BALOZI Mpya wa Tanzania hapa Uingereza, Mwanaidi Sinare Maajar amesema Rais Jakaya Kikwete hatajutia uamuzi wake wa kumteua kushika wadhifa huo mkubwa .
Akizungumza katika mahojiano maalum na waandishi wa habari katika ofisi za Ubalozi wa Tanzania uliopo Bond Street katikati ya Jiji la London, Balozi Maajar alisema kamwe hatamwangusha Mheshimiwa Rais katika utendaji wake wa kazi.
Balozi Maajar ambaye kitaaluma ni mwanasheria aliyekuwa anaongoza kampuni ya mawakili ya Maajar, Rwechungura & Makani ya jijini dare s Salaam, alisema ulikuwa uamuzi mzito kukubali nafasi hiyo ya ubalozi aliyopewa na Rai Kikwete.
Alisema alijisikia furaha na kuona heshma kubwa kwa Rais kumpa heshima na uzito wa jukumu alilokabidhiwa na atajitahidi kadri ya uwezo wake kufanya kazi hiyo kubwa sana ili kutomwangusha.
“Nilijisikia furaha kubwa sana na zaidi mimi nikiwa mwanamke kumwakilisha katika nchi kubwa kama hii ambayo tunaitegemea kwa misaada mbalimbali, kweli Mh Rais ameniamini na sintomwangusha kwa hili” alisema Balozi Maajar ambae ni msomi mwenye taaluma ya sheria.
Alisema ulikuwa ni uamuzi mzito sana kwake, lakini ilinibidi akubali kwa kuwa Mh: Rais aliahidi kutoa nafasi nyingi za uongozi kwa wanawake, hivyo mafanikio yake ni mafanikio ya wanawake wenzake na Taifa kwa ujumla.
Pia alisema ulikuwa uamuzi mgumu kwa sababu kampuni yao ya mawakili ya Maajar, Rwechungura & Makani ilikuwa imeungano na kamapuni nyingine, hivyo ilikuwa kwanza wanajipanga ili kuweza kuweka mikakati ya kazi.
Balozi huyo wa kwanza mwanamke kuiwakilisha Tanzania hapa Uingereza alisema jambo lingine lilimshawishi kukubali uamuzi huo ni mikakati, sera na miundombinu za Rais Kikwete katika kuwaletea maendeleo Watanzania.
“Ni kiongozi ninaempenda kama anavyopendwa na Watanzania wengi,mwenye sera na mwelekeo mzuri wa kumpatia Mtanzania maisha bora, hivyo nimeona ni bora nishirikiane nae kwa karibu ili kuiletea nchi yetu maendeleo,” alisema Balozi Maajar.
Alisema kamwe hataingia katika ulingo wa siasa kwa sababu yeye si mwanasiasa na kudai kuwa akimaliza muda wake kama balozi, kazi yake kubwa itakuwa kuwasaidia wanawake kisheria.
Kuhusu kazi yake kama balozi wa Tanzania hapa Uingereza, Balozi Maajar alisema itakuwa kusimamia utekelezaji wa Sera Mpya ya Mambo ya Nje ambayo inalenga zaidi kwenye diplomasia ya kiuchumi kutoka kwenye diplomasia ya siasa.
“Hivyo nawajibika kujenga mahusinao mazuri na Serikali ya Uingereza ili kuweza kupata mahusiano katika masuala ya kiuchumi na kimaendeleo,” alisema Balozi Maajar.
Alisema changamoto kubwa ambayo sasa anakumbana nayo ni kujitangaza kidiplomasia ya kiuchumi kutoka kwenye siasa.
“Mikakati iliyowekwa nyumbani na Serikali ndio tumekuja nayo huku kwenye ofisi za mabalozi,tunajitahidi kuhakikisha kwamba wawekezaji waweze kujua mengi kuhusu uwekezaji kabla ya kufika Tanzania,” alisema.
Alitaja mikakati hiyo ni pamoja na kuweka mambo muhimu yanayohitaji kwenye mtandao wa ubalozi ambao utakuwa una link na mashirika yanayohusika na uwekezaji, utalii na baadhi ya ofisi za Serikali.
“Waingia wenyewe kwenye mtandao wajue kila kitu, hali ambayo inatamfaya hasiwe mgeni pindi atakapokwenda nyumbani kutaka kuwekeza katika sehemu husika,” alisema.
Alisema mikakati mingine ni kukifanya kituo cha biashara cha Tanzania “Tanzania Trade Centre” hapa Uingereza kuwa ndani ya ubalozi tofauti na huko nyuma kituo kilikuwa kinajitegemea na bajeti yake ilikuwa finyu.
“Tayari mikakati imeshafanyika tangu mwanzo kabla ya mimi sijaja, moja ni kuhakikisha kituo cha biashara kinakuwepo ndani ya ubalozi na siyo nje na kuweza kuandaa bajeti nzuri zaidi inatakwenda na wakati katika mwaka wa fedha ujao,” alisema.
Aidha Alisema kuwa Tanzania ni kituo kikubwa cha biashara katika nchi za Afrika Mashariki na Kati na kusisitiza kuwa mazingira ya kufanyia biashara ni mazuri na masoko yapo na hivyo kuwahimiza wawekezaji kuwekeza Tanzania.
Aliongeza kuwa Tanzania ni nchi ya amani na inayotawaliwa kwa misingi ya sheria, utawala bora na kuheshimu haki za binadamu, hivyo kuwatoa hofu wawekezaji na kusisitiza kuwa kuna nafasi nyingi za uwekezaji katika maeneo mbalimbali kuanzia utalii hadi kilimo, uvuvi, biashara ya usafirishaji, madini, ufugaji na utoaji wa huduma mbalimbali za kijamii kama vile afya na elimu.
Balozi Maajar alisema bado anaendelea na mikutano na idara zake ndani ya ubalozi kujua ni vitu gani ambavyo vitaweza kusaidia msukumo wa haraka wa kujitangaza kwa lengo la kuvutia watalii na wawekezaji kuvutiwa zaidi na Tanzania.
Kwa kuanzia, Balozi Majaar alisema kwanza utoaji wa visa ubalozini utakuwa wa haraka zaidi na ubalozi wenyewe utawekwa vivutio muhimu vya Tanzania.
“Nakata kuweka vivutio muhimu ukiingia tu mlango ujue upo Tanzania, tunatarajia kuweka vivutio muhimu mbele ya ubalozi kama picha za mlima Kilimanjaro, wanyama na picha tingatinga,” alisema.Balozi Maajar.