Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Magufuli, Mramba majeruhi wa mwanzo mawaziri wa JK!
Magufuli, Mramba majeruhi wa mwanzo mawaziri wa JK!
By Habari Tanzania | Published  10/15/2006 | Habari za Kitaifa | Rating:
na Absalom Kibanda

WAZIRI wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi, John Pombe Magufuli, yuko katika wakati mgumu kikazi pengine kuliko kipindi kingine chochote maishani mwake.

Magufuli, waziri aliyeng’ara pengine kuliko mwingine yeyote katika kipindi cha miaka mitano ya mwisho ya Serikali ya Awamu ya Tatu iliyokuwa ikiongozwa na Rais Benjamin Mkapa, sasa anaonekana akianza kupewa sifa nyingine, tofauti kabisa ya zile alizokuwa nazo hadi mwishoni mwa mwaka jana.

Utendaji kazi wa Magufuli tangu akiwa Naibu Waziri wa Ujenzi chini ya Anna Abdallah, kabla ya kupanda cheo na kuwa waziri kamili katika wizara hiyo hiyo, ulipata sifa kubwa ndani na nje ya nchi, kiasi kwamba, mara kadhaa Rais mstaafu Benjamin Mkapa alipata kumwita ‘askari wangu wa mwamvuli’, akimaanisha mchapakazi hodari.

Leo hii, nyota hiyo ya Magufuli inaonekana kugeuka haraka, chini ya kivuli ambacho bado hakijajulikana sawasawa, ingawa tayari yameibuka makundi mawili yanayopingana katika suala hilo.

Habari ambazo Tanzania Daima Jumapili imezikusanya kutoka vyanzo mbalimbali vya habari ndani ya serikali, na kutoka miongoni mwa watu wanaomfahamu Magufuli na mwenendo wa sasa wa kisiasa, zinasema, kundi la watu ambalo nia yao haijulikani, linafanya kila liwezalo hivi sasa kuanika kile ambacho linakiona kuwa uchafu usiovumilika kwa waziri huyo.

Sambamba na Magufuli, mwanasiasa mwingine ambaye naye anaweza akajikuta akiingia katika kikaango hicho hicho cha Magufuli, ni Waziri wa Miundombinu, Basil Pesambili Mramba, ambaye amekuwa waziri kwa miaka mingi wakati wa serikali za awamu ya pili na tatu.

Kama alivyo Magufuli, habari hizo zinaeleza, Mramba naye anaweza akajikuta akiwa katika wakati mgumu kutokana na maamuzi kadhaa ambayo yalifikiwa na serikali wakati yeye akiwa ni Waziri wa Fedha kwenye Serikali ya Awamu ya Pili, akichukua wadhifa huo kutoka kwa Daniel Yona.

Kwa mujibu wa habari hizo, kundi hilo, linalojumuisha maofisa wa serikali, wakiwamo wale ambao ama walifanya kazi na Magufuli na Yona katika Wizara ya Ujenzi na Wizara ya Fedha au wanaofanya nao kazi sasa, limedhamiria kuendelea na mkakati wake huo hadi hapo, Magufuli na/au Mramba watakapolazimika ama kuijiuzulu wenyewe au kuachishwa kazi na Rais Jakaya Kikwete.

Jitihada za gazeti hili kuwasiliana na Magufuli ambaye yeye tayari ameshaanza kuonja makali ya mkakati huo wa siri kwa simu yake ya mkononi au kwa njia ya ujumbe mfupi wa maneno ili kupata maoni yake kuhusu mwenendo wa sasa wa mambo dhidi yake, awali zilishindikana kwani kila alipokuwa akitafutwa simu yake iliita bila kupokewa.

Hata mwandishi alipomweleza Magufuli kwa njia ya ujumbe wa maneno kwamba gazeti hili lilikuwa na ujumbe muhimu wa kuwasiliana naye, pamoja na simu kuonyesha kuwa ujumbe ulikuwa umefika katika simu yake, aliendelea kukaa kimya pasipo kujibu lolote.

Muda mfupi kabla hatujaenda mitamboni, Waziri Magufuli aliwasiliana na chumba chetu cha habari, na akizungumza kwa sauti ya taratibu baada ya kuulizwa maoni yake kuhusu taarifa hizo, alimtaka mwandishi kuwasiliana naye wakati mwingine akisema; “nitakutafuta” na kukata simu.

Habari za uhakika ambazo gazeti hili linazo kutoka vyanzo vingine kadhaa vya habari zinaeleza kwamba, kundi linalomwandama Magufuli linafanya hivyo kifua mbele likitambua kwamba, yeye hakuwa miongoni mwa watu waliokuwa wakiunda timu iliyojulikana kwa jina la wanamtandao, ambayo ndiyo iliyoongoza kampeni za kuhakikisha Kikwete anaingia madarakani.

“Unajua huyu Magufuli hivi sasa amekalia kuti kavu, kwa sababu ya kuwa kwake independent (mtu asiyefungamana na upande wowote) wakati wa harakati za kutafuta mgombea urais wa Tanzania ndani ya chama chao. Hali hiyo ndiyo ambayo imesababisha ageuzwe mbuzi wa shughuli, akichanwachanwa kila upande,” alisema mwanasiasa mmoja maarufu aliyezungumza na Tanzania Daima kwa sharti la kutotajwa jina.

Kwa mujibu wa mwanasiasa huyo, Magufuli alianza kuandamwa tangu Mkapa akiwa madarakani, hoja zilizokuwa zikielekezwa kwake zikiwa ni zile za kumhusisha na uamuzi wa serikali wa kuuza nyumba zake kwa watumishi waandamizi wa umma, zoezi ambalo lilisimamiwa na Wizara ya Ujenzi aliyokuwa akiiongoza.

Ingawa uamuzi wa uuzaji huo wa nyumba ulifikiwa kwa pamoja na Baraza la Mawaziri ambalo Magufuli alikuwa miongoni mwao, kama walivyo Rais Kikwete (aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa), Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohammed Shein na Waziri Mkuu Edward Lowassa, bado mashambulizi yanayohusu hatua hiyo ya serikali yalimlenga mwanasiasa huyo pekee.

Habari zaidi zinasema kwamba, mashambulizi makali dhidi ya Magufuli wakati huo yalikuwa yakilenga zaidi katika kumuondoa kutoka miongoni mwa wagombea urais, jambo ambalo yeye mwenyewe alilifanya.

Ingawa Magufuli mwenyewe hajawahi kueleza bayana sababu hasa zilizomfanya kutogombea urais mwaka jana, watu wanaofuatilia siasa za Tanzania wamekuwa wakihusisha uamuzi wake huo na dhamira yake ya kujali kwanza maisha yake, baada ya kunusurika kifo kutokana na kulishwa kitu kinachodhaniwa kuwa sumu miaka michache iliyopita.

Sababu nyingine zinazohusisha uamuzi wake huo, pamoja na jina lake kuwa miongoni mwa watu waliokuwa wakitajwa sana, ni nia yake ya kutokuwa tayari kuingia katika mzozo, kashfa na shutuma na makundi yaliyokuwa yamejiandaa kufa na kupona kuhakikisha wagombea wake wanashinda kinyang’anyiro hicho.

Kundi lenye mtazamo tofauti na huo ni lile ambalo limekuwa likimuona Magufuli kuwa mwanasiasa mjanja, ambaye amekuwa akitumia kivuli chake cha utendaji kazi uliotukuka kuficha madhambi yake kadhaa ya kimaamuzi ambayo sasa ndiyo yanayoanikwa hadharani.

Habari kutoka kwa watu wenye mtazamo huo wanasema, wakati wote alipokuwa Waziri wa Ujenzi, Magufuli alifanya maamuzi mengi ambayo kimsingi yalikiuka misingi ya taratibu za kikazi na kiutendaji.

“Watu hawamjui Magufuli. Siku zote wanamuona kuwa mtu mchapakazi na mwadilifu, wakati ukweli hauko hivyo. Nenda Wizara ya Ujenzi ukawasikie watu wanaomfahamu,” alisema mmoja wa watu asiyekubaliana kiutendaji na waziri huyo.

Hata hivyo rekodi ya utendaji ya Magufuli ambayo ilimfanya awe mmoja wa mawaziri vipenzi wa Rais mstaafu Mkapa, ni uamuzi wake wa kusimama kidete katika kuendeleza miundombinu, hasa barabara, kuendesha kwake vita kali dhidi ya vitendo vya rushwa na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora miongoni mwa makandarasi, maofisa wa mizani na wale wa Tanroads.

Kama hiyo haitoshi, uamuzi wake wa kuhakiki magari ya serikali, ikiwa ni pamoja na kusimamia matumizi yake na hata usajili wake ambao uliokoa magari mengi yaliyokuwa hatarini kupotelea mikononi mwa watumishi wa umma wasio waaminifu wakati akiwa Waziri wa Ujenzi, ni jambo jingine lililomjenga kisiasa, sambamba na kumuundia maadui wengi.

Aidha, uamuzi wake wa kumshauri Rais mstaafu Mkapa kuanza kutenga kiasi cha fedha kutoka katika sehemu ya mapato ya ndani kwa ajili ya kuendeleza miundombinu pasipo kuwategemea wafadhili, ni moja ya mambo yaliyomjengea kuaminika kwa Rais wake na hata kwa viongozi wa nchi jirani, akiwamo aliyekuwa Waziri wa Ujenzi na Nyumba wa Kenya, Raila Odinga.

Pengine pia uamuzi wake wa kuwafutia leseni makandarasi zaidi ya 1,000 waliokuwa wakilalamikiwa kwa ukiukwaji wa taratibu za kazi na utengenezaji wa miundombinu chini ya kiwango, ni jambo jingine ambalo lilimjengea haiba ya utendaji uliotukuka, miongoni mwa wananchi na hata viongozi wenzake serikalini.

Kwa bahati mbaya, sifa zote hizo taratibu zilianza kugeuka shubiri kwake na wakati fulani alipokuwa akihudhuria Bunge la Jamhuri ya Muungano, alianguka ghafla na akakimbizwa Ujerumani kwa ajili ya matibabu ambayo baadaye ilikuja kubainika kuwa alikuwa amewekewa sumu katika chakula.

Hali hiyo ilizaa wasiwasi ambao hatimaye ulisababisha serikali ilazimike kumpatia ulinzi aliodumu nao hadi ulipokuja kuondolewa mwanzoni mwa mwaka huu, kwa maelezo kwamba kulikuwa hakuna sababu za msingi wala tishio lolote la maisha yake.

Pamoja na rekodi yake hiyo, Magufuli kwa kufahamu au kwa kutojua, alijikuta akiingia katika mtego wa kimaamuzi ulioshirikisha Baraza la Mawaziri, pale wizara yake (Wizara ya Ujenzi) iliposimamia kazi ya uuzwaji wa nyumba za serikali kwa watumishi wa juu wa umma.

Uamuzi huu ambao Magufuli alisimama akautetea kwa nguvu zake zote, si tu kwamba ulimpunguzia heshima yeye binafsi kama msimamizi mkuu wa ajenda hiyo, bali pia uliiharibia sifa nzuri ya kuwatumikia watu Serikali ya Rais mstaafu Mkapa.

Habari zaidi zinasema kwamba, kundi linalomwandama Magufuli hivi sasa, litakapomaliza kazi hiyo au hata kabla halijamaliza, linaweza likaanza kutekeleza mkakati B, wa kumchimba Mramba katika mwelekeo huo huo.

Chanzo kimoja cha habari cha Tanzania Daima kimeeleza kwamba, Magufuli na Mramba wanaweza tu kunusurika na zahama za kisiasa zilizowahi kuwakuta wanasiasa kama Hassy Kitine, Profesa Simon Mbilinyi na Iddi Simba za kujiuzulu uwaziri iwapo tu Rais Kikwete atasimamia kauli yake aliyoitoa mara kadhaa kwamba urais wake hauna ubia na mtu mwingine yeyote.

Soma magazeti yajayo ya Tanzania Daima kujua undani wa sakata zima linalomgusa Magufuli na mwenendo wa mambo serikalini.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments
  • Comment #1 (Posted by bitariho)
    Rating
    Article nzuri sana
     
Submit Comment


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.