Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Salehe Mmoro  »  CCM Kwa Kuwajengea Vibanda vya Udongo Wawekezaji wa Madini, Haina Akili?
CCM Kwa Kuwajengea Vibanda vya Udongo Wawekezaji wa Madini, Haina Akili?
By Salehe Mmoro | Published  10/7/2006 | Salehe Mmoro | Rating:
Na Mwanahabari wa HabariTanzania.com, Dar-es-salaam



SEPTEMBA 22, mwaka 2004, Rais Mstaafu, Benjamin William Mkapa ,alipokuwa akihojiwa na Mtayarishaji wa kipindi maarufu cha Straight Talk Africa (VoA), Dk. Shaka Ssali, aliwatetea wawekezaji wa madini kwamba wamekuwa na manufaa makubwa kwa kuleta tija katika sekta hiyo na kusadia huduma za jamii nchini.

Akijibu swali la Mwandishi wa habari wa Mwanza, Stellah Mathias, aliwatetea: “wamejenga zahanati, wakajenga barabara… Unaweza pia kuchunguza faida za uwekezaji huu kwa mitazamo anuai, ili kuona taifa linanufaikaje kupitia uwekezaji huu. Ajira, kodi na tozo mbalimbali wanazolipa…kama ungeiona barabara toka Kahama kabla ya wawekezaji kuanza, usingetoa hoja hiyo(kwamba madini hayajasaidia)Mnasahau kwamba wanapaswa kulipa mikopo waliyokopa ili kuwekeza katika uchimbaji wa madini.

Naam, hizi ni fedha nyingi… Wanapaswa pia kulipa riba, gawio kwa wabia wao…” Hii ni kauli ya Rais Mstaafu Mkapa,( kwa tafsiri yangu isiyo rasmi) katika mahojiano yale.

Julai 17 mwaka huu wa 2006, (takriban miaka miwili kamili tangu Mkapa atoe kauli hiyo) Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wamesikika wakimlilia Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu J.K.Nyerere! Eti wanasema, angefufuka na kuona hali hii ya madini yetu kuporwa kinyamg’au na wawekezaji,angelia kilio cha uchungu!!

Kulingana na gazeti la Majira la Julai 18 mwaka huu, habari iliyopewa kichwa, “Mwalimu Nyerere akifufuka atalilia madini”, ilisema wabunge hao (waliokuwepo hata wakati wa utawala wa Mkapa) walionyesha kukerwa na namna madini yanavyochimbwa na kampuni za nje, na kushindwa kuboresha maisha ya Watanzania…badala yake yananufaisha wawekezaji!

Kauli hiyo eti ilikuwa ya Mbunge wa Nzega, Lucas Selelii (CCM)aliyesema eti kama Mwalimu angefufuka leo (sina hakika kama atafufuka kwa ajili ya kulilia madini!)angewasuta wanasiasa…

Kwamba Nyerere hakuziita kampuni za madini; akaayaacha madini hayo ardhini hadi Watanzania “wapate akili”ya kusimamia rasilimali hiyo. “Mheshimiwa Spika, nia ya Baba wa Taifa ilikuwa tupate akili kwanza. Lakini kwa kweli hatujapata akili hadi leo!” Selelii alikaririwa akisema.

Mheshimiwa Selelii akamshauri Spika, Samwel Sitta, kuwasilisha bungeni hoja ya kutengua kanuni, ili kuanzia sasa mikataba yote ya madini ipitie kwa wabunge, kupitia kamati iliyoundwa!

Wawekezaji wanachimba na kusafirisha madini yetu kuyauza nje bila usimamizi..mawakala huhakiki mauzo hayo! Wanaouza Wazungu, anayehakiki Mzungu! Hakuna TRA wala nini! Wananunua hata vitunguu Ulaya, wakati vya akina mama wa masoko ya karibu vinawadodea, kwa kukosa wateja!

Selelii, akajitetea kuwa wabunge waliwahi kuhoji dhambi hii, lakini wakaambiwa wabaguzi! Akawabesha msalaba wanasheria na viongozi wa serikali. Pia wamelalamikia mikataba ya IPTL, ATCL na Net Group Solutions, kuwa haiwanufaishi Watanzania.

Wengine waliochangia ni Mbunge wa Busanda,Stephen Kabuzi na wale wa upinzani.

Naam, Mkapa alipokuwa akiwasifia wawekezaji, hawa wabunge walikuwepo na hawakuchachamaa kama ilivyo sasa! Sijui kama alivyosema Selelii, hawakuwa na akili? Pia, kama hata sasa Watanzania hawana akili, kama alivyosema Mheshimiwa huyo Bungeni, Cheche za moto zinapenda kuhoji kuwa, wametumia nini kuwasilisha maumivu haya ya Watanzania Bungeni safari hii, kama siyo akili!?

Wabunge walikuwa wapi kuchachamaa hadi nchi imeuzwa namna hii? Na kama “hawakuwa na akili”, kama alivyodai Mheshimiwa huyo, walikwenda Bungeni kufanya nini! Kulala usingizi, kupiga makofi, kuonyeshana suti za bei mbaya, au kuchukua posho na marupurupu ya uheshimiwa?

Ni walewale…waliokuwepo wakati wa Mwinyi, Mkapa na sasa Kasi Mpya.Kama kilio hiki kingetolewa na akina Zitto Kabwe, Chacha Zakayo Wangwe “Rasta” Hamad Rashid Mohammed , John Cheyo na wenzao, tungewaelewa. Walikuwa wapi wabunge hao wa CCM hadi mikataba hii haramu ikazingirwa na dhambi?CCM.. acheni kulindana katikati ya mafuvu ya maiti za Watanzania! Mmesubiri tufe ndipo muangue kilio? Mlikuwa wapi kuiokoa Tanzania katika gharika, mkasubiri mauti yatukumbe ndipo muanze kulia?

Bila shaka, utawala uliopita(uliokumbatia sera za uporaji madini kupitia kibwagizo cha utandawazi na utandawizi!) ulipokuwa ukijitapa hapo Dodoma, mlikuwa hamuachi kupiga makofi: “Pwaa! Pwaaa!” Ajabu ya Mtume! Leo mwataka wafu wafufuke ili kulilia madini yanayotoroshwa na mafisadi! Acheni kukwepa wajibu! Wafu hawajui lolote…kama hamwezi kujitoa mhanga kwa ajili ya Tanzania, Mungu atahukumu unafiki huu uliotamalaki! Damu zetu, za watoto wetu, wajukuu na vitukuu, zitakuwa juu ya vichwa vyenu…tuliwatuma kusema ukweli bila kuogopa, nyie mkamchekea nyani wakati akila mahindi mabichi!

Leo mwasema, nchi inaporwa! Alichosema Profesa Lipumba, Mbowe, Mtikila na rafiki yetu Mrema, nyie mkabisha ni nini? Cheche za Moto zinaipongeza kwa dhati serikali ya Rais Jakaya Kikwete kusema kweli dhidi ya uchafu huu.Kwamba tulifungua milango ya uporaji wa madini yetu, tukawaimbia nyimbo wezi, tukawachezea ngoma, wakapewa misamaha ya kodi wakati hata watoto, vikongwe na watoto wakitozwa kwa nguvu..wakasomba dhahabu, almasi, tanzanite, ruby, sangara n.k bila kuwahakiki. Tukasubiri tugawiwe kiduchu, wakati rasilimali ni yetu…mwenye chake hugawiwa, siyo?

Wenye mali wameondolewa kwa nguvu katika maeneo yao, wamepigwa risasi utadhani wezi, ndedere, pusi wakomba mboga nk.ili kuwapisha Miungu watu kupora mali asili yetu. Mlisema ndiyo sera ya CCM! Sasa leo mwasema, walifanya dhanbi kiasi cha kuwachukiza wafu makaburini…au mlitumia sera za wapinzani? Tulisikia mkisema wapinzani ni wauaji, wanaagiza makontena ya visu kuleta maangamizi. Hata sera hizi za maangamizi ni zao akina Mbowe na Lipumba, siyo?

Zaidi ya yote, mahali wabunge wanapotamani maiti zifufuke, ili kulilia mali yake (kwa kuwa wali hai wameshindwa kufanya hivyo) kuna demoktasia, amani, usawa, haki, utawala wa sheria au utulivu tu?

Waheshimiwa wabunge, waliponyamazia rekodi mbaya ya umwagaji wa damu migodini,kupitia nguvu za dola,(rejea matukio ya Buhemba, Bulyanhulu, Mererani nk.)walikuwa hawajapata akili; na hata sasa hawana akili? Walikuwa Mangungo wa Msovero, mbele ya akina Carl Peters eeh?

Mwisho, tunatoa mwito kwa wabunge, viongozi, wananchi walalahoi wazalendo wa nchi hii kupata akili tangu sasa ili kukataa kuonewa, kuibiwa na kudhalilishwa ndani ya nchi yetu wenyewe.

Kwa kuwa CCM ndicho chama kilichoko madarakani,kukiri makosa siyo ujinga; ni akili. Shime tusimlilie Nyerere, sisi wenyewe twatosha kusema, La!! Na kubomoa vibanda hivi vya udongo.

omybabu@yahoo.com 


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments
  • Comment #1 (Posted by lugela gaspar)
    Rating
    Kwa kweli hii ndio hali halisi ya uwekezaji hapa tanzania, wazo la bure kwa waheshimiwa wabunge na Rais ni bora kufuta mikataba yote ya madini na kuanza upya.
     
  • Comment #2 (Posted by WILSON)
    Rating
    Swala hili la kukubali kuingia mikataba mibovu kwa kulipwa fedha kidogo(sawa na bei ya shanga)ni kulitia Taifa hasara na vizazi vijavyo.Adhabu inayowafaa viongozi hawa ni kufilisiwa na kifungo cha maisha ili iwe fundisho kwa vizazi vijavyo.

     
  • Comment #3 (Posted by Buberwa)
    Rating
    tufanye na kubuni mambo ya kuendeleza vizazi, nchi na hazina zetu, tuache kuleta siasa nyingi, bila hao tunaoona wanaiba hatutafanikiwa
     
  • Comment #4 (Posted by Mary Justin Shangali)
    Rating
    ukweli ndio huo wala tusidanganyane hapo.viongozi wetu wanatakiwa waamke kwenye usingizi mzito waliolala na wafanye kazi tuliyowatuma na sio kupiga makofi bungeni wakiwa wamesinzia.
     
  • Comment #5 (Posted by mapunda)
    Rating
    wewe hushangai mpaka leo madini ya Tanzanite hayana haki miliki (patent rights)kuwa ni ya tanzania, sasa hata nchi nyingine zinauza madini haya kama yanapatikana kwao!!! ni aibu tupu ndio maana tunakufa masikini.
     
Submit Comment


Article Options
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  3. Is Tanzania a safe place to invest?
  4. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
  5. Nitaendelea kugombea nafasi za kisiasa- Balozi Karume
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Linda Garner
  4. Nthelezi Nesaa
  5. Marshy Abdu
  6. Prosper Kwigize
  7. Salehe Mmoro
  8. Ramadhan Semtawa
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.