Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Kundi la wanamtandao limeipindua CCM asili’
Kundi la wanamtandao limeipindua CCM asili’
By Habari Tanzania | Published  10/12/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Mwandishi Wetu

MKUU wa Idara ya Sheria wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Sengondo Mvungi, amesema kundi maarufu linalojulikana kwa jina la wanamtandao limechukua madaraka kamili ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mvungi, daktari wa falsafa katika masuala ya sheria na mgombea urais wa NCCR katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, alisema hakuna mtu asiyejua siri hiyo ya wanamtandao kukipindua chama hicho tawala.

Akizungumza kwa kujiamini wakati wa mahojiano aliyofanya katika kipindi cha ‘Je, Tutafika’ kinachorushwa na televisheni ya Channel ten, Mvungi alisema hali hiyo imesababisha mabadiliko makubwa katika mwenendo wa mambo ndani ya chama hicho.

“Hivi sasa kundi la wanamtandao limekipindua Chama Cha Mapinduzi,” alisema Mvungi ambaye kabla hajaendelea na maelezo zaidi, mwendesha kipindi hicho, Makwaia wa Kuhenga aliamua kumkatisha kwa kusema: “Ndugu watazamaji wa kipindi hiki, ninachojua mimi ni kwamba CCM bado kipo, kwa hiyo alichokisema Dakta Mvungi hapa ni maoni yake binafsi.”

Hatua hiyo ilimfanya mwanasiasa huyo kukatisha hoja yake hiyo na akaihitimisha kwa kusema; “haya tuendelee, hakuna siri katika hilo, kila mtu anajua.”

Tanzania Daima ilipowasiliana kwa simu jana na Dk. Mvungi ili kupata ufafanuzi kuhusu kauli yake hiyo, mwanasiasa huyo alisema kwamba, kundi la wanamtandao lilianza kujipambanua waziwazi wakati wa mchakato uliomweka Rais Jakaya Kikwete madarakani, katika hatua ya kuteuliwa na chama chake kuwa mgombea.

“Hicho ndicho nilichokiona mimi binafsi katika mchakato. Tuliona kundi la mtandao likikaa pembeni na kuwapaka matope wazee. Hali hiyo ilisababisha kuwapo kwa CCM-asilia na CCM-mtandao.

Dk. Mvungi alisema kundi hili ndilo lililoongoza harakati za kuwapaka matope na kuibua kashfa dhidi ya baadhi ya wazee ndani ya CCM ambao hata hivyo hakuwataja kwa majina.

“Mimi naamini hata kama kungekuwa na makundi mawili ndani ya chama hicho, basi yangeshindana kwa hoja na si kwa kashfa… huo ndiyo mtazamo wangu na wala si wa chama.

“Ninachosema mimi ni kwamba, hawa watu wamepinduana kwa kashfa siyo kwa hoja. Rais mwenyewe hajasema hana mtandao. Hata hivyo kwangu mimi, jambo la muhimu si kupinduana bali je kile walichoahidi watatupa?” alihoji Dk. Mvungi.

Alipoulizwa ana maoni gani kuhusu serikali, Dk. Mvungi alisema anachokiona yeye ni jitihada za wanamtandao ambao aliwafananisha na wasanii, kutoa ahadi ambazo hawawezi kuzitekeleza.

“Leo mtu anaahidi kuna majenereta ya umeme, halafu kesho unaambiwa hata hiyo kampuni itakayoleta haipo. Hawa wanamtandao ni wasanii. Mimi naona tumedanganywa na hawa wasanii. Wananchi hawatapata maisha bora waliyoahidiwa kwa kuwa wanamtandao wameanza kugawana mafungu,” alisema Dk. Mvungi.

Taarifa kwamba kuna kundi la wanamtandao ndani ya CCM, zilibainishwa na Kikwete mwenyewe Mei mwaka jana katika Ukumbi wa Chimwaga, Dodoma, alipokuwa akiwashukuru wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM kwa kumchagua kwa kura nyingi kuwa mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho, akiwabwaga washindani wake wakuu wawili, Salim Ahmed Salim na Profesa Mark Mwandosya.

Dk. Mvungi anakuwa mwanasiasa wa kwanza kueleza hadharani namna alivyoutathmini mchakato wa ndani ya CCM nchini kueleza namna anavyokiona Chama Cha Mapinduzi ambacho miezi miwili na nusu iliyopita kilipata uongozi mpya chini ya uenyekiti wa Rais Jakaya Kikwete.

Tangu Kikwete alipotamka neno mtandao, kumekuwa na maneno mengi ya chini chini kuhusu kundi hilo na wakati fulani wakati alipokuwa akielekea kuunda Baraza la Mawaziri, kulikuwa na hisia kwamba wengi wa mawaziri ambao walionekana kuwa nje ya wanamtandao wangekosa nafasi za uwaziri.

Hata hivyo, kwa mshangao wa wengi, Kikwete aliunda baraza hilo akijumuisha watu ambao walikuwa wakitajwa kuwa nje ya kundi hilo la wanamtandao lililotokea kuwa na ushawishi mkubwa kisiasa.

Miongoni mwa watu wanaotajwa kuwa vinara katika kundi hilo la mtandao ni Waziri Mkuu, Edward Lowassa, aliyekuwa mwenyekiti wa vikao vyote vya wanamtandao vilivyosimamia mchakato wa kuhakikisha Kikwete anapitishwa na CCM kuwa mgombea wao wa urais.

Mbali ya Lowassa, mmoja wa makada maarufu ndani ya CCM, mchapakazi na rafiki wa karibu wa Rais Kikwete, wengine waliokuwa naye katika timu hiyo ni, Bernard Membe, Stephen Wassira, Emmanuel Nchimbi, Rostam Aziz na Mohammed AbdulAziz kwa kuwataja wachache.

Mbali ya hao, watu kama Yussuf Makamba, Aggrey Mwanri na Jaka Mwambi ambao wote wanaunda sekretarieti mpya ya CCM, wanatajwa kuwa watu ambao wamekuwa karibu na Kikwete ndani na nje ya mtandao kwa miaka mingi.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.