Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Nyerere; mtetezi na msemaji wa mataifa maskini duniani
Nyerere; mtetezi na msemaji wa mataifa maskini duniani
By Habari Tanzania | Published  10/14/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated

BARAFU ilikuwa imetanda mjini Stockholm, Sweden, wakati wa Mei Mosi mwaka 1976.

Waziri Mkuu wa Sweden wakati huo, Olof Palme, alikuwa akiongoza maadhimisho ya kitaifa ya Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani, maarufu kama Mei Mosi, akiwa sambamba na Mwalimu Julius Nyerere, aliyekuwa akitabasamu muda wote.

Tukio hilo linatukumbusha uchangamfu, umahiri wake kimataifa na urafiki wake wa dhati kwa Sweden.

Mwalimu alikuwa miongoni mwa viongozi mashuhuri, mahiri na wa aina yake ambao Afrika imepata kuwa nao kihistoria.

Mwalimu alipambana na ukoloni, ukandamizaji wa wanyonge na aliyepigania kufa na kupona, si uhuru wa taifa lake tu bali na mataifa mengine.

Julius Nyerere alikuwa mmoja wa viongozi waliojulikana na aliyeitangaza sana nchi yake na Bara la Afrika nje ya mipaka yake.

Watu wa mataifa ya nje si tu tulimhesabu Nyerere kama baba wa watu wake wa Tanzania bali pia kama msemaji wa nchi maskini hususan za Afrika na nyingine zinazaoendelea.

Tanzania, imekuwa mmoja wa washirika wakubwa na muhimu wa Sweden barani Afrika kutokana na mchango wa Mwalimu wa kuukuza ushirikiano huo.

Hayo yote yametokana zaidi na ushirikiano mkubwa wa kirafiki uliokuwapo kati ya Mmisionari Dk. Barbro Johansson na Nyerere, ambao ulisababisha kumkutanisha na Waziri Mkuu wa zamani wa Sweden, Tage Erlander. Pia alikuwa na uhusiano wa karibu na Waziri Mkuu Olof Palme. Uhusiano huu ambao umejengwa na viongozi hawa, bado umeendelea kuwapo kati ya Sweden na Tanzania.

Sweden inakumbuka na inaheshimu mchango mkubwa wa Tanzania katika harakati dhidi ya ukoloni, ubaguzi wa rangi, ukandamizaji dhidi ya wanyonge na ukombozi wa taifa.

Nyerere alishiriki kikamilifu katika uanzishaji wa iliyokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), ambao sasa unajulikana kama Umoja wa Afrika (AU), na alikuwa kinara wakati wa harakati za ukombozi wa nchi zilizo mstari wa mbele kwa ukombozi wa kusini mwa Afrika na harakati za kupigania ubaguzi wa rangi na ukandamizaji dhidi ya wanyonge.

Kuteuliwa kwa Tanzania kwenye Kamati ya Ukombozi ya OAU ni moja ya mifano michache inayoonyesha umahiri wa uongozi wa Mwalimu Nyerere katika harakati za ukombozi zilizoshuhudia Tanzania ikiwa makao makuu ya wanaharakati katika miaka ya 1960 na 1970.

Mwalimu Nyerere alikuwa kiongozi aliyekuwa akisimamia majukumu yake bila kurudi nyuma au kuyakwepa hata kama yalikuwa magumu kiasi gani.

Kama baba wa taifa lake, Nyerere aliweka misingi imara ya amani na umoja wa kitaifa tangu uhuru.

Amefanikiwa kuunda taifa lenye mshikamano wa aina yake, ambao pamoja na kuwa na makabila 120, uhasama wa kikabila ni historia na tofauti za kisiasa na kidini pia ni jambo lisilojulikana.

Shukrani zimwendee Nyerere, Tanzania imekuwa nchi ya kupigiwa mfano duniani na moja ya wawezeshaji wa amani, ushirikiano na amani na utulivu barani Afrika.

Julius Nyerere pia alikuwa mtu anayeona mbali na mambo aliyoyapa kipaumbele yalilenga wakati ujao, iwe katika masuala ya siasa, uchumi na jamii.

Miongoni mwa mafanikio mengi yaliyoletwa na uongozi wa Nyerere ni pamoja na mpango wake wa elimu kwa wote, ambayo iliiweka Tanzania kwenye chati ya juu ya kiwango cha ubora wa elimu barani Afrika.

Kama msomi, amejulikana kama Mwalimu, yaani ‘teacher’ kwa Kiingereza, jina ambalo ni la heshima lililomkaa hadi kifo chake.

Japokuwa alistaafu urais kwa hiari yake mwaka 1985, Nyerere aliweka misingi mizuri pamoja na mifano ambayo viongozi wa Afrika wanapaswa kuiiga.

Alibaki kuwa mwenyekiti wa chama hadi mwaka 1990. Pia alishiriki kikamilifu katika uanzishaji wa mfumo wa vyama vingi vya siasa mapema miaka ya 1990.

Katika maisha ya ustaafu, Julius Nyerere alirudi nyumbani kijijini kwao Butiama, lakini alibakia katika duru la kitaifa na kimataifa kuendelea katika harakati zake asizozichoka kwa ajili ya ustawi wa Bara la Afrika na nchi nyingine za dunia ya tatu. Miongoni mwa kazi alizofanya wakati wa maisha yake ya ustaafu ni upatanishi wa Burundi.

Kutokana na kifo cha Julius Nyerere tumepoteza kiongozi mkubwa barani Afrika. Mafanikio yake yatabakia katika nyoyo za watu wote Afrika na dunia nzima na kuwa chachu ya kujitafutia maendeleo, usawa na amani.

Imetafsiriwa kutokana na hotuba ya Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo, Uhamiaji na Sera za Wakimbizi wa Sweden, wakati wa misa maalumu ya kukumbuka kifo cha Nyerere, St. Klara, Stockholm.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.