsi upungufu wa kisekta isiyo rasmi unavyoshughulikiwa kwa ushirikiano kati ya wanasekta na Serikali ya Uganda.

Mfano, hakuna mshiriki asiyelipa ushuru, japo ni kidogo, lakini kwa wingi wao ni pato la kutosha linaloweza kutumika kuwasaidia katika maeneo mengi kupitia serikali yao inayokusanya pato hilo.

Uganda, hawahitaji mikopo ya serikali kwenda Makerere, sekta hiyo ilijengewa heshima iliyostahili sasa ni chemchemi ya elimu pia.

Ili haya yafanyike hapa kwetu, yanahitaji muda (si miezi sita tu yakawa yamewezekana) na uvumilivu, ili pawepo na matokeo yanayolinda pato la walengwa na ukuaji wa maendeleo yao, ikumbukwe sekta hii inaendeshwa kwa mtaji mdogo sana na ili ilindwe mitaji hii kunahitajika umakini na upolepole wa maamuzi.

Maamuzi ya kukurupuka yataua mitaji hii, matokeo yake watakuja watu wenye mitaji yao kuziba upungufu wa kimitaji uliotengenezwa na maamuzi hayo na kuitaifisha biashara hii kuwa yao na mwisho wa yote isiwe tena ya faida kwa vijana wanaoifanya bali kwa wakubwa wachache.

Uvumilivu unasaidia kuwa na mtazamo wa kimaendeleo zaidi kwa kuzingatia umuhimu wa sekta hii katika ajira na hata kimapato.

Waswahili husema: “Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo”, tukiilea sekta hii kama uchafu ndivyo itakavyokuwa, na tukiipa heshima inayostahili ndivyo itakavyo jijenga.

Wamachinga wanapata shida sana kuwa na mapokeo mazuri ya maamuzi ya kuwahusu wao, kwa sababu ya kutoshirikishwa katika maamuzi hayo, wanashangaa dola inawaona kama kinyaa, hata kutowashirikisha kuhusu mambo yao ni sawasawa na mtu kukuamulia uishi vipi na familia yako.

Ukiwauliza wamachinga kwa uelewa wao, wanaamini kabisa wanachokifanya ni juhudi ya juu ya maarifa yao, binaadamu yeyote anapokatishwa tamaa katika upeo wake wa juu kabisa wa uelewa, anaweza kubadilika na kuwa chochote, iwe katika mapenzi, kazi, imani na mengine.

Tunashangaa vijana wanakuwa ‘mateja’, mbona hatushangai, tunapowanyang'anya mitaji yao kwa kuwaamulia mambo bila ushiriki wao?

Ikumbukwe vijana ndio taifa la kesho, na wote wanastahili heshima, si walio shuleni tu, kwanza idadi kubwa ni wale walio nje ya shule, tuwashirikishe tuwape heshima ya ushiriki wa maamuzi yao, tutakuwa tunawajengea tabia ya kutafuta suluhu ya masuala yao kwa mazungumzo na si kuvuta bangi, kuwa ‘mateja’, kulazwa Hospitali ya Milembe au kufanya vurugu; yote haya ni kwa kuwa hawapewi lugha mbadala ya kushiriki katika maamuzi yanayowahusu.

Wakubwa waone matokeo haya kuwa ni kutokana na malezi yao. Sekta hii inatoa mpaka wasomi wa chuo kikuu nchini Uganda, na hili si kwa ushauri wa Benki ya Dunia, ni kwa nini isiwezekane hapa kwetu? Kwa nini wakuu wa dola hawalioni hili? Kwa kuwa kila elimu wanayo viongozi wetu, kwa nini kuna haraka ya kulishughulikia suala la wamachinga?

Mbona kwa miaka mingi lilikuwapo na hakuna aliyejali? Kinachofanywa sasa kwa maamuzi haya juu ya wamachinga, ni kuwaathiri kimapato na tatizo halitaishia hapo.

Wamachinga hao watakuwa na suluhisho la hili tatizo kila mmoja kwa namna yake, lakini kubwa ni mtaji wao utaporomoka, na tumeona mtaji wao ni sawa na nguvu zao wenyewe; nguvu hizi sasa watazibinafsisha kwa wenye mitaji ili wawe na uhakika wa kuishi na kufanya kazi.

Lakini ziada yote ni ya mwenye mtaji, matokeo yake hata kama kutakuwa na mipango kabambe hapo baadaye kuhusu wamachinga, mipango hiyo haita wafaidisha wao tena, bali wamiliki wa nguvu zao, na hakika yale yanayoonekana Uganda kwetu itakuwa ndoto, na kama itawezekana, basi si kwa juhudi zao (wamachinga) na wingi unaotegemewa mafanikio hayo kupatikana, bali kwa maamuzi ya wamiliki wa nguvu zao.

Wimbi la wahamiaji kuja mjini ni tatizo hai, ukizingatia ukweli kuwa asilimia 80 ya Watanzania wako nje ya miji, ili kukabiliana na tatizo hili, basi pawepo suluhisho hai, na uhai wa suluhisho hilo ni serikali kufanya kazi kwa ushirikiano na wahusika.

Tumeona wamachinga hata kwa jina walilopewa linaashiria uhamiaji, ushiriki wao katika maamuzi utatoa majibu na suluhisho lililo hai kuhusu wahamiaji wanaoendelea kuja mijini.

Sidhani kama uamuzi uliochukuliwa wa kuwahamisha wamachinga ni suluhisho hai, kwa kuwa sioni jibu kupitia suluhisho hilo, kwa wanaoendelea kuingia mijini.

Lakini kama maamuzi hayo yana mchango wa wahusika, suluhisho hai hilo lina kuwa na sifa ya uendelevu hata kwa wajao.

Wasi wasi wa polisi wa amani kupotea ni ishara mbaya ya suluhisho tulilonalo, zoezi la wamachinga lingeweza kutatua tatizo la amani kwa asilimia kubwa kama mazingira ya kibiashara yangezingatiwa, pakiwapo ugumu wa mhamiaji kuwa na biashara ni dhahiri atajihusisha na shughuli za kuhatarisha amani kwa nia ile ile ya kujiajiri lakini kwa njia isiyo halali.

Wamachinga wanapata ajira na kupunguza vitendo vya upoteaji wa amani lakini pakiwapo juhudi za kupunguza mitaji ambayo ni sawa na kupunguza idadi yao mijini ilhali uhalisi wa mambo unaashiria kuongezeka kwa ujio wao, basi tunajenga tatizo ambalo hakuna atakayekuwa na jibu lake miaka si mingi ijayo.

Serikali yetu inapoteza nafasi nzuri sana ya kuwajengea uwezo wa kimaendeleo vijana wake, ilichohitaji ni kujua uwezo wa wamachinga, kuwaeleza matarajio ya serikali yao ili nao wajipange kwa kujituma kufanana na matarajio hayo, serikali ingepanga malengo kwa kuwashirikisha wamachinga, iwajengee uelewa wa kiutendaji hasa katika shughuli zao, iwasaidie kwa kuwaweka pamoja ili wawe na umoja, isaidie kuwapa changamoto za kujua wenzao wanafanya nini.

Mbona hatusikii wamachinga wamepata safari na rais wao kwenda nje kuonana na wafanyabiashara kama wao, wakajifunze kwa mfano Uganda, Nigeria na kadhalika.

Wakuu wetu wanachohitaji kujua, ni kuipa heshima sekta hii, kwa kuona haja ya kuikuza na kuilinda kwa ushiriki wa hao wahusika katika maamuzi yanayowahusu wao, polepole matokeo yake yanakuwa endelevu zaidi ya vurugugu.

Kwa maoni yangu, mfumo wa Uganda ungefaa kuuiga kama tumeshindwa kuwa na wa kwetu.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.