SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi nchni (TUCTA) na vyama vyake shirikishi limeitaka serikali kurejea upya pendekezo la Kamati ya Rais ya kuboresha mishahara ya watumishi waendeshaji na kulitekeleza kama ilivyokuwa kwa wenzao wanataaluma.
Shirikisho hilo pia limesema endapo serikali itaendelea kulipuuza suala hilo, litaunga mkono hatua zozote zitakazochukuliwa na wafanyakazi wa Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia, Ufundi Stadi, Habari na Utafiti (RAAWU), kwa ajili ya kutetea masilahi yao.
Hayo yalielezwa jana na Katibu Mkuu wa TUCTA, Nestory Ngulla, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu msimamo wa TUCTA, kuhusu mishahara ya wafanyakazi waendeshaji vyuo vikuu na vyuo vikuu vishiriki vya umma.
Alisema ni lazima seriakli ikubali kuwa zipo dosari za msingi katika kushughulikia suala zima la mishahara ya watumishi hao, na kwamba dosari hizo zisiporekebishwa zitaathiri ufanisi wa kazi kwenye vyuo hivyo.
“RAAWU imetoa tamko linalokusudia kutangaza mgogoro dhidi ya serikali Oktoba 16, endapo itaendelea kukaidi kutekeleza sehemu ya mapendekezo ya Kamati ya Rais ya kuboresha mishahara ya watumishi wa vyuo vikuu na vyuo vikuu vishiriki vya umma.
“Katika kutafuta ukweli juu ya suala hili, TUCTA imebaini kuwa kumbukumbu za vikao vya kamati ya rais zinazoonyesha kuwa suala la kuboresha mishahara ya wafanyakazi waendeshaji lilijadiliwa na kufanyiwa uamuzi kuwa liwe mojawapo ya mapendekezo ya kamati ya Rais, na ndiyo inavyoonekana kwenye taarifa ya kamati maalumu ya kushauri serikali juu ya kuboresha masilahi ya watumishi hao,” alisema.
Alisema kwa mujibu wa taarifa ya RAAWU kwa TUCTA, Rais Septemba 2005, aliagiza kuundwa kwa kamati ya kuboresha mazingira ya wafanyakazi katika vyuo vikuu na vyuo vikuu vishiriki vya umma.
Kamati hiyo pamoja na mambo mengine ilipendekeza kuboreshwa kwa mishahara ya wanataaluma kwa asilimia 50 ifikapo Januari 2006 na kukamilisha asilimia 100 ifikapo Julai.
Kamati hiyo pia ilipendekeza kuboreshwa kwa mishahara ya wafanyakazi waendeshaji kwa asilimia 100 ifikapo Julai mwaka huu, kwa kujumuishwa kwenye bajeti ya 2006/2007