Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  JK azindua kamati kukusanya maoni ya Shirikisho la EAC
JK azindua kamati kukusanya maoni ya Shirikisho la EAC
By Habari Tanzania | Published  10/14/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Happiness Katabazi

RAIS Jakaya Kikwete, amesema wananchi wa Afrika Mashariki hawataweza kuheshimika wala kutamba katika majukwaa ya kimataifa bila kuwa na umoja wao.

Amewataka wananchi wa nchi zote tatu wakubali kutanguliza mbele maslahi ya Afrika Mashariki yanayozingatia na kuendeleza maslahi yao wote.

Rais Kikwete alisema hayo wakati akizindua mchakato wa kupata maoni ya wananchi kuhusu kuharakisha uundaji wa Shirikisho la Afrika Mashariki.

Uzinduzi huo ulifanyika jana katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi wa serikali, mabalozi, viongozi na wanachama wa vyama vya siasa, na mamia ya wananchi.

Uzinduzi kama huo ulifanywa pia jana na marais Yoweri Museveni wa Uganda na Mwai Kibaki wa Kenya.

“Imebainika na mataifa mengi duniani, tajiri na maskini, kwamba mataifa yanapokuja pamoja katika utangamano, ndipo yanapojenga uwezo mkubwa wa ushindi… na sisi EAC tumegundua hivyo,” alisema Rais Kikwete.

Alisema katika kipindi cha miaka sita iliyopita, shughuli za ushirikiano wa nchi zote tatu bado umejikita zaidi katika masuala ya kiuchumi na kijamii tu.

Alisema ili ushirikiano na utangamano wa nchi zote tatu uwe na nguvu zaidi, sharti umoja huo ujumuishe masuala ya kisiasa zaidi ya yale ya kiuchumi, kiusalama na kijamii.

Alisema kuanzishwa kwa umoja wa forodha miaka minne baada ya kuundwa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuundwa, ni ushaidi tosha kuwa wananchi wa Afrika Mashariki wamedhamiria kuharakisha mchakato wa mtangamano wao wa kiuchumi.

“Mchakato wa kuanzisha Soko la Pamoja uko mbioni, Soko la Pamoja litafuatiwa na Umoja wa Sarafu, yaani pamoja na mambo ya Soko la Pamoja, nchi zetu zitakuwa na sarafu moja na sera za fedha na bajeti zinazofanana… hivyo Watanzania nawahamasisha mshiriki kikamilifu kutoa maoni yenu kuhusu shirikisho hili,” alisema.

Alisema wananchi wa Afrika Mashariki hawana budi kukumbuka kwamba mambo hayo si mageni, kwani EAC iliyokufa mwaka 1977 nchi zote tatu zilikuwa na Umoja wa Forodha, Soko la Pamoja na Sarafu ya Pamoja.

Alisema wakati huo mambo yalikuwa mazuri na jumuiya ya wakati ule ilikuwa ni taasisi ya ushirikiano na mtangamano wa kanda, uliokuwa umefanikiwa kuliko yoyote ya aina hiyo hapa duniani.

“Hivyo basi, hakuna sababu kwa wananchi wa Afrika Mashariki kuwa na hofu kuhusu utangamano wa jumuiya na kudai kutokufaa au kutokuwezekana… pengine ile hali kwamba jumuiya ya zamani ilikufa, inaweza kuwa sababu ya kutilia shaka, hivyo mjitokeze kwa wingi kutoa maoni yenu kwenye kamati maalumu zilizoundwa kutoa maoni yenu,” alisema.

Rais Kikwete alisema mazingira ya dunia na ya Afrika Mashariki kwa wakati huu ni tofauti na ilivyokuwa wakati ule.

Alisema kitu muhimu kilichokosekana katika ushirikiano na mtangamano wa kwanza wa Afrika Mashariki ni mtangamano wa kisiasa.

“Kadiri tunavyoendelea kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi wa nchi wanachama wa EAC, hatuna budi tuanze pia kufikiri kwa makini zaidi ni kwa jinsi gani tunaweza kuelekeza nguvu zetu kwenye umoja wa kisiasa ulio madhubuti.

“Suala la umoja wa kisiasa mara nyingi ni suala gumu kwa sababu ni suala linalogusa mustakabali mzima wa nchi na utaifa, linagusa uhuru, utaifa pamoja na mamlaka ya nchi huru,” alisema.

Aliwahakikishia wananchi kwa kusema kwamba matakwa ya wananchi wengi wa Tanzania, Kenya na Uganda kuhusu uundaji shirikisho, yataheshimiwa.

Alisema kuwa jumuiya mpya ambayo amedhamiria kuijenga shabaha yake kuu ni kuhakikisha kuwa wananchi wanaishi kwa amani na katika maendeleo.

“Katika hoja ya Shirikisho la Afrika Mashariki kunawezekana yakajitokeza makundi katika kila nchi yatakayotaka kutetetea maslahi yao, hilo litakuwa jambo la kawaida.

“Lakini lililo muhimu ndugu wananchi ni sisi sote kutambua ukweli kwamba ili mtangamano wa kisiasa wa nchi zetu uweze kufanikiwa, lazima wote tukubali kwa dhati dhana ya ‘kutoa kidogo ili upate kidogo’,” alisema.

Kamati ya mchakato wa kukusanya maoni ya Watanzania inaundwa na wajumbe 16 ambao ni Profesa Samweli Wangwe (Mwenyekiti), Ali Ameir Mohamed (Makamu Mwenyekiti), Joseph Butiku, Zitto Kabwe, Nestory Ngulla, Hazara Pindi Chana, Ibrahim Kaduma, Christine Kilindu, Amina Shaaban na Mariam Shaba.

Wengine ni Mariam Juma, Ali Mzee Ali, Evis Musiba, Hamis Kagasheki, Khalifa Suleiman Khalifa, na Omar Bendera (Katibu wa Kamati).

Bendera atakuwa na wasaidizi wawili, mmoja kutoka Tanzania Bara na mwingine kutoka Tanzania Zanzibar.

Kamati hiyo itafanya kazi zake kwa kipindi cha miezi sita. Itatembelea mikoa na wilaya zote Bara na Visiwani


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.