Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  CCM sasa yataka kuipeleka kusiko demokrasia shindani
CCM sasa yataka kuipeleka kusiko demokrasia shindani
By Habari Tanzania | Published  10/12/2006 | Habari za Kitaifa | Rating:

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yussuf Makamba ambaye ameshika madaraka hayo makubwa ya juu ndani ya CCM kwa muda wa miezi miwili na nusu sasa, ameingia na kasumba mbaya kabisa ya kiuongozi.

Makamba ameingia kwa staili ile ya kawaida ya viongozi wakuu wa CCM ya kutembea kifua mbele kila mara chama hicho kinapofanikiwa kuwanasa viongozi kadhaa wa vyama vya upinzani.

Tangu aingie madarakani, Makamba akiwa ameongozana na mwenyekiti wake wa CCM taifa, Rais Jakaya Kikwete, walianza kuendesha harakati zao hizo za kuwanasa wapinzani waliokuwa wamekatishwa tamaa ndani ya vyama walivyokuwa.

Kwanza walimpandisha katika jukwaa lao, aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Uenezi wa Chama cha Wananchi (CUF), Tambwe Hizza na baadaye akaja Njelu Kassaka ambaye naye alijiunga na CUF akitokea CCM.

Siku chache baadaye, Makamba akiwa Arusha katika Wilaya ya Hai, akawapokea wanachama wawili wapya ambao nao walikuwa viongozi wa juu katika kambi ya upinzani.

Wa kwanza akawa Amaan Walid Kabourou, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na kufuatiwa na Jacob Nkomola ambaye alikuwa Katibu Mkuu wa chama cha Sauti ya Watu.

Kujiunga kwa wanasiasa hao CCM, lilikuwa ni jambo lililotegemewa na watu waliokuwa wakifuatilia mwenendo wa siasa za ndani ya CCM na katika vyama vya upinzani ambako wametoka.

Tambwe yeye alikuwa ni majeruhi mkubwa wa siasa za ndani ya CUF. Miezi michache baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, chama hicho kilifanya mabadiliko makubwa katika uongozi wa kurugenzi zake.

Mmoja kati ya majeruhi hao alikuwa ni Tambwe ambaye chama hicho kiliamua kumpokonya madaraka aliyokuwa nayo kwa muda mrefu ya ukurugenzi wa uenezi. Kwake hilo lilikuwa pigo, kwani lilikuja miezi tu baada ya kupoteza ubunge wa Temeke ambao amekuwa akiusaka kupitia vyama vya NCCR Mageuzi na baadaye CUF bila mafanikio.

Kassaka naye hakuwa na sababu ya kuendelea kubakia CUF. Alijiunga na chama hicho cha upinzani dhamira yake ikijionyesha dhahiri kuwa alikuwa akiulenga ubunge wa Jimbo la Lupa ambalo alilikosa baada ya CCM, chama alichokitumia kwa miaka mingi, kumteua Victor Mwambalaswa kuwa mgombea wake ubunge na baadaye akawa mbunge.

Hali ilikuwa hiyo pia kwa Kabourou, ambaye alipoteza kiti chake cha ubunge cha Kigoma na akawa Makamu Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA asiye na sauti kutokana na kuonekana siku nyingi kutengana kimaadili na wapinzani wenzake.

Makamba na CCM wakijua vyema hali ya kisiasa waliyokuwa nayo wanasiasa hao, iliamua kuwajengea ‘mazingira’ ya kurejea katika chama hicho tawala, lengo likiwa pamoja na mambo mengine, kuwathibitishia wananchi kwamba chama hicho tawala ndicho pekee kinachokubalika nchini.

Upo uwezekano kwamba CCM imefanikiwa katika hilo, na uzoefu wa miaka ya nyuma umekuwa ukithibitisha namna harakati za namna hiyo za chama hicho tawala zilivyofanikiwa kudhoofisha upinzani na hivyo kukihakikishia ushindi unaoitwa wa kishindo.

Ingawa CCM inaonekana kuvuna sana kutoka kambi ya upinzani na hata kuendelea kuwa chama chenye nguvu ambacho mgombea wake wa urais anashinda kwa asilimia 80, kitendo cha kuudhoofisha upinzani kina madhara makubwa.

Sisi wa Tanzania Daima tunaamini kwamba, chama chenye mapenzi ya kweli na taifa hili na kinachoheshimu ushindani wa haki wa vyama vingi na kuzingatia misingi ya utawala bora, hakiwezi kamwe kufurahia aina hii ya mikakati ya CCM.

Tunasema hivyo tukitambua kwamba, rekodi za nchi nyingi zilizopiga hatua katika maeneo ya uchumi wenye nguvu wa soko huria, demokrasia shindanishi na heshima kwa misingi ya utawala bora, zimeweza kusonga mbele katika maendeleo kuliko zile zinazoendekeza udikteta wa chama kimoja na mifumo kandamizi ya fikra. CCM wanapaswa kujifunza hilo


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.