WIKI mbili zimekuwa ni wiki za misukosuko katika jiji la Dar es Salaam. Zimekuwa ni wiki ambazo wafanyabiashara wadogowadogo, maarufu kwa jina la wamachinga wamekuwa wakipigwa danadana na mamlaka za umma kuhusu hatima yao.
Serikali ya Awamu ya Nne iliyoingia madarakani, Desemba mwaka jana, imekuja na vipaumbele vingi vya kazi, moja kati ya vipengele hivyo kikiwa ni kile kinachowahusu wafanyabiashara ndogo ndogo.
Miezi sita na ushee iliyopita, Serikali Mkoa wa Dar es Salaam ilifanya mambo makuu mawili. Mosi ilianzisha operesheni maalumu ya kuwaondoa wapigadebe katika vituo vyote vya mabasi ya daladala na ikaendelea hadi katika kituo kikuu cha mabasi yaendayo mikoani cha Ubungo (UBT) na pili ikawalenga wamachinga ambao wamezagaa katika maeneo mbalimbali nchini.
Operesheni hizo, ingawa zilipata umaarufu mkubwa katika Jiji la Dar es Salaam, ziliigusa pia mikoa mingine kadhaa kama Mwanza ambako pia walianzisha operesheni zenye mwelekeo huo huo.
Kwa bahati mbaya, operesheni hiyo ya miezi sita iliyopita ilianza kwa mguu mbaya, kukatokea matukio mabaya kabisa ya kihuni, ambayo yalisababisha majeruhi na maafa wakati zoezi hilo la kuwaondoa wamachinga na wapigadebe lilipokuwa likitekelezwa.
Hali hiyo ilisababisha serikali iingilie kati na Waziri Mkuu, Edward Lowassa akatangaza kuongeza miezi sita zaidi ya kuwaondoa katika mitaa ya jiji wamachinga ambao wamezagaa mitaani katika maeneo mbalimbali nchini.
Muda uliopangwa na serikali ulipokwisha, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Kandoro akasimamia utekelezaji wa kazi za kuwaondoa wamachinga hao, safari hii serikali ikionyesha hali ya ukomavu na uvumilivu.
Kwa bahati nzuri, wamachinga safari hii waliamua kutii. Walitii amri ya kuondoka na baadhi yao tayari wameshahamia katika maeneo ya masoko waliyopangiwa wakati wengine wengi wakiendelea kufanya biashara za kubahatisha katika maeneo ya umma ambayo walikwishakatazwa.
Siku chache tu baada ya baadhi ya wamachinga kuhamia walikopangiwa, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ikatangaza nia yake ya kuanza kuwatoza kodi, hatua ambayo si tu iliwashitua wafanyabiashara hao, bali pia ilimstua Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Kwa bahati njema, Kandoro alipoliona hilo, moja kwa moja akaenda TRA na akawaasa waachane na suala hilo akijua fika kwamba, uamuzi huo wa TRA ulikuwa ukitaka kuwavuruga zaidi vijana hao ambao wamekuwa wakiondolewa katika mitaa ambayo wangependa waendelee kuwapo, kwa mkono wa nguvu ya dola.
Pamoja na nia njema ya Kandoro kuwanusuru wamachinga na pengine dhamira safi kabisa ya serikali ya kuwatatufia maeneo mengine ya kibiashara nje ya maeneo ya katikati ya jiji, bado operesheni hii nzima imefanywa kwa kukabiliana na matokeo kuliko kiini cha tatizo lenyewe.
Tunasema hivyo tukitambua kwamba, hivi sasa, hasa baada ya kuingia kwa mfumo wa soko huria, tatizo la wamachinga limekuwa likisumbua miji mbalimbali mikubwa duniani.
Hakuna ubishi kwamba tatizo lililopo ni umachinga na wala si wamachinga. Shida iliyopo ni umaskini uliovuka mipaka. Jambo lililopo ni mgawanyo mbaya wa rasilimali za kimaendeleo kati ya miji na vijiji. Kikwazo kilichopo ni ukosefu wa elimu, ajira na fursa nyingine muhimu za kimaisha. Mambo yote hayo yakiwekwa pamoja, ndiyo yanayozaa wamachinga na kimsingi hayo ndiyo mambo ya kuyatafutia majibu, kabla hatujaanza kufukuzana na wamachinga barabarani.