Machinga waliohamishiwa soko la Mchikichini wakitokea mitaa ya Kongo na kwingineko Kariakoo wamedai kufurahishwa na namna biashara zao zilivyochanganya mapema katika soko hilo.
Hali hiyo ni tofauti na hofu ya wengi ambao hapo awali waliamini kuwa soko hilo halilipi na biashara zao zitadoda.
Japhet Kaaya, mmoja wa machinga hao amiambia Alasiri kuwa ’ulaji’ unaotokana na kasi nzuri ya biashara zao pale Mchikichini umewapa matumaini mapya ya kufanikiwa zaidi na kujikwamua kiuchumi.
”Awali biashara ilikuwa ngumu katika soko hili... lakini baada ya operesheni iliyowafanya wengi wahamie Mchikichini, mambo sasa yamekuwa mazuri kuliko hata tulivyotarajia. Wateja wanamiminika kwa wingi na hili linatupa matumaini,” amesema Bw. Kaaya.
Naye Bi. Susan amesema kuwa kufuatia biashara zao kuchanganya, hivi sasa kuna dalili ya kuzuka zogo la kuwania nafasi za kuendesha baishara hizo hasa baada ya wengine kujikuta wakikosa nafasi huku baadhi wakimiliki viwanja zaidi ya viwili.
Zoezi la kuwahamisha wamachinga toka katika maeneo yasiyoruhusiwa ni utekelezaji wa agizo la Serikali chini ya usimamizi wa Mkuu wa Mkoa wa Dar Bw. Abbas Kandoro.