Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Urafiki wa Rais Kikwete, wanafunzi wafika tamati!
Urafiki wa Rais Kikwete, wanafunzi wafika tamati!
By Habari Tanzania | Published  10/10/2006 | Habari za Kitaifa | Rating:
Asha Bani na Mkolo Kimenya

UKARIBU uliojengeka kati ya wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu nchini, hususan wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam na Rais Jakaya Kikwete, ulioanza kujengeka tangu akiwa mgombea urais mwaka jana, sasa unaonekana kuanza kufikia tamati.

Mwanzo wa kuhitimishwa kwa urafiki huo uliendelea kuonekana jana, wakati wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), walipoitisha mkutano wa waandishi wa habari, na kueleza dhamira yao ya kuandamana kwenda hadi Ikulu, kufikisha kilio chao cha kunyimwa mikopo.

Katika tamko lao la jana, wanafunzi hao chini ya uongozi wa chama chao cha Wanafunzi Waliokosa Udhamini (TAHUSO) waliiomba serikali kutoa tamko la kuwapatia mikopo wale ambao hawajapata mikopo hadi kufikia Jumapili ijayo ya Oktoba 15, vinginevyo wataandamana kwa ajili ya kumuona rais mwenyewe.

Hali hiyo, imekuja katika kipindi kisichozidi mwaka mmoja tangu Kikwete agawe kadi za uanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kundi kubwa la wanafunzi wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam na baadaye wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, waliokuwa wamejitoa kuunga mkono sera za elimu za CCM wakati akiwa mgombea urais.

Hata kabla ya kugawa kadi hizo, Kikwete mwenyewe wakati alipotangaza dhamira yake ya kugombea urais, Kibaha mkoani Pwani, alisema alikua amefikia uamuzi huo baada ya kushauriwa kufanya hivyo na makundi mbalimbali ya kijamii wakiwamo wasomi.

Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake jana, Mwenyekiti wa TAHUSO, Bruno Ngingo, alisema iwapo serikali haitakuwa imetoa tamko hadi kufikia siku hiyo, wataandamana kwa amani katika maandamano ambayo yatawashirikisha wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo mbalimbali vya elimu ya juu, ili kuishinikiza serikali kuliangalia suala hilo upya.

Mwenyekiti huyo alisema wamefikia uamuzi huo baada ya kubaini kwamba, barua ya kwanza waliyoiandika Julai 26 kwenda serikalini, haikujibiwa, na wanafunzi waliendelea kusota kabla ya kuandika ya pili, Agosti 8 ambayo nayo haikujibiwa na kusababisha wengine walazimike kurudi majumbani kwao kwa kukosa mikopo hiyo.

Alisema sera ya serikali ya kuweka mgawanyo katika utoaji mikopo kwa kuzingatia daraja la kwanza na la pili, haijawatendea haki wanafunzi wake waliopata nafasi ya kujiunga na masomo chuoni hapo.

“Suala la kutoa mikopo kwa kigezo kuwa hadi uwe umepata daraja Fulani, kwa kweli kwanza ni kama kudhalilishana kwa sababu inaonekana kama wengine hawakustahili kujiunga na masomo katika vyuo walivyochaguliwa,” alisema Ngingo.

Alisema wazazi wa wanafunzi wengi ni wakulima na wengine hawana uwezo wa kuwalipia, hivyo inawawia vigumu kuendelea kupata elimu bila kuwa na mikopo kutoka serikalini.

Wakati hayo yakiendelea, baadhi ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliopata mkopo wametishia kugoma tena, kwa madai fedha walizopewa ni kidogo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Tanzania Daima baada ya kumalizika mkutano wao jana, baadhi ya wanafunzi hao walisema kuwa, sh 175,000 walizopewa kwa siku 50 zimekwisha tangu Oktoba 7, hivyo wanaishi kwa shida.

“Hadi sasa tunashangaa kuona bodi imekaa kimya bila ya kuona utaratibu wowote unachukuliwa wa kupatiwa mikopo yetu, na siku 50 zimeisha na kupita, tunachokula tunakijua wenyewe,” alisema mmoja wa wanafunzi hao.

Katika mkutano huo, wanafunzi hao walikuwa wakipiga kelele na kuushinikiza uongozi chuoni hapo kujiuzulu kutokana na kutowatatulia matatizo yao.

Hali hiyo ilitokana na mmoja wa wanafunzi hao kuuliza kwa nini magari ya chuo ambayo wanayatumia kwa usafiri, yanawashusha mbali na chuoni hapo na kusababisha kutembea kwa miguu kwa umbali mrefu.

Viongozi hao walijibu kuwa, hawana taarifa wakati wanafunzi hao wanadai kuwa taarifa hizo wanazo siku nyingi, bali ni utendaji wao hauwaridhishi.

Wakati huohuo, uongozi wa chuo hicho umewapatia barua wanafunzi watano, akiwamo Waziri wa Mikopo kutoka Serikali ya Wanafunzi (DARUSO), kujieleza wakituhumiwa kuhusika kuwa vinara wa mgomo uliotokea hivi karibuni.

Akizungumza katika mkutano wa wanafunzi uliofanyika jana chuoni hapo, Rais wa wanafunzi hao, Mwita Magessa, alisema kuwa wanafunzi hao walipewa barua za kujieleza kutokana na uongozi wa chuo kuwaona kuwa wao ndio walikuwa vinara wa mgomo huo wakati si kweli.

“Barua za kuwataka kujieleza kwa wanafunzi hao, zimetoka katika uongozi wa juu wa utawala wa chuoni hapo na zimesainiwa na Profesa Mshana, ambazo aliwakabidhi Agosti 28 na kuwapa siku mbili kujieleza.

‘Waliopewa barua ya kujieleza kutokana na kutuhumiwa kwa mgomo huo ni Waziri wa Mikopo Kitivo cha Fani za Jamii, Julius Mtatiro, Nyanda Peter, Mtembwa Hussein, Makoye Benedict na Shigole. Wote ni wanafunzi wa mwaka wa tatu,” alisema.

Hata hivyo, Magesse aliwasihi wanafunzi kuwa watulivu na kuangalia uongozi wa chuo utaamua nini endapo wanafunzi hao watajieleza, na kuongeza kuwa endapo watasimamishwa au kufukuzwa chuo, wataandamana na kufanya mgomo mwingine.

“Mgomo ule haukuwa wa wanafunzi watano waliopewa barua ya kujieleza, ulikuwa ni uamuzi wa serikali ya wanafunzi DARUSO, ambao walikaa kikao na kushinikiza mgomo huo na si kama uongozi wa chuo unavyodhania,” alisema Magesse.

Septemba 15, mwaka huu, wanafunzi wa mwaka wa kwanza ambao walikuwa hawajapatiwa mikopo na Bodi ya Mikopo, waligoma na siku mbili baadaye wanafunzi wote chuoni hapo waligoma.

Akizungumza baada ya migomo hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Nimrod Mkono, aliwaita wanafunzi hao waliogoma kuwa ni wahuni kwani wote waliokuwa wanastahili kuipata walikuwa wameshapewa.

Uamuzi wa serikali kuamua kuwapa mikopo wale tu waliopata madaraja ya kwanza na pili (kwa wasichana) katika mitihani yao ya kidato cha sita, ulitangazwa bungeni na Waziri wa Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Peter Msolla kabla ya kuungwa mkono na Rais Kikwete mwenyewe wakati alipokuwa akilihutubia taifa katika hotuba yake ya mwezi Julai, mwaka huu akiwa Mwanza.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments
  • Comment #1 (Posted by Majaliwa Hassan Majaliwa)
    Rating
    Jibu la habari hii linaweza kutolewa kwenye fumbo nene la mwandisha Nthelezi Nesaa aliyeko Canada.
    Kwani kiliokuwa kikiendelea hakina tofauti na fungate ya mabwege. Chuo kikuu wameanza kesho utawasikia madaktari nk nk nk
    Big up
     
Submit Comment


Article Options
This article has been added to your 'Articles to Read' list.
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.