OPERESHENI mahususi ya serikali ya kuwaondoa wafanyabiashara ndogo ndogo katikati ya mitaa ya Jiji la Dar es Salaam imechukua sura mpya baada ya utekelezaji wake kuanza kuonekana ukivuka mipaka ya awali na kuzusha sura tofauti kabisa na makusudio ya awali.
Matokeo ya uendeshaji wa shughuli hiyo kwa kiwango kikubwa unaonekana waweza kufananishwa na operesheni za namna hiyo hiyo ambazo zimekuwa zikitokea katika mitaa ya miji mikubwa katika nchi za India, Mexico, Pakistan, Uturuki na hata Malawi, ambako nako walifanya mambo kama hayo mwanzoni mwa mwaka huu.
Katika nchi zote hizo, operesheni hizo za kuwaondoa wamachinga pamoja na kuonekana kupata mafanikio, zimekuwa zikiandamana na kuibuka kwa matatizo ya hapa na pale ambayo wakati mwingine yamekuwa yakiigharimu sana serikali.
Katika nchi ya Mexico, mwasisi wa operesheni za kuwaondoa wamachinga wapatao 2,100 mitaani, ajulikanaye kwa jina la Ernesto Uruchurto aliyekuwa meya wa Jiji la Mexico City kati ya mwaka 1952 na 1966 alijikuta akipoteza kazi baada ya kuendesha kazi hiyo kwa ukatili uliovuka mipaka na kuzusha hasira kali katika jamii.
Uchunguzi wa Tanzania Daima Jumapili uliofanywa katika mitaa mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam unaonyesha kwamba, athari zinazotokana na operesheni hiyo ya kuwahamisha wamachinga, sasa imeanza kuwakumba wafanyabishara wengi zaidi ambao awali walikuwa wakijiona kuwa salama salmini.
Kazi ya utekelezaji wa operesheni hiyo katika manispaa za Kinondoni, Ilala na Temeke inaonekana kuwa isiyo na subira na yenye kasi kubwa inayosababisha idadi ya majeruhi wa shughuli hiyo kuwa kubwa zaidi kuliko kawaida.
Waandishi wa gazeti hili waliopita katika mitaa mbalimbali ya manispaa tatu zinazounda jiji hilo, wamebaini kuwapo kwa wafanyabiashara wengi ambao wameingizwa katika mkumbo wa wamachinga, kinyume kabisa na ufahamu wao.
Miongoni mwa wafanyabiashara waliokumbwa katika operesheni hiyo, ni wanaojihusisha na hoteli, baa, migawaha, ofisi za huduma ya vifaa vya ofisi, wapiga chapa, maduka ya bidhaa ndogo ndogo na maduka ya nyama na samaki.
Katika maeneo ya katikati ya Jiji, majengo ya ghorafa yaliyokuwa yakitoa huduma za hoteli, ofisi na maduka yaliyokuwa Mtaa wa Mkwepu, saluni na baa zilizokuwa eneo la Posta Mpya zimeshabomolewa na kuacha watu vinywa wazi. Operesheni hiyo pia ilizikumba ofisi za baadhi ya vigogo zilizokuwa barabara ya Posta Mpya.
Wakati hilo likiendelea, idadi ya vijana walio katika vijiwe na wanaoonekana wakiwa hawana shughuli, inaonekana kuongezeka katika maeneo ya katikati ya Jiji la Dar es Salaam wakiwa katika makundi ya kati ya watu watano na 10.
Katika Mtaa wa Mkwepu, wafanyabiashara waliokuwa wakiuza nguo kwa kutundika ambao walikumbwa na operesheni hiyo, wamejikuta wakilazimika kurudi wakiwa wamebuni mbinu mbadala za kuendesha biashara zao kwa njia za kificho.
Tanzania Daima wiki hii nzima imeshuhudia vijana hao wakiwa na nguo ndani ya mifuko midogo ya plastic na wakifanya biashara yao hiyo katika hali ya uangalifu wa aina ya paka na panya, kinyume kabisa na matarajio aliyoyaeleza Rais Jakaya Kikwete wakati alipozungumza na wahariri wa vyombo vya habari, mwanzoni mwa mwezi huu.
Kikwete katika kauli yake alisema, alikuwa akiamini kwamba, wauza mashati wasingerejea tena mitaani kwani kitendo hicho kingewafanya waonekane kuwa ni watu wenye akili finyu.
Vijana hao walioanza kurejea na ambao jana walionekana kuongezeka kiidadi, wamekuwa wakizitoa nguo zao kutoka katika maficho na kuanza kuzitundika mitaani kuanzia saa 12:00 jioni, wakati watu wengi wanaporejea makwao kutoka maofisini na maeneo mengine ya kazi.
Katika eneo la Kariakoo, mbali na Mtaa wa Kongo uliokuwa umejaa wamachinga kuwa mweupe, mitaa mingine iliyosafishwa kwa tingatinga la Halmashauri ya Manispaa ya Ilala ni maduka yaliyokuwa yamejipanga mstari, kuanzia eneo la Kamata hadi Mtaa wa Uhuru na kuendelea hadi makutano ya Barabara ya Uhuru na Msimbazi.
Katika Mtaa wa Msimbazi, wafanyabiashara waliokuwa wamejenga vibanda pembeni ya majengo ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), wameathirika kwa vibanda vyote kubomolewa na makontena kuondolewa.
Katika maeneo ya Mwenge na Tegeta, vichochoro vinavyotengenisha nyumba na nyumba ambavyo vilikuwa vimezibwa kwa vibanda vya maduka, vimekuwa vikibomolewa usiku bila taarifa, huku vikiwa na bidhaa ndani.
Hadi jana, eneo la Stendi Mpya ya Mwenge, vibanda vyote vya biashara vinavyozunguka eneo hilo vilikuwa vimebomolewa vikiwa na bidhaa nyingi ndani. Wamiliki wa vibanda hivyo walilalamika kuwa hawakupewa taarifa ya kubomolewa vibanda vyao.
Walisema tangazo lililotolewa awali na serikali, lilieleza kwamba operesheni hiyo inawahusu wamachinga wanaouza bidhaa zao nje ya maduka makubwa au wanaotembeza bidhaa zao mkononi. Walisema maeneo waliyokuwa wakifanya biashara walikuwa wamepatiwa leseni na manispaa na kwamba walikuwa wakiyalipia ushuru.
Katika Barabara ya Shekilango, maduka mengi yamebomolewa na kubaki wazi, ikiwa ni pamoja na Ubungo NHC, ambako maeneo mengi yamekuwa wazi, wauza matunda wameondolewa na makontena kadhalika.
Baadhi ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, wameilaani serikali kwa kuwaondoa wafanyabiashara wa majeneza wanaoendesha shughuli zao karibu na eneo la Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na kusema huduma hiyo isingepaswa kuondolewa katika eneo hilo, kwani ni muhimu mno.
Wakizungumza na Tanzania Daima Jumapili kwa nyakati tofauti wiki hii, wananchi hao walisema uondoshwaji wa bidhaa hiyo utasababisha adha kubwa, hasa kwa wananchi wageni wa Dar es Salaam, ambao ndugu zao huhamishiwa hospitalini hapo ili kupatiwa matibabu kisha kufariki.
“Operesheni hiyo ya kuwaondosha wafanyabiashara wa majeneza katika eneo hilo la hospitali haikuwa sahihi. Mfano unatoka mkoani na mgonjwa na kwa bahati mbaya akafariki na wewe ni mgeni hujui hata wapi pa kuanzia ili upate jeneza, utafanyaje?” alisema Jerome Tillya, mkazi wa Majohe.
Alisema kitendo cha kuondoa wafanyabiashara hao wachonga majeneza katika eneo hilo, kitawaumiza wananchi wengi, ingawa hakuna anayeombea kufiwa na ndugu au jamaa yake.
“Jeneza ni kitu muhimu, sasa ikiwa hata hospitali, tena kubwa kama Muhimbili wanaondolewa, je, endapo mtu mwenye mgonjwa ukifiwa utalipata wapi kwa haraka?
“Mimi naona hapakuwa na sababu ya kuwafukuza wafanyabiashara hawa katika eneo hilo. Ili kuondoa adha katika hili, serikali ingewapatia wafanyabisahara hao maeneo ambayo yapo karibu na hospitali ili wafanye bishara hiyo. Majeneza ni kitu muhimu, hivyo sioni sababu ya kuyatoa, cha muhimu watengewe eneo maalumu katika hospitali zetu,” alishauri.
Naye Said Kigumi maarufu kama ‘Kidude’, alilaani kitendo hicho na kuishauri serikali ifafanue ni eneo lipi ambalo wafanyabiashara wa majeneza wanatakiwa kupelekwa.
“Unajua majeneza ni kitu kinachoogopwa na watu wengi, sijui kwa nini sasa wanayachanganya na biashara nyingine. Kwa maoni yangu kitendo cha kuwachanganya wafanyabishara hawa na wengine sijui itakuwaje.
“Ikiwa bidhaa kama hiyo ambayo ni kwa ajili ya binadamu yeyote imeondolewa katika eneo hilo, itabidi kila mtu achonge jeneza na kuliweka ndani ili endapo litatokea lolote kwake au kwa jamaa yake asisumbuke,” alisema Kigumi.
Wakati huo huo, Kigumi aliishauri serikali kufafanua mmachinga ni mfanyabiashara wa aina gani ili kuupa umma uelewa.
“Awali serikali ilitoa notisi ya miezi sita kwa wafanyabiashara wamachinga kwenda katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli hiyo, lakini cha ajabu tunaona hata hawa wachonga majeneza na wafanyabiashara wengine wanafikiwa katika operesheni hiyo,” alishangaa.
Alisema inashangaza kuona Halmashauri ya Jiji ikiwavunjia wananchi waliojenga vibanda vyao vya biashara katika maeneo ya nyumba zao, tena wengine wakiwa na vibali wakati awali zoezi hilo lilionekana kuwagusa wafanyabiashara wa maeneo ya mijini.
“Ina maana na watu wa majumbani pia ni wamachinga, watu hatuelewi kwa kweli, tunaomba serikali ituambie sifa za kuitwa mmachinga,” alisema Kigumi.
Naye Regina Ludovick, mkazi wa Mtoni, alisema uwekwaji wa majeneza katika maeneo ya hospitali kwa ajili ya kuuzwa unasaidia kurahisisha huduma, hasa pale mtu anapopata matatizo ya kufiwa, hivyo ikiwa yatakaa mbali na maeneo hayo, itasababisha matatizo mbalimbali.
Kuanzia Septemba 30, mwaka huu, Jiji liliendesha operesheni ya kuwaondoa wamachinga, baada ya Waziri Mkuu, Edward Lowassa kuwapa muda zaidi wa kukaa, ili wajiandae kuondoka na kwenda katika maeneo rasmi yaliyotengwa kwa shughuli hizo.
Rais Jakaya Kikwete, alisema mwanzoni mwa mwezi huu kwamba, mmachinga atakayerejea barabarani atakuwa na ufinyu wa akili, akasisitiza kwamba lazima waende kwenye maeneo waliyopangiwa, ili hatimaye wajisajili na kuweza kupata mikopo ya kujiendeleza.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimekuwa kikipinga operesheni hiyo, kwa maelezo kwamba serikali haikuwa imeandaa mahali pa kuwapeleka wafanyabiashara hao. Kiliitisha mkutano kuwajadili, lakini polisi ikaupiga marufuku.
Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP), Augustine Mrema, naye amekuwa akiwatetea wafanyabiashara hao. Wapo wanaoona kauli za baadhi ya wanasiasa kuwa ni kama kujaribu kujiongezea mtaji wa kisiasa, wakati Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikiwa kinatekeleza safisha safisha hiyo muda mfupi baada ya kupata ushindi kwenye uchaguzi. Operesheni kama hizo huwa hazifanyiki muda mfupi kabla ya uchaguzi.