Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Mwamuenzi Nyerere kwa midomo bila vitendo?
Mwamuenzi Nyerere kwa midomo bila vitendo?
By Habari Tanzania | Published  10/14/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated

NASEMA haiwezekani haya yote yatokee kisha wote tuweke gundi mdomoni. Iwezekaneje ninyi mfanye yasiyo ya kawaida bado tusigutuke wanakwetu? Hata kama ni laana, hii ya sasa nakuapia imevuka mipaka wandugu. Kwani msipofanya vituko ninyi hampati raha wanakwetu? Nasema ipo namna, simo!

Kila mtu anajidai kumpenda na kumuenzi sana huyo mzee wetu sio? Kumuenzi mzee wa watu bila kuiga mazuri yake bado tusiite huo ni unafiki? Wanaomuenzi Mwalimu si wangeenzi na yale aliyoyasimamia jamani?

Eti, kila kona mwathubutu kutamba kwamba mwaadhimisha miaka saba ya msiba wa Mwalimu bila kuhofu ni mangapi mnayoyafanya kiasi cha kumgeuza huko kaburini alikopumzika? Nasema hatuwezi kufumba vinywa mwanakwetu. Tutasema tu hata kama hatumo katika hayo.

Eti mwamuenzi Nyerere kwa kuendekeza hizo siasa za kubaguana? Anayebisha siasa hizo hazipo na anyooshe kidole. Kwani tuliyokuwa tukiyasikia ndani ya chama tawala wakati wa mbio za kuwania Ikulu ni kitu gani kama kwenu huo sio ubaguzi? Nasema simo kabisa mwanakwetu. Mwasahahu wakati huo mlifika hadi mahali mkaanza kuuliza ni yupi alikuwa chama gani kabla ya mapinduzi matukufu? Eti hamkuwahi hata kuona dalili za ubaguzi wa rangi zikinyemelea kinyang’anyiro cha urais? Kwa mtaji huo hao waliofanya hivyo leo wanathubutu kutamka eti wanamuenzi Mwalimu? Nasema simo katika haya yote mtoto wa watu.

Na hayo ya mpasuko wa kisiasa huko Visiwani mtathubutu kuyapinga wakati bosi wa nchi keshasema mpasuko upo? Eti ni Nyerere yupi wanamuenzi huko Visiwani ikiwa wameshindwa kuleta siasa za maridhiano? Nauliza, Shamhuna leo atathubutu kusema yeye ni mfuasi mwaminifu wa Mwalimu ikiwa ni kweli amenukuliwa akisema serikali ya mseto haipo? Iwezekane kweli kwake ni heri mpasuko wa Unguja na Pemba uendelee kuwepo kuliko kuwa na mseto wa serikali? Naomba iwe alinukuliwa vibaya. Vinginevyo wanamuenzi Nyerere mwingine si huyu tunayemjua.

Na haya ya kukataa kuhamia Dodoma nayo mwayaweka fungu gani? Eti si mlikula viapo mkisisitiza kusimamia yote aliyosimamia huyu baba wa Kizanaki? Kwani yeye aliposema makao makuu yahamie Dodoma alimaanisha mjenge nyumba mpya za mawaziri Dar es Salaam? Mbona mwafanya mambo juu-chini, chini-juu kisha bado mwajitia kumpenda na kumsifu huyu Baba wa Taifa? Nasema mimi simo katika haya yote.

Mwataka kuniambia kwamba mnayofanya katika elimu leo ndio yale aliyofanya Mwalimu au walau ambayo angependa kuyaona yakifanyika? Eti ninyi mliovaa masuti yenu na kukalia afisi za umma mmejisahahu kama sio Mwalimu ninyi mngekuwa mmeozea kwenye mapori mlikozaliwa? Mwabisha sio sera za Mwalimu ziliwaondoa tongotongo? Nasema tena kwa macho makavu bila Nyerere leo mngekuwa na ubavu wa kusimama na kusoma hotuba za Kiingereza kama mliozaliwa kwa Malkia? Kama hivyo ndivyo, chawauma nini na ninyi kuwasaidia wadogo zenu nao wapate elimu? Eti kwa masharti mliyoweka bado mwategemea katoto ka kakulima kafikie hatua ya kusoma hadi kupata shangingi la serikali kama ilivyowatokea ninyi?

Hisani za Mwalimu mwaonaje mkizirejesha kwa kuwawezesha watoto wa wakulima ambao yeye alifanya yote ili wawe kama mlivyo ninyi? Eti mwadhani kama angeamua kujiundia kausultani fulani ninyi mngefika hapo pa kusema kusomeshwa elimu ya juu ni hisani sio lazima? Ndiko kumuenzi Mwalimu huko? Yawezekana hata mmesahahu mafundisho yake kuhusu maadui wakubwa wa jamii yetu.

Mwajidai kwamba aliwataja maadui wetu kuwa ni pamoja na umaskini, ujinga na maradhi? Eti umaskini wapigwa vita kwa kuwaondosha wenyeji kwenye mashamba ya Kipunga na kuwakodishia wageni? Ndivyo alivyowafunza? Kwa nini mwamliza mzee wa watu huko peponi anakopata pumziko la milele? Nasema nisipojitoa katika hili nitajitoa katika lipi Yarabi?

Nani aliyewadanganya kwamba kazi ya kufuta ujinga itafanywa kwa kujenga madarasa bila kujali idadi ya walimu? Mwalimu anayefunzwa kwa kubaguliwa anaruhusiwa kuitwa mwalimu? Mwapuuza thamani ya ualimu kiasi hicho bado mwadai kumshabikia na kumuenzi Mwalimu. Simo, tena simo kabisa!

Niambieni ni nabii yupi aliyewaambia huko aliko Mwalimu atafurahi sana kama mtatumia jina lake katika hayo mambo yenu? Tangu shule hadi ukumbi wa sinema vyote vyapewa jina la Mwalimu? Na hizo barabara mnazozipa jina la Mwalimu zina uzuri unaoshabihiana na heshima ya mzee wetu? Mwadhani vijana wetu wasiomjua Mwalimu watapata picha gani ikiwa barabara inayoitwa jina la Nyerere ina madimbwi na isyotamanika? Hamuoni hatari ya kuwafanya waamini kwamba Mwalimu alikuwa mtu aliyekosa staha kama hizo barabara? Natamani ningekuwa mwanafamilia wa marehemu nilitafutie hilo jina hakimiliki. Kila kitu kiitwe jina la Nyerere bila kujali ubora wake, bado mjiaminishe eti mnamuenzi huyo mzee wa taifa? Simo kabisa.

Yawezekana njia bora zaidi ya kumuenzi Mwalimu ni kuuza kila alichoanzisha? Niambieni niwaelewe enyi walimwengu, kama Julius angeuza hizo nyumba wakati wa utawala wake wa zaidi ya robo karne, ninyi mngejiuzia nini? Mwadhani mwamuenzi sana kwa kujifikia ninyi na ndugu zenu pekee? Kama ni kumuenzi Mwalimu, mbona mngetanguliza maslahi ya taifa yakiwemo yale ya kizazi kijacho? Hata kama watasema umekumbuka kujifunika shuka baada ya alfajiri kupiga hodi, JK kaza uzi urudishe kilichopotea. Waswahili si wanasema heri kuchelewa kuliko kukosa? Nijitoe kabla hamjaniweka kundi moja na wale wenye wivu wa kike. Aku! Simo mwanakwetu.

Ni kweli hakuna walioko madarakani ambao wameingia kwa kile kinachoitwa takrima? Kama wapo eti na leo hao watathubutu bila soni kumlilia Mwalimu? Anayethubutu kusema kwamba Mwalimu alikuwa mpenda takrima yuko wapi? Mwabisha kila mnapopata nafasi ya kulitumia jina la huyo Mzanaki hamlitumii kwa faida yenu? Hapo kwa takrima mtatuelezaje wanakwetu? Eti mlihitaji jopo la majaji watatu wakae kitako na kuwafunza kwamba takrima ni rushwa katika msamiati mwingine? Mtathubutuje kusema ninyi ni wahitimu wazuri wa Mwalimu ikiwa somo hili la rushwa na madaraka mmepata sifuri hadi muigilizie kwa majaji? Simo kabisa katika hili!

Ya kusema yapo mengi mwanakwetu kuhusu huu unafiki wenu wa kumuenzi Mwalimu kwa maneno huku matendo yenu yakiwa mbali na matendo yake kama mbingu zilivyo mbali na ardhi. Eti enzi hizo za Mwalimu hao waliotuingiza mkenge katika mikataba mbalimbali mwadhani wangeachwa bila ya kuchapwa viboko hamsa wa sitini? Nasema simo tena, wacheni nimlilie Baba wa Taifa aliyelala kaburi kimya akiwaacha mumfukie na maadili ya uongozi. Simo katika haya yote.

kevinmakyao@hotmail.com
0748 265 072


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.