Habari Tanzania - http://www.habaritanzania.com
Bush ni pacha wa Baba yake
http://www.habaritanzania.com/articles/1332/1/Bush-ni-pacha-wa-Baba-yake
By Salehe Mmoro
Published on 10/14/2006
 
KATUNI ya gazeti la Newsweek la Septemba 12 mwaka jana, ilimwonyesha George W. Bush (Namba 43 White House) akipiga simu kutaka maafa ya janga la katrina, New Orleans , yakabiliwe kijeshi.

Na Mwandishi wa HabariTanzania.com, Dar es salaam



KATUNI ya gazeti la Newsweek la Septemba 12 mwaka jana, ilimwonyesha George W. Bush (Namba 43 White House) akipiga simu kutaka maafa ya janga la katrina, New Orleans , yakabiliwe kijeshi.

Si hoja majanga kama tsunami au katrina kukabiliwa kijeshi. Lakini mchoraji, Walt Handelsman, alimchora Bush akisema: “Tunataka vikosi  zaidi New Orleans ”. Basi, wanajeshi maelfu walioko Iraq vitani, kila mmoja akapaza sauti kubwa kusema, “Nichukue miimiii!!” Wamechoshwa na vita.

Kamwe vita ya ugaidi; au mihimili ya uovu, haviongozwi na mtu baki-kapuku,asiyeweza hata kuvurumisha dege hadi Kabul, Beirut, Pyongyang, Baghdad au popote walipo ‘martyrs’ mashahidi wa Jihad, wanaojitoa mhanga kupinga ubeberu wa Magharibi na mapokeo ya dini za mabwanyenye.

Kwake, Namba 43 ambaye hukalia kiti cha enzi cha ngozi nyeusi katika ofisi ya umbo la yai (oval), The White House,kila jambo hukabiliwa kibabe.

Majuzi nilipoandika kwamba Rais Bush aliyealikwa na Rais wetu, Jakaya Kikwete, kuja nyumbani Tanzania ni mwanajeshi, nilipigiwa simu, zingine za jazba na bezo kuwa nitoe ufafanuzi kuwa lini Bush alikuwa mwanajeshi? Si kwamba alikuwa rubani tu?

Alipohitimu Historia katika Chuo Kikuu cha Yale, ambacho hata baba yake alihitimu 1948, alikwishaota uana jeshi. Wiki mbili kabla ya Mahafali, W. Bush alikwenda katika ofisi za Jeshi la Anga (Texas Air National Gurd) akajiandikisha kufanya mafunzo ya urubani.

Nia yake ilikuwa kujifunza kuvurumisha dege la vita kama baba yake alivyofanya wakati wa vita vya Pili vya Dunia, baada tu ya kuhitimu masomo yake katika chuo hicho hicho cha Yale. Bush Baba, George Herbert Walker Bush (72) alituma majeshi Desemba 1989 kule Panama na kupindua serikali na kumkamata mateka kiongozi wa nchi hiyo,Jen. Manuel Noriega.

Aliingilia ugomvi wa Iraq na Kuwait Agosti mwaka 1990, akairejesha Kuwait mikomoni mwake, baada ya mashambulizi ya siku nne, yaliyosababisha wanajeshi wengi kujeruhiwa na uchumi mbovu uliokuja kurekebishwa na rais Bill Clinton.

Alidhoofisha Dola la Urusi (USSR) na kumfanya Mikhail Gorbachev kujisalimisha mikononi mwake mwaka 1989. Naam, Bush na baba yake ni wataka shari… ni pacha.

W. Bush mtukutu, aliyewahi kutiwa mbaroni na polisi mwaka 1976 kwa kuendesha gari akiwa amelewa chakari, alikuwa rubani 1968 hadi 1973.

Akatunukiwa cheo cha Luteni usu ( Second Lieutnant) na kufanya kazi kwa miaka miwili akivurumisha dege la kivita, F- 102 Fighter.

Bush, alirejea kila kitu katika historia ya baba yake. Ameendesha dege la vita, amefanya biashara ya mafuta na madini na amepigana vita na kupindua serikali za nchi nyingine, kama alivyofanya Bush baba.

Amempindua Saddam, Mullah Muhammad Omar wa Wataleban, yuko mbioni kumpindua Ahmadenajad na wenzake wasio mtii kama Hugo Chavez!

Miaka minne baadaye, alikuwa akivurumisha madege hayo ya F-102 kwa mkataba wa muda maalum.

Wakati huohuo alikuwa akifanya kazi katika kampuni ya Mbia wa baba yake, ya uchimbaji mafuta, kilimo na ufugaji huko Houston . Ndiyo maana nikasema katika makala iliyotangulia kuwa ni mfanyabiashara kitaaluma, na ni mwana jeshi.

Naam, huyu ndiye Luteni usu, mpangaji wa 43 wa White House, ambaye anakuja Tanzania kujaribu kujifunza Qur’an ya upendo, amani na utulivu katika madrassa za kiasili, katika mbuga za Serengeti, Manyara, Mikumi, Ngorongoro ama Mlima Kilimanjaro, penye chemchemi za upendo wa Mungu.

Ambako ndege, swala, simba na nyoka hunywa maji pamoja! Akija: Bush na mama Laura, wakipenda,waweza kufanya maadhimisho ya 30 (mwaka mmoja kabla) ya ndoa yao , “Diamond” katika moja ya vivutio vyetu.

Novemba 5 mwaka 1977 ndiyo siku waliyofunga ndoa. Maadhimisho hayo ya 30 katika utamaduni wa Kimarekani, pengine huitwa, ‘ Pearl ’.

Na yanaweza kufanywa mwakani. Wengine hawataki kuamini kuwa hapa Tanzania kuna vivutio ambavyo katika ulimwengu mwingine hakuna…vivutio vinavyoweza kuwapa mapumziko ya amani watu maarufu kama rais Bush wa Marekani.

Kwao, kila Paradiso iko Ughaibuni, au ‘Majuu’ kama wanavyoita. Hawa ni watumwa wa kasumba za ukoloni mkongwe na mamboleo. Watabaki watumwa milele, kwa kuwa myoyo yao ilikwisha lowea ugenini!

Ndiyo maana wanaona kuvaa nguo yenye maandishi, “Ilove Ngorongoro” ni ushamba. Wanavaa zili zenye maandishi, “ London Motuary Attendant”. Lo!!

Rais George W. Bush anaweza kufuatana na mabinti zake wawili: Jenna na Barbara. Jenna pia ni jina la mama mzazi wa Laura Welch Bush, na Barbara ni jina la mama mzazi wa Bush, ambaye pia ni “First Lady” mstaafu.

Laura ana taasisi ya kuhudumia yatima na wagonjwa wa Ukimwi kama ile ya Bill Clinton. Kwa kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi fukara, yenye matatizo yote mawili,ujio wa Bush na mkewe hapa ungekuwa wa faida ya kiwango cha juu..

Ziara hiyo isingekosa changamoto kwa Tume ya Kudhibiti Ukimwi, TACAIDS, kupambana kwa ufanisi na ugonjwa wa ukimwi, kuwasaidia wagonjwa wa ukimwi, kukemea utapeli wa NGOs za Ukimwi, na kusaidia kuondoa unyanyapaa.

Ujio wa mabinti wawili wa Bush, pia waweza kugeuka changamoto kwa Watanzania, kwani mbali na kuweza kuhamasisha vita dhidi ya madawa ya kulevya, watoto wa mitaani, ombaomba au hata tatizo lolote, wanaweza kuanzisha taasisi za kukabiliana na mifumo mibovu inayosababisha majanga ya kijamii, kama ujinga, vita, ukimbizi, maradhi, uharibifu wa mazingira au wakamwongezea nguvu mama yao kutuunga mkono katika vita dhidi ya ukimwi.

Kwa kusema hivi, najibu maswali kwamba mke wa Bush amekujaje katika ziara ya mumewe? Na binti zao wameingiaje katika mjadala huu wa ujio wa Bush?

Leo katika Tanzania , wapo watu wanaojidai kupambana na ombaomba, sijui wazee, watoto wa mitaani na ukimwi, kumbe wanajineemesha tu na kushibisha matumbo yao kupitia migongo ya wagonjwa hata mahututi wa ukimwi!

Haohao ndiyo hawapendi ziara za watu wa haki kama Mama Laura Bush, au Clinton , ambazo kwa vyovyote zitafukua unafiki na unyama wao dhidi ya waathirika.Naam, wanaanzisha NGO kwa nia ya kuganga njaa zao, wala si kupambana na tatizo. Ni wakali wanapoambiwa ukweli; wanataka wasifiwe wakati hawana tofauti na vibaka wanaopora maiti.

Wapo watu wanaohoji: Ziara ya Bush Tanzania , inahusishwaje na umasikini wa Watanzania? Wanataka kusema kuwa matatizo ya Waafrika, ni shauri yao ! Juzi rais Jakaya Kikwete alipokuwa Marekani alifanya mazungumzo na Bush. Kwa nini Bush alimuuliza rais wetu juu ya ‘kelele’ za joto la kisiasa Kenya ? Kwa nini Bush anafuatilia migogoro Afrika?

Marekani ni polisi au nyapara wa dunia. Nguvu zake za kijeshi, kisiasa na kiuchumi ndizo zinazoifanya nchi hiyo kuwa hivyo. Huchangia zaidi ya asilimia 30 katika misaada ya majanga duniani, vikosi vya kulinda amani, fedha za kuendesha shughuli za umoja wa Mataifa, utiaji saini mikataba ya amani n.k.

Hata mishahara ya wanajeshi wa Umoja wa Afrika (AU) ya kulinda amani DR Congo, Darfur , Somalia na kwingineko, lazima ilipwe na Marekani, na wala si nchi yoyote ya Afrika!

Marekani ni baba wa Dunia. Kwa mtu aliyesoma kidigo tu, hatakosa kuona kwa nini nimesema katika makala yangu iliyotangulia kwamba rais katili wa Marekani, asiyejali shida za Waafrika, ni janga kama yalivyo majanga kama katrina, tsunami, ukimwi na njaa.Watu wanafunga na kukesha ili kila baada ya miaka minne, Marekani impate rais mcha mungu; na si katili mpenda shari. Rais mwema wa Marekani ni baraka kwa dunia.

Rais mwanzishaji wa vita ni kitisho kwa ulimwengu. Vita vya Vietnam (1962-70) viliua watu 500,000; na kila siku viliigharimu Marekani Dola milioni 77. Kwa mwaka, Dola Bilioni 28 zilitumika vitani. Je, Watanzania wanajua vita dhidi ya Iraq , Afghanistan , Mashariki ya kati na popote Marekani inapopigania maslahi yake, huathiri chumi zetu kwa kiwango gani?

Vita husababisha watu wangapi kupoteza makazi, maisha, mali na huzalisha mabaa kiasi gani, magonjwa na wakimbizi? Biashara ngapi za watu, hata kama ni uuzaji wa vinyago Tanzania , na utalii huvurugika nyakati za vita ya Marekani au Uingereza na mataifa mengine?

Bei ya mafuta hupanda kwa kiwango gani, na kuathiri chumi za nchi changa kama Tanzania ? Ni kwa sababu hii sisi wanyonge hamtutaki rais Mbabe kutawala Marekani!

Katika vita vikuu vya kwanza vya Dunia (1914-18) wanajeshi 8,418,000 walikufa, wakiwemo Wamarekani 126,000. Raia waliokufa kutoka mataifa mbalimbali ikiwemo Tanzania ni 1,300,000.

Katika vita vya Pili (1939-45) wanajeshi 16,933,000 wakiwemo hata babu zetu, walifia vitani tangu Burma, India, Ethiopia na hata Ulaya. Walimwaga damu kutetea maslahi ya Malkia wa Uingereza! Wamarekani waliokufa ni 292,000 wakati raia wa mataifa mbalimbali 34,305,000 walikufa.

Vita vya Ghuba vilivyoanzishwa na akina Bush vimeua wangapi na kupandisha bei ya mafuta kwa kiwango gani? Kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta, vitu vidogo tu kama viberiti na huduma kama usafiri, umepanda kwa kiwango gani?

Kuna vita vya Balkans, vita vya Mashariki ya kati na hata tetesi tu za vita Iran , Syria , Korea Kaskazini n.k huvuruga uchumi wa dunia kwa kiwango gani? Lazima nchi masikini zichukie vita hata vya magaidi, ambavyo huzuia misafara ya watalii inayotuingizia faida.

Hatutaki vita, tunataka faida kutokana na biashara za haki katika masoko ya dunia. Nchi fukara zinachelea rais mbabe wa Marekani anapoapishwa Januari 20 ya mwaka wa nne, wa Uchaguzi wa taifa hilo la watu zaidi ya milioni 270.

Kwa upande mwingine rais wa taifa babe kama Marekani anapotembelea jamii za watu fukara walionyonywa na mifumo ya kibepari, inayochota rasilimali zao kama sangara, madini,mazao ya kilimo, misitu n.k anaweza kuingiwa na roho mtakatifu, badala ya ‘roho mtakavitu’. Ndiyo maana nikauliza katika makala yangu ya kwanza: Bush yupi atakuja Tanzania :

Mfanya biashara au Dracula? Bila shaka tunahitaji asiwe katika makundi yote ya faida za maguvu ya kijeshi au chumo la kibiashara lililozingirwa na mikataba ya kinyonyaji, bali awe mtu mpenda wanyonge kama Bill Clinton, James Earl Carter, Franklin Delano Roosevelt na Abraham Lincoln aliyeamuru watumwa kuwa huru baada ya vita.

Dunia haitaki vita, bali amani.Kamwe wanyama wa mwitu kama Serengeti hawajawahi kuua watu kwa maelfu kama silaha za vita, au mashambulizi ya kigaidi kama ya Osama Bin Laden, anayetetewa hata hapa Tanzania kuwa si fungu moja na Adolf Hitler…Osama ni nani kama si mwuaji wa watu
5,500 walioteketea Septemba 11, 2001?

Mwisho, Tanzania ni kisiwa cha amani. Pamoja na unyonge wake kiuchumi, kulinganisha na Marekani, ni shule pekee ya kufundishia mithili ya madrassa, watawala wababe wa ulimwenguni, ambao nao wamelevywa mafundisho ya itikadi kali ya kuua, wakati huohuo wakijidai kumtumikia Mungu wao, awe Allah, Yahweh, Adonai, nyoka au hata vyura, muradi hii miungu isiyotaka amani inatuletea mateso , uharibifu wa makazi, ufukara, ukimbizi na kila dhiki.

Wote wanaounga mkono vita na wafanya vita hawana Mungu wa kweli, maana tunda la roho wa Mungu ni Upendo, Upole, utu wema, amani ,uvumilivu dhidi ya mabaya, ndiyo kuwaombea adui, na kukabiliana na tofauti kwa njia ya mazungumzo, na kamwe si vita.

Kamwe Watanzania msishangae, baada ya ugeni wa Bush hapa, akautangazia ulimwengu kuacha Operesheni zake za kijeshi duniani, na badala yake Luteni usu mtukutu wa jeshi, akatumia gharama hizo kusaidia jamii masikini, kupitia somo analoweza kupata katika “madrassa” za amani na utulivu!!

omybabu@yahoo.com