MAJAMBAZI wenye silaha, nusura wamteke Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Diodorus Kamala, ndani ya pori la Lugufu mkoani Kigoma.
Tukio hilo lilitokea juzi asubuhi, wakati Dk. Kamala alipokuwa akisafiri kwa gari akitoka Kigoma kwenda Tabora.
Watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wanaoishi katika kambi za Lugufu I na Lugufu II, waliweka mawe barabarani, kilometa chache kutoka katika kambi hizo.
Kilichomnusuru Dk. Kamala na ujumbe wake ni lori la mizigo ambalo liliwahi kufika eneo la tukio na kujikuta dereva na msaidizi wake wakitekwa na watu hao.
Baadhi ya polisi wenye uzoefu wa utendaji kazi katika eneo hilo, walisema watuhumiwa wa tukio hilo ni wakimbizi wanaoishi katika kambi hizo.
“Kila palipo na kambi ya wakimbizi, matukio ya utekaji nyara ni mengi, kuna wakimbizi wanaotoroka kambini, wanakwenda kufanya uhalifu na kisha wanarudi,” alisema mmoja wa polisi hao.
Mali kadhaa, zikiwamo fedha, simu selula na shehena mbalimbali, ziliporwa kutoka kwa wahanga wa tukio hilo la juzi.
Cha kusikitisha ni kwamba, polisi katika eneo hilo, hawana usafiri wa aina yoyote, zaidi ya kutegemea miguu.
Gari moja walilokuwa nalo lilipata ajali, lakini baada ya kutengenezwa, “wakubwa” wamelishikilia mjini Kigoma.
Dk. Kamala alishuhudia polisi zaidi ya 10 wenye silaha wakiwa na watuhumiwa wawili wa tukio hilo, lakini wakiwa hawana usafiri japo wa baiskeli.
Matukio ya ujambazi katika mikoa ya Kigoma, Kagera, Tabora na Rukwa, yanaonekana kuwa ya kawaida. Wananchi wanaporwa mali, na wengine wanauawa na wahalifu hao.
Wiki kadhaa zilizopita, ofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wilayani Kibondo, aliuawa na watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi kutoka nchi jirani.
Kabla yake, dereva teksi na abiria kadhaa alipigwa risasi na kuuawa katika eneo hilo.
Kutokana na mauaji ya kutisha yanayoendelea, magari ya abiria na mengine ya kawaida, sasa yanasindikizwa na polisi wenye silaha.
Hata hivyo, polisi hao wanafanya kazi katika mazingira magumu mno, wengine wakilazimika kuomba lifti za baiskeli wakati wakitaka kurejea katika vituo vyao vya kazi baada ya kusindikiza magari hayo.
Kwa hali ilivyo, watumishi wengi wa vyombo vya ulinzi na usalama wanajiona kama waliosahaulika, huku wenzao wa mjini wakifaidi mazingira yenye unafuu wa kazi.