KATIKA makala nne zilizopita, nilipendekeza kwamba katika dola mseto kanuni ya mafiga matatu ya kitendo adilifu yaweza na inapaswa kutumika kama mizani huru ya maadili bila kujali dini wala utamaduni wa mtu.
Hii maana yake ni kwamba hii ni kanuni ya maadili yanayoweza kukubalika kwa watu wote wenye akili timamu, katika mataifa yote na katika milele yote! Yaani yenyewe ni “kanuni ya maadili-gumegume” (absolute moral law) zikiwa na msingi wake katika ukweli-gumegume (absolute truth).
Hata hivyo, baadhi ya wasomaji wamehoji uhalali wa pendekezo hili kwa madai kwamba hakuna kitu kinachoitwa maadili gumegume hapa duniani! Kwa maoni yao kitu pekee kilichopo ni kanuni za maadili tepetepe (relative moral laws) zikiwa na msingi wake katika ukweli tepetepe (relative truth).
Hoja yao ni kwamba kila mtu anautazama ukweli wa kimaadili kwa kutumia miwani ya utamaduni wake, miwani ya dini yake, miwani ya mazingira yake, na kadhalika. Baada ya kuisanifu vizuri hoja hiyo inaonekana kuwa na muundo ufuatao:
- Tamaduni tofauti duniani hutumia mizani tofauti ya maadili;
- Maadili maana yake ni kufanya wanachofanya wenzako;
- Hivyo, kutokana na madokezo mawili hapo juu, inafuata kwamba maadili hubadilika badilika kutoka utamaduni mmoja hadi mwingine;
- Aidha, kutokana na madokezo mawili hapo juu, na pia kutokana na hitimisho la hapo juu, kanuni ya jumla ni kwamba: ukienda Roma sharti uenende kama Warumi.
Lakini kwa bahati mbaya kabisa, kiwiliwili cha hoja hii kina makovu mengi sana yanayokatisha tamaa. Katika makala hii nakusudia kuiwekea hamira hoja hii ili iumuke kwa kiasi cha kutosha kuonyesha makovu hayo kwa kila msomaji.
Katika zoezi hili nitatumia mifano ambayo watetezi wa ‘itikadi ya maadili tepetepe’ wanaitumia kulinda hoja yao hii. Mifano inafuata:
Katika jamii ya Wamakonde hapa Tanzania supu ya nyama ya panya (samaki nchanga) ni halali kabisa; Kwa Watanzania baki kama vile Wasukuma, Wachaga na Wahaya, supu ya nyama ya panya ni habari nyingine.
Hivyo, watetezi wa itikadi ya maadili tepetepe wanahitimisha kwamba hakuna na haiwezekani pakawapo maadili gumegume, kwa maana kwamba ubaya au uzuri wa kitendo cha kula nyama ya panya unategemea utamaduni, dini, na mazingira mengine! Wanashauri kwamba mtu akienda Roma sharti aenende kama Warumi!
Katika jamii ya Wahehe hapa Tanzania supu ya nyama ya mbwa (mbuzi wa porini) ni halali kabisa; Kwa Watanzania baki, supu ya nyama ya mbwa ni habari nyingine, sana sana kutokana na imani kwamba nyama hiyo ni chungu sana.
Hivyo, watetezi wa itikadi ya maadili tepetepe wanahitimisha kwamba hakuna na haiwezekani pakawapo maadili gumegume, kwa maana kwamba ubaya au uzuri wa kitendo cha kula nyama ya mbwa unategemea utamaduni, dini, na mazingira mengine! Wanashauri kwamba mtu akienda Roma sharti aenende kama Warumi!
Katika Kanisa Katoliki ni haramu kwa mwanamke kupewa daraja la upadri, angalau kwa hoja kwamba, Kristo Kuhani Mkuu, hakuwa mwanamke; katika Kanisa la Anglikana na makanisa mengine ya Kipentekoste, ni ruksa wanawake kupewa daraja la upadri, angalau kwa hoja kwamba mbele ya Kristo watu wote ni sawa.
Hivyo, watetezi wa itikadi ya maadili-tepetepe wanahitimisha kwamba hakuna na haiwezekani pakawapo maadili-gumegume, kwa maana kwamba ubaya au uzuri wa kitendo cha kumpadirisha mwanamke unategemea utamaduni, dini, na mazingira mengine! Wanashauri kwamba mtu akienda Roma sharti aenende kama Warumi!
Wakristo wanaamini kwamba kuna Mungu mmoja mwenye nafsi tatu - Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu, ambapo Mungu Mwana ni Mungu - mtu; Waislamu wanaamini kwamba kuna Mungu mmoja mwenye nafsi moja tu, bila mtoto wala mjukuu.
Hivyo, watetezi wa itikadi ya maadili tepetepe wanahitimisha kwamba hakuna na haiwezekani pakawapo maadili gumegume, kwa maana kwamba ukweli kuhusu idadi ya nafsi alizo nazo Mungu asiye na dini unategemea utamaduni, dini, na mazingira mengine! Wanashauri kwamba mtu akienda Roma sharti aenende kama Warumi!
Katika Kanisa la Anglikana, matumizi ya kondomu kama kizuia mimba ni ruksa tangu mwaka 1931. Katika Kanisa Katoliki matumizi ya kondomu kama kizuia mimba ni mwiko. Hivyo, watetezi wa itikadi ya maadili tepetepe wanahitimisha kwamba hakuna na haiwezekani pakawapo maadili gumegume, kwa maana kwamba ubaya au uzuri wa kitendo cha kutumia kondomu kama kizuia mimba unategemea utamaduni, dini, na mazingira mengine! Wanashauri kwamba mtu akienda Roma sharti aenende kama Warumi!
Katika dini ya Wa-Mormon ndoa za mitala zinaruhusiwa kwa ujumla ilimradi tu mume awe na uwezo wa kuwatunza wake zake.
Katika dini ya Ukatoliki ndoa za mitala zinahesabiwa kuwa ni dhambi dhidi ya usawa wa binadamu ambapo, mwanamke na mwanamume, wote kwa pamoja wameumbwa kwa mfano wa Mungu.
Hivyo, watetezi wa itikadi ya maadili-tepetepe wanahitimisha kwamba hakuna na haiwezekani pakawapo maadili-gumegume, kwa maana kwamba ubaya au uzuri wa kitendo cha kuoa wake wengi unategemea utamaduni, dini, na mazingira mengine! Wanashauri kwamba mtu akienda Roma sharti aenende kama Warumi!
Katika jamii ya Wagiriki, ushoga ulihesabiwa kuwa sehemu ya maisha ya wastaarabu, kiasi kwamba Plato, Aristotle na wafalme wote wa dola ya Kirumi inaaminika walikuwa ni wateja wazuri wa mashoga.
Katika dini ya Ukatoliki, ushoga ni dhambi dhidi ya mwili ambao ni aina mojawapo ya matilaba ya binadamu, kwa maana kwamba hii ni tabia inayobomoa bawaba za ‘mlango wa nyuma’, kwa kuulazimisha uwe unafunguka kutokea sehemu zote mbili, kinyume cha maumbile yake asilia.
Hivyo, watetezi wa itikadi ya maadili-tepetepe wanahitimisha kwamba hakuna na haiwezekani pakawapo maadili-gumegume, kwa maana kwamba ubaya au uzuri wa kitendo cha kufanya ngono kupitia ‘mlango wa nyuma’ unategemea utamaduni, dini, na mazingira mengine! Wanashauri kwamba mtu akienda Roma sharti aenende kama Warumi!
Katika Kanisa la Anglikana, matumizi ya kondomu kama kizuia maambukizi ya magonjwa yatokanayo na ngono kama vile VVU ni ruksa.
Katika Kanisa Katoliki, matumzi ya kondomu kama kizuia maambukizi ya magonjwa yatokanayo na ngono kama vile VVU ni mwiko.
Hivyo, watetezi wa itikadi ya maadili-tepetepe wanahitimisha kwamba hakuna na haiwezekani pakawapo maadili-gumegume, kwa maana kwamba ubaya au uzuri wa kitendo cha kutumia kondomu kama kizuia-mimba unategemea utamaduni, dini, na mazingira mengine! Wanashauri kwamba mtu akienda Roma sharti aenende kama Warumi!
Katika jamii ya Wa-Nazi wa Ujerumani, chini ya uongozi wa Adolf Hitler, mauaji ya halaiki ya watu wenye asili ya Kiyahudi yalikubalika kimaadili. Tamaduni nyingine nyingi, ikiwamo Ujerumani ya leo, zinakiona kitendo hicho kama kitendo cha kinyama kwelikweli.
Hivyo, watetezi wa itikadi ya maadili-tepetepe wanahitimisha kwamba hakuna na haiwezekani pakawapo maadili-gumegume, kwa maana kwamba ubaya au uzuri wa kitendo cha mauaji ya halaiki unategemea utamaduni, dini, na mazingira mengine! Wanashauri kwamba mtu akienda Roma sharti aenende kama Warumi!
Katika jamii ya Waswazi wa Swaziland, kila mwaka ni halali kuendesha sherehe za ‘Ngoma ya Kiswazi’, ambapo wasichana wadogo hucheza wakiwa nusu-uchi mbele ya mfalme ili kumwezesha kuchagua msichana mmoja ambaye atakuwa mke wake wa nyongeza kama alivyofafanua mama yake Mfalme Mswati III juzi.
Hapa Tanzania ngoma za wasichana wadogo wanaocheza nusu-uchi ili waweze kuopolewa na kuolewa katika matabaka ya watawala kama wake wa nyongeza, zinachefua kama wanaharakati wa FemAct wanavyofafanua vizuri kabisa.
Hivyo, watetezi wa itikadi ya maadili-tepetepe wanahitimisha kwamba hakuna na haiwezekani pakawapo maadili-gumegume, kwa maana kwamba ubaya au uzuri wa kitendo cha kuwaoa wasichana wadogo na kuwafanya vyombo vya anasa za mwili kwa faida ya watu walio katika tabaka la watawala unategemea utamaduni, dini, na mazingira mengine! Wanashauri kwamba mtu akienda Roma sharti aenende kama Warumi!
Katika jamii za kale kabisa biashara ya utumwa ilikuwa ni halali, kwa maana kwamba binadamu alikuwa anaweza kukamatwa na kupelekwa mnadani na kisha akapigwa bei kama nguruwe ili aende kutumiwa na mnunuzi wake kadiri mnunuzi atakavyoona inafaa. Katika jamii za siku hizi, biashara ya utumwa inachefua, kwa sababu thamani ya kiutu aliyo nayo binadamu (human dignity) inapita bei zote.
Hivyo, watetezi wa itikadi ya maadili-tepetepe wanahitimisha kwamba hakuna na haiwezekani pakawapo maadili-gumegume, kwa maana kwamba ubaya au uzuri wa kitendo cha kumpiga bei binadamu mwenzako unategemea utamaduni, dini na mazingira mengine! Wanashauri kwamba mtu akienda Roma sharti aenende kama Warumi!
Aidha, watetezi wa itikadi ya ukweli-tepetepe (relative truth) wanasema kwamba, watu kabla ya enzi za Galileo na Copernicus waliamini, si kwamba dunia inalizunguka jua, bali kwamba jua linaizunguka dunia. Watu baada ya Galileo na Copernicus, tunaamini, si kwamba jua linaizunguka dunia, bali kwamba dunia ndiyo inalizunguka jua.
Hivyo, watetezi wa itikadi ya ukweli-tepetepe wanahitimisha kwamba hakuna na haiwezekani pakawapo maadili-gumegume, kwa maana kwamba ukweli kuhusu kipi kinakizunguka kipi kati ya jua na dunia unategemea utamaduni, dini, na mazingira mengine! Wanashauri kwamba mtu akienda Roma sharti aenende kama Warumi!
Hao ndio watetezi wa itikadi ya maadili-tepetepe (mora realitivism). Kwa ujumla basi, nafikiri sasa imeeleweka kwa nini nimesema kwamba watu wanaoyakweza maadili-tepetepe dhidi ya maadili-gumegume wanayo hoja yenye muundo wa hoja niliyoitaja hapo juu. Nairudia hapa chini kwa ajili ya uhakiki sasa:
- Tamaduni tofauti duniani hutumia mizani tofauti ya maadili;
- Maadili maana yake ni kufanya wanachofanya wenzako;
- Hivyo, kutokana na madokezo mawili hapo juu, inafuata kwamba maadili hubadilika badilika kutoka utamaduni mmoja hadi mwingine;
- Aidha, kutokana na madokezo mawili hapo juu, na pia kutokana na hitimisho la hapo juu, kanuni ya jumla ni kwamba: ukienda Roma sharti uenende kama Warumi.
Ukweli ni kwamba hoja hii imepinda! Kitaalamu tungesema kwamba ni fallacy! Nitaeleza kwa kina.
Usahihi wa hoja yenye madokezo na hitimisho kama hii hapo juu unakubalika, ikiwa hitimisho linatokana na madokezo, tena madokezo sahihi. Hii maana yake ni kwamba huwezi ukayakubali madokezo na kisha ukalikataa hitimisho linalotokana na madokezo hayo!
Kwa hiyo, ili kuibomoa hoja kuna mambo mawili: ama unaonyesha kwamba angalau dokezo moja si kweli au unaounyesha kwamba madokezo yote ni kweli lakini hitimisho halitokani na madokezo hayo!
Mimi, kwa kuanzia nimeamua kuibomoa hoja hiyo hapo juu kwa msingi kwamba, japo dokezo la kwanza linakubalika, hitimisho halikubaliani na dokezo hili! Hii ni kweli, kwa kuwa, kutokubaliana juu ya jambo fulani hakumaanishi kuwa hakuna ukweli kuhusu jambo linalobishaniwa!
Ni suala moja kusema kwamba jua linaizunguka dunia na suala tofauti kuthibitisha ukweli wa usemi huo! Na kwa ujumla basi, ni suala moja kuamini kwamba jambo fulani ni kweli na suala jingine kuthibitisha ukweli wa imani hiyo! Mfano wa hapo juu kuhusu historia ya uhusiano uliopo kati ya jua na dunia unathibitisha ukweli huu!
Pili, hoja tajwa hapo juu inaweza kubomolewa kwa msingi kwamba, dokezo la pili si kweli. Maadili maana yake si kufanya kama wanavyofanya wenzako! Maadili maana yake ni kufanya kama anavyotaka Mungu, asiye na dini! Maadili maana yake ni kufanya kama anavyotaka Mungu asiye na utamaduni! Maadili maana yake ni kufanya kama anavyotaka Mungu asiye na kabila! Hayo ndiyo maadili ya kweli!
Na tatu, hoja tajwa, inaweza kubomolewa kwa kuzingatia upotofu unaoambatana na hitimisho lake la pili. Hitimisho hili linasema kwamba ‘ukienda Roma sharti uenende kama Warumi.’
Kauli hii kama ilivyo ni kanuni ya jumla, kwa sababu wao wanaipendekeza kwamba itumiwe na kila mtu, katika mataifa yote na katika milele yote. Kwa maneno mengine, watetezi wa itikadi ya maadili-tepetepe wanakubali ukweli kwamba hapa duniani angalau kuna kanuni moja ya maadili-gumegume!
Lakini lengo la hoja yao ni kukanusha ukweli huu! Kwa hiyo hoja ya kutetea itikadi ya maadili-tepetepe inajifuta yenyewe! Na watetezi wa itikadi ya maadili-tepetepe kwa kukubali kwamba angalau kuna kanuni moja ya maadili-gumegume, wamejipinga wenyewe! Kwa sababu hii pia tunaikataa pia!
Kwa sababu hizi tatu, hoja ya kutetea itikadi ya maadili-tepetepe kama ilivyofafanuliwa hapo juu inabomolewa na kifusi chake kutupwa katika Bahari ya Hindi!
Msimamo wangu ni kwamba: Ni kweli kwamba kuna maadili-tepetepe hapa na pale, lakini hiyo haimaanishi kwamba hakuna maadili-gumegume popote hapa duniani! Tena inawezekana kabisa utamaduni mmojawapo au dini mojawapo ikawa inakubaliana na kanuni za maadili-gumegume!
Na msingi wa maadili gumegume ni matilaba ya binadamu wote! Kila binadamu hupenda mwanga wa upendo, akachukia giza la chuki; kila binadamu hupenda mwanga wa muamana akachukia giza la shaka. Kila binadamu hupenda mwanga wa matumaini akachukia giza la utapia-matumaini; kila binadamu hupenda mwanga wa furaha akachukia giza la huzuni. Kila binadamu hupenda mwanga wa uhai akachukia giza la mauti.
Kila binadamu hupenda mwanga wa maarifa akachukia giza la ujinga; Kila binadamu hupenda mwanga wa shibe akachukia giza la njaa; kila binadamu hupenda mwanga wa amani akachukia giza la vurugu; kila binadamu hupenda mwanga wa uhuru wa kuabudu akachukia giza la shuruti zinazohujumu uhuru wa kuabudu.
Yote haya yanayopendwa yanaitwa matilaba ya binadamu. Na kila binadamu mwenye akili timamu huyafukuzia haya kwa sababu anaona kwamba yatamfaa. Hata kama binadamu anafukuzia kitu kibaya, anafanya hivyo kwa kuamini kwamba ni kizuri. Atagundua vinginevyo baadaye!
Na kwa ujumla basi, tunaweza kuhitimisha kwa usia kwamba, kila binadamu hupenda mwanga wa matilaba ya binadamu (human goods) na akachukia giza la majanga ya binadamu (human evils).
Hii ndiyo kusema kwamba, tukitunga sheria zenye msingi wake katika matilaba ya binadamu, kwa lengo la kulinda masilahi ya vatu wengi, sheria hizo zitapata utii kutoka kwa binadamu wote wenye akili timamu. Atakayekataa kuzitii atakuwa hana akili timamu na ni halali mabavu ya dola kumshughulikia.
Hiyo ndiyo tofauti iliyopo kati ya sheria za maadili (moral laws) na sheria za nchi (civil laws). Sheria za kimaadili hubadilishwa na kuwa sheria za nchi pale ambapo kuna ulazima wa kutumia mabavu ya dola ili kulinda masilahi ya wengi! Kwa maneno mengine, sheria za nchi ni seti ndogo iliyo ndani ya sheria za maadili, ambayo ni seti kuu!
Ni kwa sababu hizo, wahariri, waandishi, wanasiasa na wanaharakati wanaoshauri kwamba mtu akienda Roma sharti aenende kama Warumi, sikubaliani nao! Sikubaliani nao kwa sababu naona kwamba tukiendekeza itikadi ya maadili-tepetepe tutaligeuza taifa hili kuwa kama zizi la kondoo, kama si taifa la madodoki!
Deusdedit Jovin anapatikana kwa S.L.P 2916, Dar es Salaam. Simu 0713425579; na kwa barua pepe deus_jovin@ttcl.co.tz