KAMPUNI ya Interstate inayojihusisha na uchimbaji madini sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi, inakusudia kumfikisha mahakamani, Mkuu wa Wilaya (DC) ya Ulanga mkoani Morogoro, Dk. Ramadhan Utengwe.
Hatua ya kampuni hiyo imekuja baada ya DC huyo kuamuru wachimbaji wadogo katika eneo la Ipanko, Morogoro wavamie mgodi unaomilikiwa na kampuni hiyo kisheria.
Wiki iliyopita, DC huyo alitangaza kufunguliwa kwa mgodi huo uliofungwa kwa mwezi mmoja, kutokana na mzozo kati ya Kampuni ya Interstate na wachimbaji wadogo.
Dk. Utengwe, aliwatangazia wachimbaji wadogo kuwa, sasa wana haki ya kurejea eneo hilo na kuendelea na shughuli za uchimbaji madini.
Alitumia fursa hiyo pia kuwapiga marufuku Interstate ambao wanadai kwamba wamepewa leseni halali iliyosainiwa na aliyekuwa Waziri wa Niashati na Madini, Dk. Ibrahim Msabaha.
Wakili wa kujitegemea wa Kampuni ya Makoa, Anney, anayeiwakilisha Kampuni ya Interstate, alisema Interstate inamiliki eneo hilo kihalali, jambo ambalo DC analifahamu.
Alisema eneo hilo sasa limevamiwa na wachimbaji wadogo kutokana na maelekezo ya DC, na hivyo kuhatarisha hali ya amani na utulivu katika eneo hilo. Wakili huyo amempelekea barua DC, na kulaani dhana ya ukabila inayotumiwa na kiongozi huyo kuitenga Kampuni ya Interstate.
Kampuni hiyo inamilikiwa na mwekezaji mzalendo anayetoka mkoani Arusha.
“Maelekezo yako kwa wachimbaji wadogo, yamesababisha hasara kubwa kwa Kampuni ya Interstate ambayo imewekeza vifaa mbalimbali kwa ajili ya kuanza kazi ya uchimbaji madini katika eneo hilo na kuhatarisha hali ya usalama na amani kwa wafanyakazi wa Interstate wanaolinda na kufanya kazi katika eneo hilo ambao sasa wamekuwa paka na panya,” ilisema sehemu ya barua ya mwanasheria huyo.
Alisema DC huyo analalamikiwa kwa kutoa amri kwa wafanyakazi wa Interstate, akiwazuia wasiingie katika eneo hilo, huku akijua fika kuwa wao ni Watanzania, wana haki na wanaruhusiwa kwa mujibu wa katiba kuhamia sehemu yoyote na kufanya kazi yoyote kisheria ndani ya taifa lao.
Wakili huyo alisema DC huyo anajua fika kwamba Kampuni ya Interstate imepata leseni namba 4110/2006 iliyotolewa na Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Msabaha na leseni hiyo inahusu pia eneo lililovamiwa na wachimbaji wadogo baada ya kuruhusiwa kufanya hivyo na DC huyo.
Licha ya kukusudia kuchukua hatua, wakili huyo alisema Kampuni ya Interstate nayo inajiandaa kuanza kuchimba madini katika eneo hilo lililovamiwa na wachimbaji wadogo kama leseni inavyoruhusu.
Kwa upande wake, DC huyo jana alizungumza kwa simu na Tanzania Daima na kusema uamuzi wa kuwarejesha wachimbaji wadogo katika eneo hilo umetolewa na Wizara ya Nishati na Madini.
“Wizara imewaruhusu waendelee, mmiliki halali wa eneo hilo ni Joseph Mworia, Interstate hawana leseni halali,” alisema DC huyo.
Kwa msimamo huo, kuna dalili za kutokea vurugu katika eneo hilo, hasa ikizingatiwa kuwa wabunge wawili, Dk. Juma Ngasongwa na Celina Kombani, wametoa baraka zao zote za kuwaunga mkono wachimbaji wadogo.
Dk. Ngasongwa ni Mbunge wa Ulanga Mashariki, na Waziri wa Mipango, Uchumi na Uwezeshaji; ilhali Kombani ni Mbunge wa Ulanga Magharibi na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Miezi kadhaa iliyopita, Dk. Ngasongwa, kwa niaba ya mwenzake (Kombani), alitoa taarifa ya kimaandishi akiunga mkono juhudi zote wa wachimbaji wadogo kuwang’oa Interstate katika eneo hilo.
Habari ambazo Tanzania Daima imezipata kutoka Mahenge, zinasema kuwa hali ya usalama katika mgodi huo iko shakani kutokana na chuki iliyopo sasa kati ya wafanyakazi wa Interstate na wachimbaji wadogo.
Mgogoro huo ni wa muda mrefu. Ulianza baada ya Ofisa Madini Kanda ya Morogoro, Hamisi Komba, kutoa barua iliyotofautiana na leseni iliyotolewa na serikali kwa Interstate, ikiruhusu wachimbaji wadogo kuendelea na kazi zao katika eneo hilo ilhali akijua kwamba Interstate ndiyo iliyokabidhiwa eneo hilo kisheria.
Hali hiyo iliifanya Wizara ya Nishati na Madini ipeleke maofisa wake Mahenge na kuzungumza na pande zote mbili kwa lengo la kupata muafaka. Haieleweki kama agizo la DC la kuwarejesha wavamizi hao ndiyo msimamo mpya wa serikali.