Na Mohammed Mhina wa Jeshi la Polisi, Moshi
ALIYEKUWA Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Inspekta Jenerali mstaafu Omari Mahita, amesema kuwa ataendelea kuwa askari mwaminifu kwa jeshi hilo na taifa hadi atakapoaga dunia.
Mahita alisema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumaliza kukagua gwaride lililoandaliwa kwa ajili yake wakati wa sherehe ya kumuaga rasmi iliyofanyika kwenye viwanja vya Chuo cha Polisi cha Kimataifa cha CCP Moshi mkoani Kilimanjaro.
Mahita alisema kuwa changamoto iliyopo hivi sasa katika kutokomeza uhalifu, ni kuwashirikisha wananchi katika kutoa taarifa za wahalifu na mbinu wanazozitumia.
Alisema kuwa kama kila mwananchi atajitokeza kuwafichua wahalifu, kazi ya Polisi itakuwa rahisi kwa sababu kila kundi litakalojitokeza litabainika na kukamatwa mmoja baada ya mwingine na hivyo kuliacha taifa kuwa salama.
Awali, Mahita aliwaaga wananchi kwa kutumia gari la wazi la Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) akisindikizwa na mrithi wake Inspekta Jenerali Saidi Mwema.
Koplo Herman Dunstan, mwenye nambari E.1125 wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia mkoani Kilimanjaro, ndiye aliyejijengea historia pekee katika maisha yake kwa kuwaendesha Ma-IGP wawili kwa wakati mmoja wakati wa sherehe hizo.
Akizungumza mara baada ya shughuli hizo, Mkuu wa zamani wa Jeshi la Polisi nchini Inspekta Jenerali mstaafu Samwel Pundugu, alisema kuwa Mahita ataendelea kukumbukwa na vizazi vya sasa na vijavyo kama mpigania uhuru na mjenzi wa Afrika mpya.
Pundugu ambaye alikuwa Mkuu wa tatu wa Jeshi la Polisi nchini aliyeliongoza jeshi hilo kwa kipindi cha miaka miwili tu kuanzia mwaka 1973-1975, aliwaasa polisi kuiga mfano ulioonyesha na Mahita wakati akiwa kiongozi wa jeshi hilo na kwamba kwa kufanya hivyo watafanikiwa katika utumishi wao wa umma.
Naye Kamishna wa Polisi mstaafu Hussein Rashid, alisema kuwa uhalifu unaotokea hivi sasa ni wa kisomi zaidi ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
Alisema kuwa Polisi waliobaki kazini hivi sasa wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kushinda vita dhidi ya uhalifu.
Rashid alipongeza ubunifu uliofanywa na Mkuu wa Jeshi la Polisi aliyestaafu IGP Mahita kwa kuboresha makazi na vifaa vya mawasiliano kwa askari wake na hata kubadilisha namba za magari ya jeshi hilo ikilinganishwa na miaka iliyopita ambapo kulikuwa hakuna tofauti ya namba za magari ya Polisi na Idara ya Maji, Misitu ama Kilimo.
Sherehe hizo zilihudhuriwa na maafisa wakuu wa Jeshi la Polisi waliostaafu wakiongozwa na IGP Pundugu, Harun Mahundi na Makamishna Hussein Rashidi, Wakurugenzi wa zamani wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Edwin Mann na Adadi Rajabu.Wengine ni Kamishna Jafari Mustafa wa Zanzibar na viongozi mbalimbali wa vyombo vya ulinzi na usalama, majaji na viongozi wa serikali na vyama vya siasa.
IGP Mahita Mwenye umri wa miaka 60, mwezi mmoja na siku 19 amelitumikia Jeshi la Polisi kwa miaka 38 na kati ya hiyo, miaka 10 alikuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini