JUZI RAIS Jakaya Kikwete aliongoza wananchi wa Tanzania katika uzinduzi wa mchakato wa kitaifa wa kupata maoni ya wananchi kuhusu kuharakisha kuanzishwa kwa shirikisho la Afrika Mashariki litakalotoa kipaumbele katika mtangamano wa kisiasa.
Uzinduzi huo, ulifanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam na mbele ya viongozi mbalimbali wakiwemo marais wastaafu, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa. Kwa mujibu wa ratiba ya mcakato, pia, viongozi wa Kenya, Mwai Kibaki na Yoweri Museveni wa Uganda, nao walizindua mchakato huo juzi katika nchi zao.
Akizindua kamati ya mchakato huo, Rais Kikwete alisema mazingira ya sasa, hasa katika dunia ya utandawazi yanahitaji kuwa na ushirikiano wa aina hiyo katika kujenga uwezo wa kuhimili ushindani uliopo.
Kama wadau muhimu katika mchakato huu, kwanza tunapongeza hatua hii muhimu iliyofikiwa na serikali zote tatu katika kufikia ushirikiano wa hakika na wenye lengo la kunufaisha kila mmoja.
Tunapenda kuwaomba na kuwashauri wananchi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla wetu kwamba tujitokeze kwa wingi mbele ya kamati hizo na kushiriki kikamilifu katika kutoa maoni yetu kwa uwazi na kwa uhuru katika jambo hili muhimu na la kihistoria.
Tunasema hivi kwa sababu tunaona kazi hii haitaweza kufanikiwa, wala sisi hatuwezi kuheshimika, wala kutamba katika majukwaa ya kimataifa iwapo tutabakia nyuma na kisha kuwa watu tuliogawanyika, tusioshirikiana na maskini.
Haitakuwa jambo la busara wala la hekima, kama tutaachia zoezi hili la kutoa maoni liende hivi hivi tu, bila ya kwanza kufahamu kwa kina na kisha kutoa maoni yetu kwa kuzingatia maslahi ya utaifa wetu.
Tunaamini kuwa kama wananchi tutajitokeza na kuwasilisha maoni yetu kama tunavyotarajia, basi tutaendelea kushuhudia na kuvuna na au kuchangia katika jitihada za kulipeleka mbele taifa letu kimaendeleo.
Hatuna shaka kwamba kamati zlizoteuliwa kukusanya maoni ina kila uwezo, kila nia njema na kila kifaa cha kuweza kufanikisha malengo mazuri ilichojiwekea, lakini kilio chetu ni kuweza kwao kuwafikia watu wengi kadri inavyopaswa.
Tunajua kamati hiyo makini na kamambe, imeundwa na watu wenye ujuzi na tunajua pia ina majukumu mengi ya kitaifa na kimataifa, hatutapenda tena kusikia eti kunakuwapo na tatizo la watu kutofikiwa. Itatuangusha.
Kwa hiyo, hatukatai pia kwamba kunaweza kukawa na matatizo ya hapa na pale na hasa kwa kuwa nchi yetu au mataifa yetu matatu yana eneo pana basi na tujitahidi ili kusudi tutekelezea tunachokitaka.
Tunapenda kuikumbusha Kamati ya kukusanya maoni kwamba fursa waliyo nayo inaenda sambamba na majukumu mengi na changamoto pia hivyo hatuna shaka kwamba wataweza kukabiliana nazo.
Kwa kufanya hivi, tunaamini kabisa kwamba tutajisaidia wenyewe, tutaisaidia jumuiya yetu ya Afrika Mashariki, tutamsaidia Rais, katika kusonga mbele kwa mataifa yetu pamoja na kupeleka mbele maendeleo kwa kasi zaidi. Sote, tutimize wajibu wetu