WAZIRI Mkuu, Edward Lowassa, amewakemea wazee wa Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga, wanaowapa mimba wanafunzi wakati wakiwa masomoni kuacha tabia hiyo mara moja.
Lowassa alitoa karipio hilo jana wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Manundu wilayani hapa.
“Taarifa za wilaya yenu zinaonyesha kati ya wanafunzi 100 wanaoandikishwa darasa la kwanza, wanafunzi 66 ndio wanaomaliza darasa la saba… taarifa hizo zinaonyesha tangu Januari hadi Mei mwaka huu, wanafunzi 30 wa shule za msingi wamepata ujauzito… hii ni aibu ndugu zangu,” alisema Waziri Mkuu.
Alisema kinachosikitisha, kati ya kesi 50 zinazofunguliwa mahakamani kuhusu masuala yanayohusu mamba, 30 zinamalizika nje ya mahakama. “Watu hawa wanamaliza kesi hizo kwa kutoa kitu kidogo, sikatai msioe, ninachohimiza muwaache wasome wafaulu halafu mnaweza kuoa hata wanawake 50, oeni tu,” alisema.
Alisema kuanzishwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutahitaji watu wenye taaluma. Kwa kuwapeleka watoto shuleni kutawasaidia kupata ajira, wasipowapeleka shule, watu kutoka Kenya na Uganda watapata ajira hapa.
“Wanafunzi nawahimiza muwaambie wazazi wenu wanaowatia mimba na wanaofahamika kwa vitendo hivyo mitaani wakamatwe, viongozi wa makanisa na misikiti wahimizeni wananchi waache tabia hii,” alisema Lowassa.
“Nakuagiza DC waswage ndani wote wanaowatia mimba wanafunzi, polisi na mahakama jamani, msaidieni DC katika kazi hii,” alisema.
Awali, akitoa taarifa yake Mkuu wa Wilaya (DC) ya Korogwe, Betty Mkwassa, alisema wilaya hiyo imetenga jumla ya sh milioni 175 kwa ajili ya kuwajengea uwezo watu mbalimbali kwa ngazi za wilaya na vijiji katika shughuli za maendeleo.
Alisema wilaya yake imepokea sh zaidi ya bilioni 3.2 kwa ajili ya shughuli za ukamilishaji wa Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM), tangu mwaka 2001 hadi 2006.
Mkwassa, alisema katika Mpango wa Maendeleo kwa Elimu ya Sekondari (MMES), awamu ya pili ya mwaka 2006/2007 imetenga sh milioni 47 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba saba vya madarasa na sh milioni 36 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba nne za walimu.
Kwa upande wa afya, mkuu huyo wa wilaya alisema, kuanzia Januari hadi Septemba mwaka huu, takwimu zinaonyesha watu waliopima damu kuwa ni 1,408 kati yao wanaume ni 1,347 na wanawake 61.
Alisema kuwa walioonekana kuwa na maambukizi ya virusi vya UKIMWI ni watu 90 kati yao wanaume ni 87 sawa na asilimia 5.8 na wanawake 7 sawa na asilimia 0.5.
Alisema, kutokana na kasi ya maambukizi ya UKIMWI, idadi ya yatima imeongezeka na takwimu zinaonyesha kuwa kati ya Januari hadi Septemba mwaka huu, idadi ya watoto yatima imeongezeka na kufikia 4,727. Kati yao watoto wa kiume ni 2,453 na wa kike 2,274 ikiwa ni ongezeko la watoto 432 sawa na asilimia 9.1.
Waziri Mkuu anaendelea na ziara yake katika wilaya za Handeni na Kilindi mkoani Tanga.