WAZIRI Mkuu, Edward Lowassa, amesema watendaji ndani ya Halmashauri ya Jiji la Tanga wamejaa ubabaishaji na uswahili mwingi.
Alisema hayo jana alipokuwa akipokea taarifa ya utendaji ya Wilaya ya Tanga Mjini iliyohusisha pia watendaji wa halmashauri hiyo kwenye siku ya mwisho ya ziara yake mkoani hapa ya kukagua shughuli za maendeleo.
Lowassa alisema watendaji wa jiji hilo wanalaumiwa kwa kufanya mambo kinyume cha taratibu, ikiwa ni pamoja na kuidhinisha matumizi ya fedha isivyo halali na kutoa zabuni kinyume cha taratibu.
Moja ya mambo yaliyozua mjadala mkubwa kwenye mkutano huo ni lile lililomhusisha Mganga Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Dk. Pili Ntuka, ambaye alidaiwa kutumia fedha kinyume cha maudhui yaliyokusudiwa.
Dk. Ntuka, anatuhumiwa kushirikiana na Mhasibu wa Jiji aliyetambulika kwa jina moja la Karia, kuchukua sh milioni 17 na kuzitumia kwa shughuli nyingine. Fedha hizo zilitengwa kwa ajili ya mapambano dhidi ya UKIMWI.
Dk. Ntuka alikiri mbele Waziri Mkuu kuwa alifanya makosa na tayari alipewa adhabu ya kusimamishwa kazi, lakini akasema fedha hizo aliziazima kwa ajili ya kampeni ya chanjo ya kitaifa ya surua.
Mjadala huo ulionyesha wazi kuwa fedha hizo zilichukuliwa visivyo halali na mganga huyo, akishirikiana na mhasibu wa jiji ambaye kwa sasa yupo nje ya jiji kwa kozi ya muda mfupi.
Husna Rajabu ambaye ana shahada ya pili ya mambo ya afya, alidai mbele ya kikao hicho kuwa baada ya kutoa malalamiko juu ya matumizi hayo yasiyo halali, alishushwa cheo kutoka ukaimu Ofisa Afya Jiji hadi kuwa Ofisa Afya wa Kata ya Ngamiani.
Alisema nafasi yake alipewa mtu mwingine ambaye alikuwa akifanya mtihani wa kidato cha nne, na ambaye hana uzoefu wa kutosha kwenye shughuli hizo, na ambaye analindwa na viongozi wa halmashauri hiyo.
Mkurugenzi wa Jiji la Tanga, Paul Baruti, akijitetea mbele ya Waziri Mkuu, alidai kuwa kuteremshwa cheo kwa ofisa huyo hakutokani na mgogoro huo, bali ni kutokana na kutokuwa mtendaji makini, hali iliyolifanya jiji hilo liwe chafu. Lowassa alionekana dhahiri kutokubaliana na hoja hiyo.
“Mkurugenzi, lakini mmemshusha cheo huyo mama baada ya kufichua hiyo habari ya fedha na wewe unasema kwa sababu ya utendaji mbovu, lakini ulim- demote tu baada ya kufichua habari hii, lakini si kwa hili au siyo?” alihoji.
Waziri Mkuu alisema kumekuwapo lawama nyingi zinazoelekezwa kwa Mstahiki Meya wa Jiji, Kasim Kisauji, pamoja na watendaji wengine wa jiji, kupitia barua.
Alisema viongozi hao wanadaiwa kupendelea baadhi ya watu katika ushindani wa zabuni.
Kisauji alisema hahusiki kwenye Bodi ya Zabuni, na kwamba kinachofanyika ni fitina za kisiasa ambazo zinaongozwa na Katibu Mwenezi wa CCM Wilaya, Mhandisi Sheke Pashua.
Anasema kiongozi huyo mwenzake, hakutaka awe meya wa jiji hilo.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu hapa kuna zaidi ya haya ya tenda, kuna maneno yanapikwa hapa na barua nyingi zinaandikwa… hata kwenye ofisi ya CCM kuna barua nyingi zinazonihusu, lakini haya yote ni majungu,” alijitetea.
Alipoulizwa na Tanzania Daima kuhusu lawama hizo, Katibu Mwenezi huyo ambaye pia ni mfanyabishara, alisema maneno ya meya ni ya kujitetea, lakini ukweli ni kuwa anashutumiwa kwa kushawishi tenda hizo zitolewe kwa watu anaowajua.
Waziri Mkuu alifanya kikao cha faragha na wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM Mkoa, kikao kinachoaminika kujadili suala la mgawanyiko huo.
Mambo mengine yaliyozua mjadala kwenye halmashauri hiyo ni kuwapo kwa wataalamu 15 wa kilimo na watano wenye shahada, lakini halmashauri hiyo iko chini katika uzalishaji.
Waziri Mkuu, pia aliwashutumu watendaji wa halmashauri hiyo kwa kushindwa kuhimiza uanzishaji na utumiaji vyama vya akiba na mikopo (SACCOS).
Alimwagiza meya ahakikishe kikao cha madiwani kinafanyika haraka ili kuondoa kero zinazokigawa chama. Ametaka apewe taarifa baada ya siku 14.
Wakati huo huo, Lowassa, ameipatia Hospitali ya Mkoa ya Bombo sh milioni 10 ili zisaidie kupunguza matatizo yanayoikabili.
Watumishi katika hospitali hiyo, wanaidai serikali sh zaidi ya milioni 400.
Pamoja na msaada huo, Waziri Mkuu alisema nia ya serikali ni kujenga hospitali nyingine ili kupunguza msongamano wa wagonjwa uliopo Bombo