Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Mpasuko wawavuruga vigogo wa CCM Z’bar
Mpasuko wawavuruga vigogo wa CCM Z’bar
By Habari Tanzania | Published  10/9/2006 | Habari za Kitaifa | Rating:
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

JITIHADA za Rais Jakaya Kikwete kutafuta suluhisho la kudumu la mpasuko wa kisiasa wa Zanzibar, zinaonekana kuanza kuwavuruga viongozi wakuu wa Zanzibar.

Tukio la hivi karibuni kabisa linalotoa mwelekeo lilitokea majuzi ndani ya kikao cha Kamati Maalum ya CCM Zanzibar kilichokutana mwishoni mwa wiki ambacho kilishuhudia kuibuka kwa mabishano makali ya hoja, zote zikihusisha ajenda hiyo hiyo ya mpasuko.

Habari ambazo Tanzania Daima imezipata kutoka ndani ya kikao hicho zinasema kwamba, mabishano hayo yalisababishwa na hoja ya Waziri wa Habari, Michezo na Utamaduni, Muhammed Seif Khatib, aliyehoji sababu hasa zilizomfanya Naibu Waziri Kiongozi, Ali Juma Shamhuna kutoa kauli zenye mwelekeo wa kuvuruga juhudi za Rais Kikwete katika kupata ufumbuzi wa kudumu wa tatizo la Zanzibar ambalo limedumu kwa miaka takriban 10 sasa.

Katika hoja yake ilielezwa kuwa, Waziri Khatib alitaka kupata ufafanuzi wa hoja ya Shamhuna ambaye hivi karibuni alikaririwa akieleza kwamba, hakutakuwa na serikali ya mseto Zanzibar kinyume na kile alichokielezea kuwa ni maneno ya mitaani yaliyokuwa yakisikika Zanzibar katika siku za hivi karibuni.

Naibu Waziri Kiongozi huyo alisema madai hayo yaliyozagaa mjini hapa ya kuwa kuna mpango wa kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa, ni propaganda za wapinzani na hakuna mpango kama huo.

Alisema uchaguzi Zanzibar umemalizika tangu Desemba mwaka 2005, serikali imekwishaundwa, na hakuna uchaguzi mwingine hadi mwaka 2010.

Alisema jukumu kubwa la wanachama wa CCM hivi sasa, ni kuelekeza nguvu zao zote kuwavuta wapinzani wenye ushawishi kujiunga na CCM ili iwe imara zaidi na kushinda 2010.

Shamhuna alitoa kauli hiyo siku mbili tu baada ya Rais Kikwete kuwaeleza wahariri wa habari aliokutana nao mwanzoni mwa mwezi huu kwamba, alikuwa amefikia mahali pazuri katika kupata ufumbuzi wa tatizo la kisiasa la Zanzibar.

Kilichoonekana kumgusa Shamhuna na pengine Serikali ya Mapinduzi Zanzibar baada ya kauli hiyo ya Kikwete, ni namna viongozi wakuu wa Chama cha Wananchi (CUF) ambacho ndicho mahasimu wakuu wa CCM Visiwani, walivyoipokea kauli hiyo ya rais wakisema walikuwa na imani nayo.

Habari zaidi kutoka ndani ya kikao cha kamati maalumu ambacho Khatib aliibua hoja ya kutaka maelezo ya Shamhuna, zinaeleza kwamba, baada ya hoja yake hiyo, Mwenyekiti wa kikao hicho, Amani Abeid Karume alikaririwa akisema watu walikuwa wamemnukuu vibaya Rais Kikwete, aliposema alikuwa amefikia mahali pazuri.

“Alichozungumza Rais Kikwete ni tofauti za Unguja na Pemba zinazojitokeza katika kipindi cha uchaguzi na wala si suala la kuundwa kwa serikali ya mseto,’’ alisema Rais Karume katika kauli yake iliyoonekana kuunga mkono kauli ya Shamhuna.

Hali hiyo inatokea wakati hivi sasa kukiwa na mjadala mkubwa Visiwani kuhusu mustakabali wa kisiasa wa visiwa hivi, tangu Kikwete atoe kauli hiyo, kundi moja likiamini kwamba kutakuwa na serikali ya umoja wa kitaifa karibuni, wakati jingine linaloungwa mkono na wahafidhina wenye mawazo ya aina ya Shamhuna. wakipinga hali hiyo.

Kikubwa kilichoifikisha Zanzibar hapo ilipo, ni kuendelea kuwapo kwa hali ya kutoaminiana kati ya CCM na CUF na namna Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ilivyosimamia chaguzi tatu zilizopita za vyama vingi za mwaka 1995, 2000 na 2005 ambazo mara zote ushindi wa CCM ulionekana kupingwa na CUF ambao wamekuwa wakidai kupikwa kwa matokeo.

Hali hiyo ya kupinga mwenendo wa uchaguzi ndiyo ambayo mwaka 2001 ilisababisha kuibuka kwa vurugu kubwa Visiwani hapa zilizoshuhudia watu zaidi ya 20 wakipoteza maisha na wengine wengi wakijeruhiwa.

Katika hatua nyingine, habari kutoka ndani ya kikao hicho zinasema, Rais Karume alitumia fursa hiyo kuwaonya wanasiasa wanaowania kumrithi ilhali akiwa bado madarakani

Habari zinasema Karume aliwaeleza kwamba, muda wa kurithi kiti cha urais wa Zanzibar bado haujafika, na kwamba watu wanatakiwa waendelee na kazi za maendeleo, kwa sababu Uchaguzi Mkuu utafanyika tena 2010, miaka minne tangu sasa.

Aliwaasa wale wote wanaowania kiti hicho, kuacha kufanya hivyo na wasubiri kwanza hadi wakati wa kampeni utakapoanza.

Kumekuwa na harakati nyingi za chini chini kuhusu urais wa Zanzibar, na kikubwa kinachoonekana sasa ni kutajwatajwa kwa baadhi ya majina ya wanasiasa wanaotarajiwa kugombea urais wa visiwa hivyo mwaka 2010.

Miongoni mwa majina ya wanasiasa wanaotajwa sana ndani ya CCM, ni pamoja na Waziri Kiongozi Zanzibar, Shamsi Vuai Nahodha; naibu wake, Ali Juma Shamhuna; Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani katika Serikali ya Rais Kikwete, Mohammed Aboud; Waziri Kiongozi wa zamani, Dk. Mohammed Gharib Bilal na Waziri wa Nchi (Mazingira), Dk. Hussein Mwinyi ambaye pia ni mtoto wa Rais mstaafu wa Tanzania na Zanzibar, Ali Hassan Mwinyi.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.