Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Makamba: Nitawarudishia Maalim Seif ndani ya CCM
Makamba: Nitawarudishia Maalim Seif ndani ya CCM
By Habari Tanzania | Published  10/11/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Kulwa Karedia

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Luteni Yusuf Makamba, amesema ataendelea na kasi ya kusomba viongozi wa vyama vya upinzani, na safari hii amepania kumrejesha katika chama hicho tawala, Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad.

Makamba alisema hayo jana wakati akifungua kikao cha siku mbili cha Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), katika Ofisi Ndogo za CCM Lumumba, Dar es Salaam.

Makamba alisisitiza kuwa chama hicho kitaendelea na wimbi lake, kwa vile viongozi wanaorejea ndani ya CCM hawalazimishwi na mtu, bali wanafanya hivyo kutokana na sera nzuri za chama hicho.

“Nitaendelea na wimbi la kuwapokea viongozi wa upinzani wanaorudi CCM, kwa vile wengi wanaokuja wanafuata sera zetu nzuri, ambazo zimetuwezesha kuwa madarakani kwa kipindi chote hiki, lakini hawa huwa hawalazimishwi na mtu, bali hutokana na sera zetu kuwa bora,” alisema Makamba.

Alisema kutokana na hali hiyo, amemwalika Katibu Mkuu wa CUF, Seif Sharif Hamad, naye kurejea CCM, kwa vile ndicho chama kinachokubaliwa na wananchi wengi kuliko CUF.

“Namwalika Maalim Seif kama anataka arudi CCM, kwani milango iko wazi kwake. Tutampokea kwa mikono miwili, kwa vile chama hiki bado ni imara na kasi ya watu wanaojiunga nacho inaonyesha wazi tunakubalika, tunamkaribisha kwa mikono miwili,” alisema Makamba.

Alisema mbali ya kumkaribisha Maalim, CCM ilipata pigo wakati mmoja wa wana CCM aliyekuwa na nguvu zaidi, Augustine Mrema, alipohama chama hicho na kujiunga na kambi ya upinzani. Alisema CCM ilipata mshituko mkubwa, lakini ilifikia wakati walizoea.

“Tulipata mshutuko Mrema alipoamua kuhamia upinzani, kwa vile wakati ule alikuwa na nguvu kubwa, lakini tulikwenda hivyo tukazoea, sasa kama wanakuja wenyewe, tutaendelea kuwapokea tu, kwani umma hauwezi kukusanywa kwa viboko, bali umekubali sera zetu,” alisema Makamba.

Alisema tangu kuteuliwa kwa sekretarieti hiyo miezi miwili na nusu iliyopita, imeanza kufanya kazi zake kwa ufanisi mkubwa, tofauti na madai yaliyotolewa siku za karibuni kuwa sekretarieti imeshindwa kuonyesha mabadiliko yoyote.

“Toka tumeteuliwa tuna miezi miwili na nusu iliyopita, lazima tupime utendaji wetu wa kazi, viongozi wengi nimesoma ripoti zenu mlipokuwa kwenye ziara mikoani…nimefurahishwa kuona kila sehemu wananchi wameonyesha imani kubwa kwetu, nanyi mnatekeleza majukumu yenu,” alisema Makamba.

Tangu ashike wadhifa huo, Makamba amekuwa akisafiri huku na kule, na katika kipindi chake, viongozi watatu kutoka upinzani wakiwamo wawili ambao walishindwa kwenye ubunge kwenye vyama vyao walijiunga na chama hicho tawala.

Jitihada za kuwasiliana na Maalim Seif ambaye aliondoka CCM mwaka 1988, baada ya kutoelewana na aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Abdul Wakil Nombe, ili kupata maoni yake kuhusu kauli hiyo ya Makamba hazikuzaa matunda, kwani simu yake iliita kwa muda mrefu bila ya kupokewa.

Mmoja wa viongozi wa CUF walio karibu na Maalim Seif, Jussa Ismael, alipoulizwa kuhusu hilo, alisema: “Tunaisubiri kwa hamu hiyo siku ambayo Maalim atajiunga.”

Viongozi waliovihama vyama vyao na majina ya vyama vyao kwenye mabano ni Tambwe Hiza (CUF), Dk. Amaan Walid Kabourou (CHADEMA) na Jacob Nkomola (SAU).

Tambwe alikuwa Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Sera wa CUF, wakati Kabourou alikuwa Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA na Nkomola alikuwa Katibu Mkuu wa SAU, na kabla ya hapo, alikuwa miongoni mwa viongozi wa mwanzo wa CHADEMA.

Katika hatua nyingine, vuguvugu la kampeni za chini kwa chini limeanza miongoni mwa wagombea wa nafasi ya ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki kupitia CCM.

Hali hiyo ilianza kuonekana tangu jana wakati wagombea hao walipoitwa mbele ya Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama, Makao Makuu ya Ofisi Ndogo, CCM Lumumba, kwa ajili ya kujadili baadhi ya mambo muhimu, kabla ya kwenda Dodoma ambako uchaguzi huo utafanyika.

Miongoni mwa wagombea hao yumo Dk. Kabourou, Rogers Jacob Shemvelekwa, Anamringi Isaya Macha, Mbwana Rajabu Kambangwa na Addo Aloyce Mwasongwe.
Uchaguzi wa wabunge hao unatarajiwa kufanyika mara baada ya kuanza kwa kikao kijacho cha Bunge, kitakachoanza Oktoba 30, mjini Dodoma.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
This article has been added to your 'Articles to Read' list.
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.