Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Bomoa bomoa yazidi kuuma
Bomoa bomoa yazidi kuuma
By Habari Tanzania | Published  10/9/2006 | Habari za Kitaifa | Rating:
na Timothy Kahoho

DIWANI wa Kata ya Hananasif katika Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam, Abbas Tarimba, ni miongoni mwa wafanyabiashara waliopata hasara kubwa kutokana na amri ya serikali ya kuliweka jiji hilo katika hali ya usafi.

Tarimba alikumbwa na kimbunga hicho wiki iliyopita, pale askari wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni walipovunja duka lake la vifaa vya ujenzi lililopo Argentina, Manzese, wakati wa operesheni ya kuwaondoa wamachinga kuanzia Mwembechai hadi Barabara ya Shekilango.

“Sielewi ni kwa nini upande wa mbele wa jengo langu uvunjwe na askari wa manispaa bila ya kupewa kwanza taarifa ya maandishi na hata kuharibu tangi hili jipya la maji, wakati jengo hili lipo mbali sana na eneo la hifadhi ya barabara,” alilalamika Tarimba.

Diwani huyo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliyepata pia kuwa kiongozi wa klabu ya soka ya Yanga ya Dar es Salaam, alifika Alhamisi saa 6:00 mchana, na kukuta sehemu ya jengo lake hilo imeshabomolewa na askari wa manispaa hiyo na kuacha vitu vyenye thamani ya mamilioni ya fedha katika hatari ya kuibwa.

“Tangi lenye thamani ya sh laki saba limeharibiwa na mali nyingi zimeibwa na kusababisha biashara yangu kusisimama hadi leo,” amezidi kulalamika kada huyo wa chama tawala.

Diwani huyo amekuwa akiendesha duka la vifaa vya ujenzi, linaloitwa Smart Hardware Limited (SHL) kwenye jengo lake lililopo kando ya hifadhi ya Barabara ya Morogoro.

Mbali ya diwani huyo wa CCM kupatwa na janga hilo, wapo wafanyabiashara wengine waliokumbwa na kimbunga hicho na kuwafanya wapate hasara ya mamilioni ya fedha. Baadhi yao ni Simon Lewanga, anayemiliki baa mbili zilizopo Manzese, kando mwa Barabara ya Morogoro, na Thadei Massawe, wa Friends Corner Hotel Limited.

Lewanga ameelezea kusikitishwa kwake na kitendo cha kuvunjiwa kiambaza cha Rombo Silent Inn bila taarifa na kusababisha hasara ya sh milioni mbili na pia kuvunjiwa ukumbi wa mbele wa Kisare Bar bila kulipwa fidia na kusababisha hasara ya sh milioni tatu.

“Baa yangu ya Rombo iko mbali sana na eneo la hifadhi ya barabara, lakini wakaamua kubomoa bila hata kunitaarifu na kunifanya nipate hasara ya sh 2, 000, 000,” amelalamika Lewanga.

Mmiliki wa baa hizo amesema kuwa miezi mitatu iliyopita aliona maofisa wa manispaa hiyo wakitia alama ya ‘X’ kwenye ukuta wa Kisare Bar na kuambiwa kuwa angefidiwa kutokana na eneo lake kutumiwa kwa upanuzi wa barabara.

Naye mwanawe Massawe, Dismas Massawe, alieleza kushangazwa na askari wa halmashauri hiyo kuchukua hatua ya kubomoa ukuta wa ndani wa eneo la hoteli yao na kuhatarisha usalama wa magari ya wateja wa hoteli.

“Ukuta uliopo kando mwa barabara upo nje ya mawe ya mpaka wetu, lakini ni vipi wabomoe ukuta uliopo ndani ya eneo la hoteli?” alihoji kijana wa huyo.

Askari wa manispaa hiyo walibomoa kuta za baa nyinginezo na pia upande wa mbele wa nyumba kadhaa zilizosemekana kujengwa miaka ya 1960. Kati ya nyumba hizo ni ile yenye hati ya kumiliki ardhi Na. 48395, iliyotolewa Februari 25, 1989, ikionyesha kujengwa ndani ya kiwanja Na. 113, Kitalu ‘A’, eneo la Tandale.

Mwanahawa Kilimamula (35), alidai kuwa baba yake, hayati Mohamed Kilimamula, aliijenga nyumba hiyo kwenye miaka ya sitini, kisha akamilikishwa kiwanja hicho mwaka 1989, kabla ya upanuzi wa Barabara ya Morogoro.

Mwanamke huyo alisema kuwa, askari wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni walifika jana na kubomoa kiambaza cha mbele cha nyumba yao kwa kuingia meta tatu kutoka kwenye mawe ya mpaka wa kiwanja cha nyumba hiyo.

“Tumebomolewa kiambaza cha nyumba yetu na kuharibu kiwanda cha kushona nguo na pia kuvunja kabati,” alilalamika Mwanahawa.

Binti Kilimamula amedai kuwa kitendo cha kuvunjwa kwa kipande cha nyumba yao kumesababisha uharibifu mkubwa na kuwaletea hasara ya sh milioni 25.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.