Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Salehe Mmoro  »  Ni Kweli, Katika msafara wa Mamba na Kenge wamo.
Ni Kweli, Katika msafara wa Mamba na Kenge wamo.
By Salehe Mmoro | Published  10/14/2006 | Salehe Mmoro | Rating:
Na Mwandishi wa HabariTanzania.com, Dar es salaam

MWAKA 1831, Seneta wa New York , William L. Marcy aliwahi kusema wakati wa majadiliano katika Bunge la Congress kwamba mshindi (wa uchaguzi) huja na majahili na mafisadi!

Maneno hayo hueleza bayana kwamba mfumo wa uharibifu huja serikali mpya inapowateua wafanyakazi watakaoisaidia kuendesha shughuli zake.

Kila mara, utawala mpya unapoingia madarakani, mamia kama si maelfu ya watumishi wapya wa umma wanapoteuliwa kushika nyadhifa , baada ya wale wa zamani kuenguliwa, aghalabu nafasi hizo huchukuliwa na kundi lililoshinda uchaguzi.

Na kwamba, aghalabu mabadiliko hayo hayaandamani na kujali kwamba wateuliwa wanao uwezo wa nafasi walizopewa au hata uzoefu.

 Matokeo: ufanisi wa serikali iliyoingia madarakani, huwa duni; ndiyo maoni ya Seneta huyo kuhusu serikali mpya.

Wapo wanaokasirika na kuzua visasi baada ya kutoteuliwa kushika nafasi yoyote katika serikali mpya. Mwaka 1881 rais James A. Gerfield wa Marekani aliuawa kwa risasi na mmoja wa waliokuwa wakitafuta nafasi ya ulaji katika serikali mpya. Nitajadili hili baadaye kidogo.

Naam. Ukichungulia kwa makini katika jamii ya Kitanzania leo, miezi takriban kumi na moja baada ya serikali ya Kasi Mpya kuingia madarakani, Desemba mwaka jana, hutakosa kuona waharibifu waliofanikiwa kujikweza katika serikali hii mpya.

Hawana jipya; bali wamo mradi wamekuwemo katika mfumo ulioshinda uchaguzi. Pengine wamekuwemo katika mfumo wa utumishi wa umma kwa bahati, kwa kujuana au kwa vyovyote vile viwavyo.

Hawana uchungu na hali ya wapiga kura, wala hachomwi dhamiri zao juu ya ahadi zilizomo katika ilani ya uchaguzi, zinazopaswa kutekelezwa katika kipindi kifupi cha miaka mitano.Kwao, kila kitu ‘shegha’ maadam wanalipwa mshahara!

Katika Tanzania , kuna ahadi nyingi zilizotolewa na Rais Jakaya Kikwete; lakini ‘Baba wa yote’ ni hii ya Maisha Bora kwa kila Mtanzania. Ahadi hii ni kubwa na ni kitanzi cha shingoni dhidi ya utawala huu, kama haitatekelezwa hadi wakati wa kikao cha Bunge la Bajeti cha Juni 2010.

Ndiyo maana serikali sasa, hususan rais Jakaya Kikwete mwenyewe leo yuko makini kufanya semina elekezi kwa watumishi wa umma, ili kung’oa magugu: uzembe, tabia ya wizi, rushwa, ufisadi na watumishi wa umma kutowajibika kwa wananchi.

Hawa wote, wakiwemo wanywa gongo, wavuta bangi, wabwia unga, vibarua, wasukuma mikokoteni, walala hoi na makabwela walio vijiweni, “kula-kulala” na wakulima na wafanyakazi wameahidiwa maisha bora…kila Mtanzania, pasipo kujali kuwa ana tabia gani!

Serikali imekwisha andaa utekelezaji wa mpango (Road Map) wa kuboresha maisha ya Watanzania wote; wakiwemo omba-omba tunaowapita vibarazani leo, watoto yatima wanaoranda mitaani na kuvuta bangi, gundi, petroli, kunywa pombe na kisha kukwapua mali za wananchi usiku na mchana, nao wamo katika ahadi hii kamambe.

Hii ni kusema kwamba, safari hii watumishi wa umma wana kazi ya kujisafisha: Kuacha mazoea, wizi au udokozi wa mali ya umma, kama si rushwa uzembe, rushwa na ufisadi, na kutafakari namna ya kuboresha maisha ya Watanzania, wakiwemo hao wanaolala vibarazani.
Ziko changamoto bila shaka katika utekelezaji.

Lakini, kwa kuwa upo usemi kwamba bila utafiti mtu asijitie kuzungumza,( No research, no right to speak) tuna hakika ahadi ya maisha bora kwa kila mtanzania, ni hakika; ni bayana kutokana na tafiti za kina zilizofanywa, ili kutekelezwa katika kipindi cha miaka minne iliyosalia ya utawala wa awamu hii.

Ni kwa sababu hii tunadhani kila mtumishi aliyesalia katika utumishi wa umma, amechunguzwa na kuhakikishwa kuwa anaweza kuwa chombo cha utekelezaji wa ilani na ahadi zake nyingi, yakiwemo majumuisho ya maisha bora kwa kila mtanzania, bila kujali hali aliyo nayo sasa.

Tumeanza kuona sheria zikibadilika, tozo, kodi na malipo ya mirahaba ya maliasili kama madini, zimeanza kubadilishwa, ili wawekezaji walipe stahili. Pia mashirika ya umma tuliyosema yanawanufaisha wageni yanafanyiwa ukarabati ili kuongeza kasi katika mwendo kuelekea Tanzania yenye neema, ambayo rais amethibitisha inawezekana.

Tumesikia rais na hata Waziri Mkuu, wakitangaza ole kwa watumishi wasiotaka kuwajibika; wasiotaka kutekeleza ahadi ngumu zilizotolewa tangu vijijini, majimboni na hata kitaifa.

Kama nilivyokwishatangulia kusema, katika msafara wa mamba na Kenge wamo! Kwamba katika kikosi cha wateule wa rais, Mawaziri, Naibu mawaziri, Makamishna, Wakurugenzi, wakuu wa wilaya, mikoa, Majaji na wengineo waweza kuwemo waharibifu watakaoufanya umma kulia kilio cha uchungu kwamba, heri tunakotoka, kuliko tunakokwenda, kheri mkoloni, n.k.

Dalili za kuwa tambua kenge zimenza kuonekana tayari; ambako hata sasa wapo mawaziri wanaotia mashaka kama wataufikisha umma wa Watanzania katika nchi ya ahadi.

Wamechoka; hatua waliyokuwa nayo enzi za “Ukweli na Uwazi” zimefifia, haieleweki kama ‘kasi mpya’ wataiweza, au watabebwa katika mbeleko hadi mwisho wa safari mwaka 2010.

Wapo waliaoanza kudaiwa kutumia madaraka vibaya, waliojenga kwao kwa fedha za walala hoi, wenye migongano ya kimaslahi (conflict of interest), walioanza kukimbia vivuli vyao wenyewe, walioanza kulipa visasi kwa sababu tu wameulizwa juu ya utusitusi na mashaka yaliyomo katika viti wanavyokalia n.k.

Kama hawa si kenge katika msafara wa mamba, ni Wamisri waliowafuata Waisraeli kwa kuogopa mapigo kumi ya Mungu dhidi ya Wamisri, na tamaa ya ulaji!

Wapo waliokosa nafasi katika serikali hii ambao wako pembeni wakichekelea kila baya linapotokea. Wako tayari kuvuruga au kuwekwa vizingiti ili mafanikio yasije, lengo lao likiwa ‘kunenepesha donge’ walilonalo myoyoni, baada ya kutupwa nje, au ili wapate cha kulaumu mwisho wa wakati.

Hakuna tofauti kati ya kumuua kiongozi aliyeko madarakani kwa sababu ya kutomteua muuaji , na kukwamisha mafanikio ya serikali dhidi ya wananchi. Hapa kuna choyo kijicho, kulipa visasi, ubinafsi na roho mbaya.

Hakuna uzalendo, bali kufikiri matumbo yao , watoto wao na jamaa zao. Hawakubali kupoteza roho moja ( yao ) kwa ajili ya taifa lao, Tanzania , ila wapate, wale wanywe na kushiba wakati wengi wakiteseka mitaani kwa sababu ya maisha mabaya.

Hawa ni mchwa walao jahazi wakati wa safari katika bahari yenye mawimbi makali ya uchumi, kama mgao wa umeme, kuporomoka kwa thamani ya shilingi, ukame, njaa, kushuka nwa bei za mazao, wizi na utapeli dhidi ya rasilimali zetu na ukosefu wa usawa katika bishara ya kimataifa.

Mbali na haya, kuna mafisadi kama kenge walioandamana na mamba, ambao kama hawatabainishwa mapema na kuondolewa, maisha bora kwa kila Mtanzania, utabakia wimbo.Wao kazi yao ni kutekeleza demokrasia na uzalendo wa matumbo yao, bila kujali kitakachotokea, ahadi zikishindwa kutekelezwa.

Upo uharibifu wa mazingira bora ya kilimo cha kisasa, ambacho rais aliahidi kuwanufaisha zaidi ya asilimia 80 ya wanaoshi vijijini. Urutubishaji wa ardhi, kuhifadhi misitu iletayo mvua, utunzaji wa vyanzo vya maji kama mito , maziwa, chemichemi.

Kuachana na kilimo cha kikale kinacholeta mmomonyoko wa udongo, kuboresha viwanda vidogo maeneo ya mashambani na vijijini, utekelezaji wa Mkukuta na Mkurabita kwa moyo mmoja, uboreshaji wa bodi za mazao na kuwatimua au kuwafunga jela wezi wa ushirika na mali za wakulima.

Kwa kuwa watanzania wengi ni wakulima wa pamba, korosho, pareto, kahawa n.k serikali haina budi kuwaondoa dumuzi wanaokula faida wanayopata. Kwa muda mrefu, wadudu wengine wamekuwa wakinyunyiziwa sumu na kufa, ili kupisha chumo, lakini hao dumuzi-watu hawajashughulikiwa ipasavyo!

Serikali ya kasi mpya inapaswa kuwatia mbaroni, badala ya kukalia kuwaonya kwa maneno kuwa warejeshe mali za wakulima au za ushirika. Wana masikio lakini hawasikii; macho wanayo lakini hawaoni.

Kama watanzania wote wako sawa katika sheria, wapo vigogo wanaozungukwa na riha mbaya ya uporaji wa mali ya umma, lakini hawajachukuliwa hatua. Badala yake, tunawaona polisi wakiwasomba wezi wa kuku, wanywa gongo, wezi wa mifukoni na wazururaji wakijaza magereza yetu, wakati walioiba mabilioni wakiendelea kuishi peponi!

Hapa, kuna usawa au haki kweli katika sheria? Au mahakama ziliwekwa kwa ajili ya watu masikini, lakini matajiri wanapoitendea jamii jambo baya huogopwa na sheria kupindishwa. Huku ni kurutubisha makundi ya walio nacho na wasio nacho au hata ubaguzi wa rangi na ukabila katika nchi.

Tunategemea waliopora mali ya umma kwa kutumia nafasi zao wanakamatwa haraka na kupewa adhabu zinazowastahili. Kamwe serikali hii iepuke mtindo wa kulindana ambao haukosi kuwa mwiba mchungu dhidi ya utekelezaji wa ilani na ahadi.

Hata sasa tumeona watumishi hususan wa Halmashauri za miji, majiji na wilaya wakihamishwa kutoka sehemu moja kwenda nyingine, licha vilio vya umma kuwa walibadhili fedha mahali walikotoka.

Haiingii akilini kama Waziri husika hakujua juu ya tuhuma zao au ndio kulindana kirafiki na kikabila. Je, kumhamisha mwizi toka kituo A. kwenda B, au C, kutamfanya kutubu? Au ni kusambaza uoza toka kituo kimoja kwenda kingine? Ni kuweka mvinyo mpya katika viriba vya zamani?!

Haiingii akilini kuwa Wakurugenzi 20 tu waliosimamishwa kazi na kufunguliwa mashitaka ndio walioziibia Halmashauri, wakati hadi leo miradi yote ya umma imeliwa tangu Tanga hadi Kigoma, Dar es salaam hadi Musoma! Wengine wamejiuzia nyumba za halmashauri bila hata madiwani kujua, lakini hakuna anayewagusa! Ni ni miungu(sacred cows) katika jamii ya kifalme?

Ukiacha hao, wapo watumishi wa umma, ambao bila kuwapa rushwa hawakutazami. Wakati kasi mpya ilipoingia madarakani, walibadilika. Siku zilipozidi kwenda, wakarejea katika ulevi wao wa kawaida. Leo bila fedha hata hospitalini, hakuna wa kukutazama. Badala yake Watanzania wanaendelea kufia hata vyumba vya upasuaji, kwa kukosa 120,000.

Kumwona Daktari ni kati ya 20,000 hadi 50,000. Maisha bora kwa masikini yatakujaje hapa, bila kupambana? Hawa wana zahanati zao mitaani; wanatumia hata vifaa vya hospitali za umaa kufanya operesheni mitaani.

Kuna wanaotumia hata magari ya umma kusomba nyasi za ngombe wao, kupeleka wake au hata nyumba ndogo saluni, na wakati mwingine husubiri vigogo baa hata usiku wa manane, wakati Wajawazito wakipoteza maisha kwa kuchelewa kufika hospitali.

Wako wengi, wizarani, katika mashirika ya umma, sekta binafsi zinazotoa huduma za uwakala; naam hawa ni kenge katika msafara wa mamba! Shime wasipewe muda ili wabadilike!

Je, chui hubadili madoa-doa yake na kuwa mbuzi? La hasha! Na muda uliosalia ni mdogo tu, kila Mtanzania atapata maisha bora ifikapo Juni 2010 wakati wa bajeti ya mwisho?

omybabu@yahoo.com


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments
  • Comment #1 (Posted by mkuu)
    Rating
    very excellent nashindwa kuongeza nisije kuharibu
     
Submit Comment


Article Options
This article has been added to your 'Articles to Read' list.
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.