WANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, wameanza kuvunja ukimya na kuzungumzia suala la mpasuko wa kisiasa, ambalo Mwenyekiti wao, Rais Jakaya Kikwete, amesema amefika pazuri kulipatia ufumbuzi.
Wanachama hao wa CCM, wakiwamo viongozi wa matawi, wamekuwa wakitoa maoni yao kupitia vikao vya Naibu Waziri Kiongozi, Ali Juma Shamhuna, ambaye anazunguka kuzungumza na viongozi hao katika kuimarisha chama.
Katika Tawi la CCM Fukuchani, Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja, wana CCM hao walisema kama kiongozi yeyote wa CCM atakwenda na ajenda ya kuwaeleza masuala ya kuwapo serikali ya mseto, watamkimbia katika kikao na kumwacha peke yake.
“Kama kiongozi yeyote atakuja kutuelezea suala hilo, tutamkimbia na kumwachia kikao,” alisema Hamdu Bakar.
Mjumbe mwingine wa Halmashauri Kuu ya Tawi la Fukuchani, Faki Ame Wadi, alisema kimsingi Zanzibar hakuna mpasuko wa kisiasa kama inavyodaiwa. Alieleza kwamba sula la uchaguzi limekwisha na hivi sasa imebakia kazi moja tu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi.
Wanachama hao wa CCM walisema kwamba, katiba zote mbili zinaeleza wazi kwamba chama kinachopata ushindi mkubwa katika uchaguzi ndicho chenye mamlaka ya kuunda serikali, kwa kuteua mawaziri, makatibu wakuu na watendaji wengine serikalini.
“Uchaguzi umemalizika na CCM ndiyo iliyoshinda, hivyo hoja ya kuundwa kwa serikali ya mseto haina msingi wowote,” alisema Ame.
Katika kikao hicho, Shamhuna aliwataka viongozi hao kuhakikisha wanachama wanalipa ada, kwa vile ndio uhai wa chama.
“Kama wanachama hawatawajibika kulipa ada zao chama kitayumba na kuwa legelege, na msisahau kwamba bila ya CCM imara, nchi hii itayumba,” alisema Shamhuna.
Alieleza kwamba chama kimeweka kiwango cha chini cha ada, ili kuhakikisha kwamba wanachama wanamudu kiwango hicho.
Alisema kwamba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), pamoja na kutopata kiti hata kimoja kisiwani Pemba, kitaendelea kupeleka maendeleo kwa wananchi wa kisiwa hicho.
Naibu Waziri Kiongozi huyo alisema kwamba, tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu, serikali imefanikiwa kwa kiwango kikubwa kuimarisha miundombinu ya huduma za maji safi, elimu na umeme.
Hata hivyo, alisema ni aibu kwa kiongozi wa CCM kujitokeza kuomba kuchaguliwa, wakati idadi kubwa ya familia yake ni washabiki wa vyama vya upinzani.
Alieleza kwamba viongozi kama hao lazima kwanza waanze kushawishi familia zao kujiunga na CCM.
Tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu mwaka mmoja uliopita, kumejitokeza mpasuko mkubwa wa kisiasa kati ya vyama vya CCM na Chama cha Wananchi (CUF), ambapo CCM ilipata ushindi mkubwa Unguja na CUF kuchukua viti vyote vya Pemba.
Viongozi wengi, wakiwamo wasomi maarufu nchini na nje ya nchi, wamekuwa wakishauri kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa, ili kumaliza mpasuko huo.
Chama cha CUF kiliweka bayana katika kampeni zake za uchaguzi kwamba iwapo kingeshinda, kingeunda serikali ya umoja wa kitaifa.
Hata hivyo, kwa upande wa CCM Zanzibar, suala hilo limekuwa gumu, licha ya kuzungumzwa katika hadidu rejea za muafaka uliosainiwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Philip Mangula na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad.
Baada ya Rais Kikwete kusema amefika pazuri katika kushughulikia muafaka huo, aliungwa mkono na Maalim Seif, aliyesema wanajua kwamba kweli amefikia pazuri, wakati Kiongozi wa Upinzani bungeni ambaye pia ni kiongozi wa CUF, Hamad Rashid Mohamed, alitaka Rais aonyeshe kwa vitendo. Shamhuna alitoa kauli mwishoni mwa wiki iliyopita kwamba, katu hapatakuwapo serikali ya mseto Zanzibar