MABADILIKO ya mawaziri, yaliyofanywa na Rais Jakaya Kikwete, yamezua maswali mengi kuliko majibu.
Baadhi ya wananchi, wakiwamo wanasiasa wa vyama mbalimbali waliohojiwa, wamejikuta wakishindwa kueleza sababu hasa za mabadiliko hayo. Wakati baadhi wakiponda mantiki ya kubadilishwa wizara badala ya kufukuzwa, wengine wanauona uamuzi huo wa Rais Kikwete kuwa usio na manufaa kwa taifa.
Kama ilivyokuwa kwa wananchi, baadhi ya mawaziri waliobadilishwa ambao waliapishwa Ikulu jijini Dar es Salaam, nao walijikuta wakipata kigugumizi kutoa maoni yao kuhusu mabadiliko hayo.
Mmoja wa mawaziri aliliambia gazeti hili kwamba, siri ya mabadiliko hayo anayo Rais Kikwete na wengine wote watabakia kujenga hoja zisizo na uhakika.
Wananchi kadhaa waliohojiwa na Tanzania Daima juzi na jana walisema, ni ukweli ulio wazi, kwamba wapo mawaziri na naibu mawaziri walioshindwa kazi tangu wateuliwe Januari 4, mwaka huu. Kwao hao, wanasema ingekuwa busara wakatupwa nje ya Baraza, badala ya kuwahamishia kwingine.
Pia baadhi ya waliohojiwa, walisema mawaziri na naibu mawaziri kadhaa wanahusishwa na kashfa kadhaa, zikiwamo za kutoa taarifa potofu kwa Rais Kikwete. Kwa sababu hiyo, wanasema ingekuwa vema kama wangeadhibiwa kwa kuachwa.
Chama cha Wananchi (CUF) katika kauli yake kilisema, mabadiliko hayo yanadhihirisha kushindwa kwa baadhi ya mawaziri kutimiza wajibu wao sawasawa.
Kaimu Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Uhusiano wa Umma, Mbaralah Maharagande, alisema: “Sisi kama CUF tulimshauri rais aunde baraza dogo ambalo angeweza kulimudu, matokeo yake aliunda kubwa ambalo anashindwa kulimudu, hadi anafikia hatua ya kuwapanga upya.”
Alisema hali hii inaweza ikaendelea na hivyo ikasababisha ajikute wakati mwingine tena siku zijazo akalazimika kuwaondoa kabisa. “Kuna watu wana uwezo wa kushika nafasi hizo ambao si wanachama wa chama tawala, wengine hawapo kwenye chama chochote, lakini wameachwa tu,” alisema.
Alisema mawaziri na naibu mawaziri walioharibu na kuhamishwa wizara, watasambaza uoza.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia, amesema kitendo cha Rais Kikwete kufanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri, kinaonyesha udhaifu mkubwa.
“Watanzania tumekuwa tukishuhudia mtu akiharibu anahamishiwa mahali pengine badala ya kufukuzwa, awali tulielezwa kuwa tatizo la umeme litamalizika mwezi wa nane mwishoni, na hata wiki mbili zilizopita rais alitembelea pale Ubungo na kusema tatizo hilo litaisha, lakini hadi sasa hakuna hata jenereta pale Ubungo.
“Ushauri wangu kwa rais ni kwamba kama anataka wananchi wawe na imani naye, basi mawaziri wanapoharibu wawajibishwe na si kuwahamisha, anawatoa sehemu moja kuwapeleka sehemu nyingine na kule wataenda kufanya yale yale,” alisema Mbatia.
Wabunge kadhaa wa CCM ambao wameomba majina yao yahifadhiwe wamesema, mabadiliko hayo hayana faida kwa maelezo kwamba baadhi ya waliobadilishwa, hawana uwezo wa kuchapa kazi. Walikosoa mabadiliko hayo, wakisema ni mapema mno kwani walipaswa wapewe muda walau wa kumaliza bajeti ya mwaka mmoja.
“Rais kufanya mabadiliko ni dhahiri kabisa ameona kuna upungufu kwa viongozi wake, lakini ikumbukwe kuwapangua si suluhisho,” alisema mmoja wa wabunge hao.
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Erasto Tumbo, ameponda mabadiliko hayo. Alisema mabadiliko hayo yameharibu mtiririko mzima wa utendaji kazi kwa viongozi hao.
Tumbo alisema pamoja na nia nzuri au mbaya aliyokuwa nayo rais, amepotoka kwa kuwa kasi mpya iliyokuwa ikisubiriwa na wananchi, sasa inazimika. “Juzi tu, mawaziri ambao miongoni mwao wamebadilishwa, walikuwa bungeni wakiwasilisha na kutetea bajeti zinazohusiana na wizara zao; na Bunge kuzipitisha, sasa leo hii kumekuwa na mabadiliko ya mawaziri na naibu mawaziri, sioni kama utendaji utakuwa mzuri, hasa katika upitiaji wa bajeti hizo ikiwa kuna mabadiliko haya.
“Kama waziri ameondolewa na kupelekwa katika wizara nyingine, unatarajia nini? Hata kuuona udhaifu wa mtu kiutendaji umeuona lini? Hapa rais kachemsha, alichofanya ni pupa, wanatupotezea muda; kubadilisha mawaziri na naibu mawaziri ni kurudi nyuma,” alisema Tumbo.
Aliendelea kusema: “Nilikuwa na imani kuwa Januari mwakani kwa bajeti iliyopitishwa, tungeanza kuona matunda ya utendaji kazi kwa mawaziri na naibu mawaziri hao.”
Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labor (TLP), Augustino Mrema, amesema kuwa Rais Kikwete anafanya mzaha kwa wananchi. Amesema kilichotakiwa si kuwahamisha mawaziri na naibu wao, bali kuwaweka nje kabisa ya Baraza la Mawaziri.
Mrema alisema kuna baadhi ya mawaziri ambao hawakutakiwa kuhamishwa.
“Wizara ya Miundombinu ilikuwa inashikiliwa na Basil Mramba ambaye anaonekana hakufanya lolote katika kipindi cha miezi tisa,” alisema.
Mrema alisema kuwa Rais Kikwete hajiamini kwa anachofanya. Alimkosoa kwa mabadiliko hayo, akisema tayari viongozi hao walishaanza kuzoea nafasi zao. “Anatakiwa akumbuke kuwa aliwahi kuwapeleka Ngurdoto na kuwapa semina akiwa nao, sasa leo anawageuka… hili rais anafanya mzaha na wananchi kwa kuwa anawachanganya,” alisema Mrema.
Mmoja wa wasomi mahiri nchini, Profesa Haroub Othman, alipozungumza na Tanzania Daima kwa simu, alikataa kutoa maoni yoyote kuhusu mabadiliko yaliyofanywa na Rais Kikwete.
Baadhi ya mawaziri na naibu mawaziri waliohamishwa kutoka kwenye wizara walizokuwa wamezishika kwa miezi tisa kwenye mabadiliko aliyofanya Rais Jakaya Kikwete, na kuyatangaza, jana walitoa maoni mbalimbali juu ya mabadiliko hayo kabla na baada ya kuapishwa kwenye viwanja vya Ikulu, Dar es Salaam.
Sura za mawaziri na naibu mawaziri hao zilionekana dhahiri kuwa na mshituko na hakika baadhi yao hawakuweza kuficha hisia zao wakati wote walipokuwa katika viwanja vya Ikulu, kabla, wakati na hata baada ya kuapishwa na Rais Kikwete.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Joseph Mungai, ambaye amehamishiwa Wizara ya Mambo ya Ndani akitokea Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, aliiambia Tanzania Daima, alipokuwa akiingia kwenye lango la Ikulu kuwa, mabadiliko hayo kwake yalikuwa ni ya kushitukiza, lakini anakubaliana nayo, na kwake itamsaidia kubadilisha upepo kwa sababu amekwisha kukaa kwenye wizara hiyo ya kilimo tangu enzi za serikali ya awamu ya pili.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Basil Mramba, alisema mabadiliko hayo ni chanya na kwake yeye sio mageni, na wizara ambayo amepelekwa amekwisha ifanyia kazi kwenye serikali ya awamu ya pili.
“Nitakachoanza nacho kwenye wizara hii ni kuhakikisha kunakuwa na ubora kwenye bidhaa zetu tunazozalisha, kuimarisha viwanda vidogo vidogo na kuvifufua vile ambavyo vilikuwa vimekufa… ajira nyingi zinaweza kupatikana kutokana na viwanda hivi,” alisema Mramba.
Aliyekuwa Waziri wa Maji, Stephen Wasira ambaye amehamishiwa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, yeye alisema siri ya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri anayo rais mwenyewe, na kama kuna mtu mwingine ataitoa atakuwa anaunda tu sababu zake ambazo hazitakuwa na uhakika wowote.
Alipoulizwa kama kubadilishwa kwake kunatokana na utendaji mbovu alisema, rais hawezi kubadilisha waziri na kumpeleka kwenye wizara nyingine kama hakutenda vizuri. “Mimi ninachoamini ni kuwa, nimefanya vizuri na ndio maana ananipeleka kwenye wizara nyingine ili nifanye vizuri na huko pia,” alisema Wasira.
Alisema ni kweli kuwa, miezi tisa tu isingetosha kuondoa tatizo kubwa la maji, lakini kwa miezi hiyo tisa, ameweza kutengeneza mpango ambao walikuwa wameanza kuufanyia kazi na hakika unaweza kufanikiwa.
Kwa upande wake, Waziri mpya wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi akizungumzia sekta ya madini alisema, tayari kazi imeanza kufanyika kama ilivyoonekana kwenye kampuni za madini zilizoingia mkataba mpya na serikali hivyo, safari yake imekwisha anza na ana uhakika itaweza kufanyiwa kazi na mambo mengi kuhusu mikataba hiyo yataeleweka.
Naibu Waziri, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Salome Mbatia, yeye kwa upande wake alisema anayafurahia mabadiliko hayo na kumshukuru rais kwa uamuzi huo aliosema ameupokea kwa moyo mkunjufu.
“Hii ni serikali moja na naahidi kufanya kazi kwa moyo wangu wote... kuna mengi ya kuangalia kwenye wizara hii, lakini hasa masuala ya watoto yatima na maendeleo ya kina mama ambao mara kwa mara wanaachwa nyuma kwenye shughuli za maendeleo,” alisema Mbatia.
Dk. David Mathayo, yeye anasema mabadiliko hayo ya Baraza la Mawaziri ni jambo la kawaida kwa sababu rais amepewa mamlaka ya kikatiba kulibadilisha baraza lake la mawaziri wakati wowote atakapoona inafaa. Anasema katiba haisemi ni lini na wala kwa muda gani. Ameyapokea mabadiliko hayo na ameahidi kufanya kazi kwa bidii kubwa.
Lawrence Masha anayetoka Nishati na Madini kwenda Mambo ya Ndani kama Naibu Waziri na Ibrahim Msabaha aliyehamishiwa Wizara ya Afrika Mashariki, walipotakiwa kutoa maoni yao walikataa kwa madai kuwa walikuwa wakihitaji kujiandaa na kuwa baada ya sherehe za kuapishwa ni kunywa maji ya matunda (juice, na sio kufanya mahojiano na waandishi wa habari).
Rais mara baada ya kuwaapisha mawaziri na naibu mawaziri hao na kupiga nao picha ya pamoja, hakuwa na muda tena na mazungumzo nao zaidi ya kusalimiana na wachache na kuwaambia kuwa atapata muda wa kuzungumza nao baadaye na kuinga ndani ya Ikulu huku akisindikizwa na wasaidizi wake.
Walioapishwa jana ni Andrew Chenge, aliyetoka kwenye Wizara ya Afrika Mashariki Kuwa Waziri wa Miundombinu; Mramba, Wizara ya Viwanda na Biashara; Joseph Mungai, Wizara ya Mambo ya Ndani; John Chiligati, Wizara ya Kazi na Vijana; Anthony Diallo, Wizara ya Maendeleo ya Mifugo; Ibrahim Msabaha, Wizara ya Afrika Mashariki.
Wengine ni Stephen Wasira, Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika; Jumanne Maghembe, Maliasili na Utalii; Nazir Karamagi, Nishati na Madini. Dk. Shukuru Kawambwa anayekwenda Wizara ya Maji, hakuwepo kwenye kuapishwa kutokana na kuwa nje ya nchi kikazi.
Naibu mawaziri walioapishwa na wizara zao mpya zikiwa kwenye mabano ni, Dk. Emmanuel Nchimbi (Kazi na Maendeleo ya Vijana), Daniel Nsanzugwanko, (Habari, Michezo na Utamaduni), David Mathayo David (Kilimo, Chakula na Ushirika), Hezekiah Chibulunje, (Viwanda, Biashara na Masoko), Dk. Batilda Buriani, (Mipango, Uchumi na Uwezeshaji), Salome Mbatia, (Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto), Lawrence Masha, (Mambo ya Ndani) na Bernard Membe (Nishati na Madini).