MWENYEKITI wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Augustine Mrema, amesema leo atatoa ukweli kuhusu kifo cha mwanamke aliyezaa naye, Angelina Mushi ambaye alifia katika nyumba ya kulala wageni iliyopo Kawe Kisalasala, jijini Dar es Salaam.
Mrema alisema kuwa vyombo vya habari vinaandika mambo wasiyoyajua na kuwa leo atatoa ukweli kuhusu suala hilo.
Huku akizungumza kwa hamaki, Mrema alisema kuwa hakuna mtu asiyemfahamu mke wake na mpango wa kusema kuwa alizaa na mwanamke ambaye kwa sasa ni marehemu, analifahamu hilo.
“Sitaki mnichimbe kwa mambo yasiyo na msingi, nataka muongee mambo ya jamii, ya kuendeleza jamii na kushughulikia matatizo ya wanajamii. Naombeni muachane na hizo habari, na mkaandike kuhusu matatizo ya wanafunzi na kuvunjiwa kwa haki watu wa Jangwani,” alisema Mrema.
Alisema hiyo ni mipango imepangwa ili kumchafulia jina lake. “Naelewa kila kitu ambacho kimetendeka hadi watu wananipakazia. Mimi mke wangu ni huyu hapa (huku akimuonyesha Rose), narudia tena, nadhani wote mmemuona hakuna haja ya kuhoji kuwa nina mke mwingine,” alisema Mrema.
Akizungumza huku aking’aka na kuvua kofia alisema kuwa, kuna mwandishi amemvunjia heshima kwa kuwa alimuuliza swali kama hilo mbele ya mke wake.
Mwanamke anayedaiwa kuzaa na Mrema, Angelina Mushi, alifariki dunia katika nyumba ya wageni eneo la Salasala Kawe, jijini Dar es Salaam, wiki mbili zilizopita.
Shabani Matutu anaripoti kuwa; hadi jana mchana, mwili wa Angelina ulikuwa bado upo katika Hospitali ya Muhimbili na kwamba ndugu zake waliokuwa wamejitokeza kuuchukua juzi kwa ajili ya mazishi, hawakutokea kama walivyoahidi.
Ofisa Uhusiano wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Jeza Waziri, aliithibitishia Tanzania Daima kuwa, ndugu wa marehemu ambao awali juzi walifika hospitalini hapo, hawakuweza kufika mpaka saa 9 mchana jana.
“Hata mimi nilipata habari kuwa ndugu zake walifika juzi na jana walitarajia kurudi kuchukua mwili wa ndugu yao, tayari kwa mazishi, lakini cha kushangaza mpaka sasa hawajajitokeza,” alisema Waziri.
Habari zinasema kuwa kwa sababu mwili wa marehemu huyo haukuchukuliwa jana na ndugu zake, hospitali imechukua jukumu la kuukabidhi kwa Halmashauri ya Jiji tayari kwa mazishi leo.
Habari zinasema kuwa, sheria ya hospitalini hapo inasema mwisho wa kuhifadhi mwili wa marehemu ni wiki moja na baada ya hapo anakabidhiwa kuzikwa na Halmashauri ya Jiji.
Mmoja wa maofisa wa hospitali hiyo amesema kuwa, hospitali hiyo imefanya uungwana kwa kuuhifadhi mwili huo mpaka sasa ambapo umefikisha siku 28