JESHI la Polisi nchini, limeshindwa kuanza operesheni maalumu ya kuhakiki madereva, iliyotatajiwa kuanza jana katika Kituo Kikuu cha Mabasi cha Ubungo (UBT), Dar es Salaam.
Operesheni hiyo ilikuwa na lengo la kuhakiki madereva halali kwa kukagua leseni halisi, hati ya ushindi, upimwaji afya, uchukuaji wa alama za vidole, upigwaji picha, ikiwa ni pamoja na kuwasilisha vielelezo vyote wanavyotakiwa kuwa navyo madereva kwa mujibu wa sheria.
Tanzania Daima ilifika katika kituo hicho asubuhi kwa ajili ya kufuatilia operesheni hiyo, lakini hapakuwa na mtendaji yeyote kutoka katika moja ya mamlaka zilizotarajiwa kushiriki katika operesheni hiyo.
Watendaji waliotakiwa kushiriki katika operesheni hiyo ni pamoja na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Kitengo cha Utambulisho (IB) cha Makao Makuu ya Polisi.
Wengine ni Tanzania Technology Transfer (TANT), Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA), Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, pamoja na Kikosi cha Usalama Barabarani Makao Makuu.
Baadhi ya madereva ambao hawakutaka kuandikwa majina yao, waliiambia Tanzania Daima kuwa walikuwa na taarifa ya operesheni hiyo, lakini cha kushangaza tangu asubuhi hakuna kazi iliyofanyika na kuwa hawakuona hata mtendaji kutoka mamlaka yeyote iliyotarajiwa kushiriki.
“Baadhi ya magari ambayo yalifanyiwa ukaguzi na kubainika kuwa ni mabovu yameng’olewa namba na yameegeshwa katika gereji iliyoko humu ndani na mengine wamiliki wameshayaondoa na kuyapeleka katika matengenezo nje ya kituo,” alisema.
Jitihada za kumpata Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Tanzania, Mselem Mtulia pamoja na mkuu wa operesheni hiyo, Mrakibu wa Polisi (SP) Edward Balele, ili kuelezea sababu za kukwama kwa operesheni hiyo, hazikufanikiwa kwa taarifa kuwa walikuwa katika mkutano makao makuu