JESHI la Polisi Zanzibar limemuua mtu mmoja kwa kumpiga risasi na kujeruhi wawili, baada ya kuwatuhumu kuwa ni majambazi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Ramadhan Khatib Shaaban, alisema kwamba tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia jana majira ya saa 7:00 katika Mtaa wa Mwembeladu.
Kamanda Shaaban alisema hadi sasa mtu aliye kufa bado hajafahamika, na kuwataja majeruhi kuwa ni Hussein Omar Abdalla (33), mkazi wa Dar es Salaam na Hassan Mohammed Hassan (23), mkazi wa Amani, mjini Zanzibar.
Hata hivyo watuhumiwa hao wote si miongoni mwa wale ambao Jeshi la Polisi liliwatangaza mwanzoni mwa mwezi huu kuwa ni majambazi, ambao wamekuwa wakiendesha vitendo hivyo Zanzibar na Tanzania Bara.
Kamanda Shaaban alisema kwamba, katika tukio hilo, watu saba wanashikiliwa akiwamo Mohammed Ali Juma (20), mkazi wa Kilwa, Adam Rajab Hussein (17), mkazi wa Kunduchi, Titu Ayoub Kibelelo, Mzee Haji, mkazi wa Kwamtipura, Unguja na Ibrahim Saleh.
Akizungumza na waandishi wa habari, alisema askari polisi wakiwa katika doria walipofika katika eneo la Maisra waliliona gari aina ya Toyota Hiace lenye namba za usajili ZNZ 36634 na kuanza kulifuatilia.
Alisema baada ya gari hilo kulisimamisha, dereva wake hakusimama, na wakaendelea kulifukuza kupitia Mtaa wa Miembeni, Kijangwani hadi katika eneo la Mwembeladu.
Kamanda huyo alisema baada ya kufika katika eneo la Mfereji wa Wima watu hao walianza kurusha risasi na ndipo polisi walipolazimika kujibu mapigo.
Alieleza kwamba polisi walifanikiwa kuipiga risasi mipira yote ya nyuma gari walilokuwa wakisafiria na kuwajeruhi wawili kwa kuwapiga risasi za begani.
Hata hivyo, alisema polisi haijafanikiwa kukamata silaha, isipokuwa ilikamata vitu wanavyodhania kuwa ni milipuko ya baruti.
“Tuna wasiwasi huenda silaha waliitupa katika hilo eneo na baadhi ya wananchi wameificha,’’ alisema kamanda huyo.
Alisema kwamba wakati wakiwafukuza kuna vitu vingi walikuwa wakidondosha, lakini hata hivyo hakutaja vitu hivyo vilikuwa ni vya aina gani.
‘’Vitu hivi ni vya hatari, siwezi kukuonyesheni zaidi,’’ alisema huku akiwa ameshika mfuko wa rambo wenye nyaya na vitu vilivyofungwa kwenye magazeti.
Alisema bado ni mapema kumtaja mmiliki wa gari lililokamatwa.
Hata hivyo habari kutoka katika Hospitali ya Mnazi Mmoja walikolazwa majeruhi hao, zinasema kwamba, watu hao walisafiri kwa jahazi kutoka Dar es Salaam baada ya kukosa boti na kufika Zanzibar usiku.
Imeelezwa kwamba baada ya kufika katika Bandari ya Kizingo, mmoja wa abiria alikwenda kupokewa na gari hilo na wengine kuomba lifti.
Hata hivyo, baada ya kutoka katika eneo hilo na gari majira ya saa 7:00 usiku walifuatwa na gari aina ya Land Rover, na baada ya kufika katika eneo la Mfereji wa Wima, walianza kusikia risasi zikirushwa nyuma yao.
Gari lililokuwa likitumiwa na watu hao limekutwa na matundu ya risasi zaidi ya 10, pamoja na damu ikiwa imetapakaa kwenye viti