Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Wasiofaa wawekwe kando
Wasiofaa wawekwe kando
By Habari Tanzania | Published  10/17/2006 | Habari za Kitaifa | Rating:

RAIS Jakaya Kikwete, jana aliwaapisha mawaziri 10 na naibu mawaziri wanane, baada ya kufanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri.

Haya ni mabadiliko ya kwanza kufanywa na Rais Kikwete, tangu atangaze Baraza la Mawaziri Januari 4, mwaka huu.

Mabadiliko haya ni kama ‘mvinyo wa kale ndani ya chungu kipya’. Wananchi wameyapokea kwa maoni tofauti. Wapo wanaopongeza uamuzi wa Rais, wakiamini kuwa kitendo hicho kinaweza kuwafanya mawaziri na naibu mawaziri wasibweteke.

Kitendo hicho kinawakumbusha kuwa wao wameteuliwa ili kuwatumikia wananchi, na kwamba wasijisahau kwa kudhani kuwa wanaweza kuvurunda kazi, kisha wakaachwa hivi hivi. Uamuzi wa Rais unathibitisha kauli yake kwamba kwenye urais hana ubia na yeyote awaye.

Lakini wapo walioponda mabadililiko haya. Hawa ni wale wanaoamini kuwa Rais Kikwete alichopaswa kufanya ni kuwaweka nje ya Baraza, mawaziri na naibu mawaziri wababaishaji.

Si siri kwamba kuanzia Januari hadi Oktoba, Watanzania wameweza kujua ni mawaziri na naibu mawaziri wapi ni wachapakazi, na wapi ni wababaishaji.

Kwa mfano, kumekuwapo kauli nyingi za kugongana kuhusu suala la umeme. Rais Kikwete ameweza kusimama na kuwahakikishia Watanzania kuwa tatizo la umeme lingemalizwa ndani ya muda fulani.

Rais alisema haya baada ya kuwa amehakikishiwa na viongozi wahusika. Naye bila hiana, akasimama na kutoa kauli zilizosheheni tambo, za kuwahakikishia Watanzania kuwa tatizo la umeme, linadhibitiwa.

Kinyume cha tambo hizo, hali inazidi kuwa mbaya siku hadi siku. Mara wananchi wanaambiwa kuwa kampuni iliyopewa kazi ya kuleta vifaa vya umeme, ni ‘kampuni hewa’. Haipo. Tayari wahusika wameshalipwa mabilioni ya shilingi.

Tunaamini kuwa tuhuma hizi ni nzito, na kwa kweli zinahitaji majibu ya haraka kabla wananchi wenyewe hawajachukua nafasi ya kuutafuta ukweli huo.

Tuhuma kama hizi si za kuacha zielee elee katika jamii bila kupewa majibu. Kama ni kweli kwamba kuna utapeli umefanyika, viongozi wahusika wajipe moyo, wasimame waueleze umma wa Watanzania ukweli wa mambo.

Kuendelea kunyamaza, kunaashiria mambo mengi. Mosi, inawezekana yanayosemwa ni kweli; pili, inawezekana viongozi wanawadharau wananchi, na kwa maana hiyo, hawaoni sababu ya kulizungumzia suala hilo.

Pamoja na ukweli kwamba kilichofanywa na Rais Kikwete bado kinaitwa mabadiliko, sisi tunadhani anapaswa kwenda mbali zaidi.

Aanze kuwashughulikia viongozi wanaotuhumiwa kwa makosa kadha wa kadha.

Tunasema hivyo tukiamini kuwa tabia ya kuleana haipaswi kupewa nafasi hata kidogo. Kuleana au kulindana kumeligharimu taifa kwa mambo mengi, yakiwamo ya upotevu wa mabilioni ya shilingi.

Kama kiongozi anaonekana hafai, ni vema kumwondoa. Rais aache nadharia ya ‘pengo halizibiki’.

Kuna Watanzania wengi ambao ni wazalendo wanaoweza kushika nyadhifa mbalimbali na kuwaletea Watanzania maendeleo ya kweli.

Pia viongozi katika ngazi nyingine wahakikishe kuwa wanaowasimamia, wanatekeleza wajibu wao.

Tukiwa na utaratibu wa kubanana katika utekelezaji wa dhima zetu, taifa letu litabadilika. Litakuwa taifa la kupigiwa mfano. Lakini kama ni suala la kuoneana haya au kulindana, ile ahadi ya ‘maisha bora kwa kila Mtanzania’, haitatekelezeka.

Kila mmoja wetu, katika nafasi yake, akitekeleza wajibu wake, jamii yetu itapiga hatua kubwa kimaendeleo.

Pamoja na kumpongeza Rais Kikwete kwa mabadiliko aliyofanya, sisi tunasema bado ana kazi kubwa. Asiwaonee haya watendaji wasiowajibika. Awaweke kando. Kuna Watanzania wengi wanaoweza kuongoza vizuri.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.