Kutoka Gazeti la Tanzania Daima.
LEO ni miaka saba tangu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alipoaga dunia.
Watanzania na walimwengu wapenda haki, wanaendelea kulia kila wanapomkumbuka Mwalimu.
Ingawa kimwili hatunaye, fikra na mafundisho ya Mwalimu vimeendelea kuwa dira sahihi ya namna binadamu wanavyopaswa kutenda na kuishi kwa usawa na upendo.
Miaka saba baada ya kifo, pengo aliloacha linaonekana. Yapo masuala mengi ya kitaifa na kimataifa yaliyokosa ufumbuzi, na laiti kama Mwalimu angelikuwapo, bila shaka majibu yangepatikana.
Wakati Watanzania na walimwengu wengine wanaomheshimu Mwalimu wakiadhimisha siku ya leo kwa uchungu, kuna mengi ya kujiuliza.
Mwalimu aliamini katika umoja, haki, mshikamano, upendo, demokrasia na maendeleo ya binadamu wote bila kujali rangi, tabaka, asili, jinsia au hali.
Mambo haya ambayo aliyasimamia kwa kipindi chote cha uhai wake, yako katika hali gani?
Je, Watanzania wameendelea kuwa wamoja? Je, wanapendana? Je, maskini wanapungua au wanaongezeka nchini? Je, watoto wenye sifa za kuanza shule za msingi wanapata nafasi? Je, elimu wanayopata watoto wa makabwela inafanana na wanayopata watoto wa matajiri?
Je, uporaji rasilimali za taifa umepungua au unaongezeka? Je, ule moyo wa uzalendo aliowafundisha Watanzania bado upo? Je, Watanzania bado wana moyo wa kusaidiana?
Ile elimu ya kujitegemea aliyowafundisha Watanzania, akaenda hadi vijijini kupiga kambi ili kutoa mfano, inatekelezwa?
Je, maisha ya kifahari, maisha ya kufuja mali za umma, maisha ya wizi na ufisadi, maisha ya anasa na kutowajali wasiokuwa nacho yametoweka?
Vita aliyoianzisha dhidi ya udini, ukabila na aina zote za ubaguzi, inaendelezwa kama alivyofanya?
Maswali yanaweza kuwa mengi, sawia na majibu. Lakini lililo wazi ni kwamba ile misingi mizuri ya umoja wa kitaifa ambayo Mwalimu aliiasisi na kuisimamia kwa vitendo, imeanza kutoweka, tena kutoweka kwa kasi.
Kiongozi anayeweza kusimama jukwaani leo na kutamba kwamba anamuenzi Mwalimu Nyerere, anakuwa anawadanganya walimwengu.
Tuna baadhi ya viongozi wezi wa mali za umma, waliopora mali za taifa kupitia kivuli cha utandawazi.
Tumeshuhudia viongozi wachache wakijitwalia mali za umma, wakiuza majengo na mali za umma, wakijenga majengo wasiyoyahitaji kwa matumizi yao, na wakifanya kila linalowezekana, alimradi tu wapore utajiri.
Leo kuna viongozi wahubiri udini, viongozi ambao ni wa kwanza kuuliza: “Rais ameteua Wakristo wangapi? Rais ameteua Waislamu wangapi?” Hakuna aibu tena ya kuzungumzia udini au ukabila.
Watu wameanza kupeana vyeo kwa kuulizana makabila au kanda wanazotoka na kadhalika. Mwalimu Nyerere alilaani vikali tabia hii.
Viongozi wamekuwa wakwasi kupindukia. Hawana majibu ya ukwasi huo. Wanakula na kusaza ilhali maelfu kwa maelfu ya watoto wakitaabika kwa kukosa huduma za afya, elimu, maji safi na salama na huduma nyingine muhimu za kijamii.
Watoto wanasoma wakiwa wameketi chini, huku baadhi ya watoto wa matajiri wakisoma nje ya nchi kwa gharama kubwa kupindukia.
Tofauti za maisha sasa ni njia inayolipeleka taifa katika hatari ya kuvunjika amani na utulivu nchini.
Maelfu ya wamachinga wanaoonekana mijini sasa, ni matokeo ya kupuuzwa kwa sera zilizoasisiwa na Mwalimu - sera za kutoa elimu ya kujitegemea, na sera za kuhakikisha kunakuwapo viwanda na shughuli nyingine za uzalishaji mali.
Mwalimu hakufa. Wanaotaka kumuua ni baadhi ya viongozi wasio waaminifu. Fikra zake daima zitakuwa hai.
Anayetaka kuthibitisha haya, asikilize hotuba au asome maandiko yake. Mungu ibariki Tanzania, Mungu mpumzishe kwa amani, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Burito.