Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Salehe Mmoro  »  Heri Kulamba Miguu ya Kikwete Kuliko ya Mabeberu
Heri Kulamba Miguu ya Kikwete Kuliko ya Mabeberu
By Salehe Mmoro | Published  10/7/2006 | Salehe Mmoro | Rating:
Na Mwanahabari wa HabariTanzania.com, Dar-es-salaam

JUMAPILI, Oktoba Mosi mwaka huu, Gazeti la Sunday Nation la Kenya liliwakejeli waandishi wa habari wa Tanzania kwamba walikuwa wakikalia ‘kumlamba miguu’ Rais Jakaya Kikwete, na kukariri kila akisemacho, kama kasuku!

Kejeli hiyo kupitia katuni iliyochapwa ukurasa wa nane wa gazeti hilo, iliwaonyesha Waandishi wa TZ ( Tanzania) waliokuwa wakishangilia, na wengine wakiwa wamemsujudia Kikwete, huku wakimlamba miguu, kuonyesha kuwa waandishi wa nchi hii ni mbumbumbu wasioweza kufanya tafakuri tunduizi dhidi ya kauli za watawala, isipokuwa, kufagilia tu!

Naam, licha ya kumsujudia Kikwete, kumlamba miguu na kushangilia kila alichokuwa akisema, katuni hiyo ya mwaka, iliwaonyesha baadhi yao wakionyesha unyenyekevu kwa rais aliyeketi katika kiti cha enzi, huku akiwa kavalia kanzu, suruali na ‘mabuti’.

Japo ni ujumbe uliotumwa kwa njia ya kejeli kupitia katuni, lakini maudhui ya katuni hiyo yamebeba ukweli uliotiwa chumvi nyingi, dhana iliyowahi kupingwa na hata Yesu wa Nazareti; ya kutoa kibanzi jichoni mwa mwenzako, wakati kwako kuna boriti.

Ukweli mwanana uliomo katika katuni hiyo ni juu ya vyombo vya habari kuacha wajibu wa kuutumikia umma, na kugeuka kasuku; ili kuwasifia watawala.

Tatizo hili halipo Tanzania peke yake, limeota mizizi tangu Kenya, ambako hadi majuzi tu, kila sentensi katika kila Taarifa ya Habari ya Sauti ya Kenya (VOK) na baadaye KBC, ilikuwa ikianza na “Mtukufu!!”Binadamu atakuwaje mtukufu, kama si kulamba dole gumba la watawala? Mtukufu ni Mungu ambaye wengine hudai hayupo.

Mtukufu Rais husika alikuwa akiimbwa kwa takriban asilimia 80 ya muda wa taarifa ya habari, wakati habari zinazohusu maendeleo ya watu, kero zao na hata habari za wanaharakati wa Haki za Binadamu na zile za wapinzani ,zikibezwa!

Sijafahamu; kama habari hizo za kumwita mwanadamu mmoja, “Mtukufu !” kama Mungu, zilikuwa zikikusanywa, zikiandikwa na kuhaririwa na kina nani, kama si waandishi wa habari wa Kenya?

‘Mtukufu, Baba Moi’ alikuwa akiimbwa redioni tangu alfajiri KBC ilipokuwa ikifunguliwa hadi wakati wa kufungwa usiku wa manane.

Haki za wananchi kuzungumza kupitia vyombo huru vya habari, haukuwepo. Badala yake jamii isiyo huru ilikuwa ikichaguliwa wimbo gani waimbe; bila shaka kusifia harakati za serikali ya NYAYO katika kuwaletea watu wake Demokrasia na Maendeleo!

Si Kenya tu. Hata waandishi wa Marekani ambako kunadaiwa Demokrasia imekomaa, na vyombo vya habari viko huru hata kuandika habari za Hugo Chavez kumtukana Bush shetani, vimekuwa vikisambaza pumba na propaganda kwamba Iraq ilikuwa na silaha za maangamizi.

Waandishi wa habari wa Marekani waliokuwa wakiandamana na majeshi ya nchi hiyo Iraq na Afghanistan, hawakuacha kuandika habari za uongo, za upande mmoja, kwamba majeshi ya Washirika yalikuwa yakisonga mbele kwa kasi, huku yakishangiliwa, hata kama walikuwa wakipigwa na maiti za askari wao kuburuzwa mabarabarani na wenyeji.

Hata leo, vyombo vya habari vya Magharibi haviachi kumsifia Bush na Tony Blair na mikakati yao ya kutaka kuzivamia Korea Kaskazini, Iran na Syria, kwa sababu zozote za uongo. Wala hawajakoma kuudanganya umma kwamba Bush anapendwa ulimwengu mzima, wakati Chavez akimtukana Ibilisi, katika mkutano wa mataifa yote, mjini New York! Vipi kuhusu kipigo cha Israeli dhidi ya Hizibollah? Wanasema nani shetani, kati ya Israeli na Lebanon…ni politiki tu.

Kwa kusema hivi, sipendi kutetea uandishi wa upande mmoja; wala sipendi kuunga mkono ‘ukasuku’ wa vyombo vya habari vya ulimwengu mzima, ikiwemo Tanzania.

Ningeridhika, kama gazeti la Nation lingetoa mada kuhusu waandishi wote wa habari wa nchi zetu hizi, ili wafuate maadili ya uandishi na kukosoa watawala wanapokwenda kinyume cha matakwa ya watu.

Ni kichekesho magazeti ya Uingereza kumkosoa Robert Mugabe wa Zimbabwe, kwa kunyang’anya mashamba ya Wazungu na kuwapa Waafrika, wakati waki ‘mfagilia’ Tony Blair kushirikiana na Bush kutesa watu na kuwafunga jela bila kuwafikisha mahakamani huko Guantanamo Bay, Abu-Ghraib na jela za siri Ulaya! Wakati huo huo wakibomoa makazi ya mamilioni ya watu kwa mabomu Iraq, Afghanistan na Lebanon…na sasa wanatishia kwenda Syria, Iran na Korea Kaskazini.

Huku ni kutetea haki za binadamu wapi? Au ndio kama walivyosema wahenga, “nyani haoni nonino?” Tazama CNN, BBC, ABC,CBS,NBC au hata SKY NEWS, n.k. hutakosa kuona habari hasi kuhusu Bara la Afrika na Waafrika…makamasi, mapanki, ukimwi, njaa, vita na kila uchafu!

Hii ni kuonyesha kuwa si lazima sana vyombo vya habari vya kizalendo kupiga kelele nyingi zinazoweza kuivunjia hadhi nchi hiyo miongoni mwa mataifa. Vitakosoa watawala kwa namna ambayo haileti migogoro ya kisiasa inayosababisha “kelele nyingi” hadi masikioni mwa akina Bush, Marekani kiasi cha kutilia shaka ‘Political stability’ katika nchi hizo!

Ulimwengu haujasahau Desemba 30; dakika chache rais Mwai Kibaki wa Kenya akikaribia kuapishwa kuwa rais wa tatu wa Kenya. Katika uwanja wa Uhuru Park, Mtangazaji maarufu wa nchi hiyo (simtaji) ali ‘katwa mtama’ na wananchi waliokuwa wakimshangilia kwa nguvu rais Mpya, wakampokonya chombo cha kutangazia!

Sababu za Mtangazaji huyo wa siku nyingi VOK na KBC kupigwa mtama na wananchi, ni kutangaza habari za kujikomba sana kwa utawala uliopita, na kuwabeza wapinzani, ambao muda mfupi tu waliapishwa kuchukua dola. Hao ni waandishi wa Kenya.
Enzi ya Nyayo wasingethubutu kuwabeza ndugu zao wa Tanzania kuwa wanawafagilia watawala. Vipo vyombo vya habari katika nchi zote vinavyofanya kazi bila upendeleo, wala kujikomba.

Hapa nchini, Kikwete amekosolewa sana; hata sasa Mama Salma anakosolewa kwa kwenda kuhudhuria sherehe za Kimila huko Swaziland, ambako kila mwaka Mfalme Mswati II huchagua kigoli na kuoa.

Wala hatuhitaji kupiga kelele sana hadi akina Bush wasikie huko Washington hadi wafadhili wafikiri tutatoana ngeu!
Kenya, katika Uchaguzi mkuu uliopita, watazamaji wa uchaguzi wakiwemo wa Umoja wa Ulaya (EU) walisema KBC ilikipendelea chama cha Kanu, hususan mgombea wake, Uhuru Kenyatta, kwa asilimia kati ya 32 na 33; wakati wapinzani hususan Narc wakitangazwa kwa asilimia 25 tu katika televisheni ya KBC.

KTN walimtangaza Kibaki kwa asilimia 45, Kanu wakatangazwa kwa asilimia38. Televisheni ya Nation ilimpa Kibaki ‘coverage’ ya asilimia 44, wakati Uhuru Kenyatta na Moi walitangazwa kwa asilimia 34 tu. Je, kuipinga serikali iliyoko madarakani na kuwapendelea wapinzani kwa jinsi hiyo, ndio kulinda maadili ya uandishi? Sio kuwa bias?

Wapi impatiality?
Umoja wa Ulaya walisema,ingawa Tume ya Uchaguzi ya Kenya ilitoa mwaongozo kwa vyombo vya habari, vyombo vya habari vya Kenya, likiwemo gazeti la Nation, walishindwa kuwapa wapiga kura habari sahihi.

Kwa upande mwingine vyombo vya habari vya Kenya, vilikuwepo wakati wa Utawala wa Moi. Lakini vilishindwa kufichua vyumba vya vya siri vya mateso dhidi ya wapinzani wa Kanu, katika jengo la makao Makuu, ya Kanu, Jogoo House, hadi utawala mpya wa Narc ulipoingia madarakani.

Vilishindwa kusema ukweli juu ya watu waliokufa katika mazingira ya kutatanisha enzi za Nyayo. Hawa ni pamoja na Dk. Robert Ouko, na mpiga picha wa Kiingereza, Julie Ward (28) aliyeuawa katika mbuga za wanyama za Masai Mara.
Mauaji ya Julie yaliifanya serikali ya Kenya kuwa lawamani, kufuatia Uingereza kuwatuma Scotland Yard kupeleleza chanzo cha mauaji hayo, kufuatia serikali kusema aliuawa na wanyama wakali!

Kwanini Scotland Yard walikuja kufanya upelelezi wa mauaji ya msichana huyo Kenya, wakati wapo polisi wa nchi hiyo? Rushwa? Kwa nini vyombo vya habari vya nchi hiyo vimeacha nchi kufika huko, kama vyatenda kazi yao barabara?

Vyombo vya habari vya Kenya havikusema muuaji, hadi utawala wa Kibaki ulipoingia madarakani ndipo wakaanza kuandika haja ya kuchunguza vifo vya akina Julie, Dk. Ouko, J.M. Kariuki, Pio Gama Pinto, Tom Mboya na wengine ambao vifo vyao vilikuwa utata mtupu. Je, huu ni Uungwana?!

Na kwanini mahali ambapo vyombo vya habari haviwalambi miguu watawala, kuwe na mauaji ya siri na mawingu ya mashaka , jinsi mfumo mzima unavyofanya kazi… hadi waje Scotland Yard?

Nation waliandika nini kuhusu kifo cha Julie Ward?Waliikosoa serikali kwa asilimia mgapi?

Moi aliiongoza Kenya kwa miaka 24, tangu kifo cha mwasisi wa Taifa hilo, Jomo Kenyatta, 1978.Lakini hadi Kibaki alipoingia madarakani 2002 ndipo ‘siri’ za mauaji ya akina Dk.Ouko ya Feburuari 1990 na siri ya vita vya kikabila vya miaka ya 90 zikaanza kuvuja.

Nation walikuwepo Kenya, walifanya nini badala ya ‘kuulamba miguu’ utawala wa Moi? Kuhusu kashfa za Goldenberg na Anglo Leasing; vyombo vya habari vya Kenya havipaswi kujitazama kuwa viko juu katika kufichua ‘skandali’.Kinachoufikia umma wa Kimataifa, wakiwemo akina George W. Bush, ni fujo na makelele, kana kwamba nchi hiyo haina ‘political stability?’

Mtindo unaotumiwa na waandishi wa habari wa nchi hiyo, na ambao wanataka waandishi wa Tanzania wauige, ni kushambuliana kila kukicha. Vyombo hivyo na waandishi wake hawajapona majeraha ya kikabila, kimajimbo na hata kidini.
Bila shaka waandishi wa kabila fulani huwatetea wanasiasa wa kabila lao hata kama wanaleta mgawanyiko.

Waandishi wa itikadi fulani hudumu kuipinga serikali hata kama haijafanya makosa, mradi tu watu wao washinde uchaguzi. Huu si uhuru wa vyombo vya habari wala kufuata maadili; bali fujo tu zinazo dunda kwa fujo masikioni mwa akina Bush, Washington.

Kuhusu udini, katuni ya Nation imekosa hoja kutaka kuwaambia Watanzania waliokwisha sahahu ukabila na udini, kwamba Kikwete aliyekalia kiti cha enzi ni Muumini wa Madhehebu fulani, ambao hutambulishwa kwa vazi la kanzu!

Kikwete, awe Muislamu, Mkristo, Budha, Baniani, Mpagani au hata asiye na dini yoyote, Watanzania hawajali!
Nijadili kidogo waandishi wa nchi hii kumfagilia Kikwete. Kama udhaifu huu upo hapa Tanzania kama Kenya na Marekani, si wajibu wa waandishi wa Kenya kutufundisha maadili ya kazi. Zaidi sana kila nchi ina maadili yake ambayo hata vyombo vya habari huyafuata.

Kwanza Watanzania hawajazoea fujo; hawajawahi kupigana; wa kabila moja dhidi ya lingine kiasi cha kuathiri nyanja mbalimbali hadi kuanza kushambuliana kwa ukali na kuzua mtafaruku.

Tatizo la vyombo vyetu vya habari kumfagilia Kikwete halina tofauti na vyombo vya Magharibi kutoona uvunjaji wa Haki za Binadamu wa Marekani na washirika wake Iraq na Afghanistan, na badala yake kukalia kumlaani Osama bin Laden, Wataleban, Magaidi, Mullah Muhammad Omar na wengineo wanaopinga ubeberu kwa staili ya kujitoa mhanga.

Pengine, kuipinga serikali iliyoko madarakani na kuwaunga mkono wapinzani bila kujiondoa katika upendeleo wa upande mmoja, si kipimo sahihi cha utendaji kazi au kutimiza wajibu.

Nani asiyejua kuwa kelele za vyombo vya habari vya nchi hiyo juu ya harakati za wanasiasa wa nchi hiyo kupendelea ukabila na migawanyiko ndizo zinazoifanya Kenya kuonekana haijatulia?

Katika nchi ambayo vyombo vya habari hufanya kazi vizuri hakuna rushwa ya kutikisa kama Goldenberg na Anglo Leasing; na wananchi wananeemeka kwa amani inayowaletea uchumi mzuri, potelea mbali utulivu usiwepo.

Ubora wa vyombo vya habari haupimwi kwa picha nzuri za televisheni na magazeti, na mbwembwe za watangazaji wa redio,bali hupimwa kwa amani na ustawi walionao wananchi au jamii inayotumikiwa na vyombo hivyo.

Kipimo cha uandishi bora hakiji kupitia mashambulizi yasiyo na sababu dhidi ya serikali, bali kuutafuta ukweli mkamilifu, bila mashaka, wala shinikizo la wanasiasa wa upande fulani kwa maslahi yao…uandishi bora uliotukuka huwatumikia wananchi wanyonge, makabwela; wala siyo wanasiasa wa upinzani tu.

Bob Woodward na Carl Bernstein au kama walivyokuja kujulikana, “ The Woodstein” ni waandishi wa gazeti la Washington Post, waliofichua kashfa ya Watergate, iliyomfanya Rais Richard Milhouse Nixon kujiuzulu Agosti mwaka 1974.

Waandishi hao wa kitabu maarufu cha All The President’s Men, waliweka bayana matumizi ya fedha haramu kwa maharamia waliovunja makao makuu ya kampeni ya chama cha Democrat, (wapinzani wa Nixon), yaliyoitwa Watergate.

Nixon alikabiliwa na mashitaka ya uhaini kutoka Baraza la Congress, baada ya waandishi hao kulipua skandali la Watergate.Akajiuzulu, na makamu wake wa Rais Gerald Ford, akachukua mahali pake. Ushahidi ulikuwepo, na ungeweza kutolewa mahakamani dhidi yake.

Naam, kuandika habari nzito hakujitengi na ushahidi wa dhati; na wala siyo dhana na kusingizia kusikowanusuru waandishi na mashitaka,kama waandishi wa Kenya wanavyotaka tuanze kumfanyia rais wetu!

Hatuna ugomvi mkubwa na serikali ya Kikwete. Wala Mama Salma hajawahi kuvamia chombo chochote cha habari na kuwapiga bakora waandishi, kubomoa makompyuta na kutupa magazeti.

Kwa kusema hivyo, hatuna maana kuwa tunamlamba miguu au kutowajibika kwa umma, kulingana na wajibu na maadili na uhuru wa vyombo vya habari. Umma wa Tanzania unawajibika kuwa mashahidi, na wala si waandishi wa Kenya.

Tunatambua kuwa serikali na vyombo vya habari ni maadui wa tangu enzi, lakini wenye majukumu tofauti, lakini kila mmoja apaswa kumheshimu mwenzake na majukumu yake.

Kwa misingi hii waandishi wa Tanzania hawaachi kuiheshimu serikali yao hata kama watafichua uoza, rushwa na kutowajibika dhidi yake. Kuheshimu si kulamba miguu. Na kusababisha vita si kufuata maadili yoyote. Ni ushenzi, uchochezi na unyama mkubwa.

Tunakiri; vipo vyombo vya habari au mwandishi mmoja-mmoja waliojibatiza ukasuku. Lakini si wote. Hata Kenya na Marekani wapo kama tulivyoona, wala hatuhitaji nyapara toka Kenya kuwapigia kelele! Sisi wenyewe twatosha.

Nani aliwachagua waandishi wa Kenya kuwa nyapara na walimu wetu? Wanalipwa na nani kwa kazi hiyo? Kwa kujitia mafundi, wanaipa nguvu serikali yao au ugoigoi? Wanapata faida gani kwa kuidhoofisha serikali ya Narc, ili ODM iingie madaearani?

Tunaingia katika Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC) tunahitaji upendo na utulivu kwa nchi zetu na si chokochoko na uchochezi toka upande mmoja. Ule umoja uliokuwepo ulivunjika kwa sababu za ubinafsi toka hukohuko; na sasa dalili zimeanza kuonekana hata kabla ya wakati!

Tunarudia, tunathamini maoni ya kila mtu, yakiwemo ya waandishi wa Kenya, lakini kamwe si kudhalilishwa na mtu kwa sababu tu ya kusigana kwa mawazo na mtindo wa kuendesha mambo yetu.

Biblia inasema, “u-mimi” ni chanzo cha vita, bali tunda la roho ni upendo, utu wema, upole, uvumilivu na tafakuri tunduizi isiyo na vita na kuwapenda maadui hata kuwashangilia kwa mema wanayofanya. Wala hatuhitaji nyapara toka Kenya kwa hili la upendo, umoja, amani na utulivu.`

omybabu@yahoo.com 


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments
  • Comment #1 (Posted by Eng. Magafu, F.F)
    Rating
    Poa sana, hii makala itafsiriwe kwa kiingereza na ichapishwe kwenye magazeti ya East African na mengine yanayouzwa Kenya ili nao wajisomee. NI WASHENZI HAWA wakenya!!
     
  • Comment #2 (Posted by Charles)
    Rating
    Napenda kuanza kwa kuwapongeza wanahabari wetu, mnajitahidi katika hali mliyonayo kutupatia habari zenye ubora na kuelimisha. Labda msifadhaike, kwani wa kulalamika kuwa habari hazina ubora au hazieleimishi ni sisi wananchi wa TZ. Niwakumbushe tena msijisahau mkawa waandishi wanasiasa, muendelee kuwa neutral hivyohivyo. Kwetu sisi upinzania siyo vita/ vurugu. Upinzania maana yake ni kukosonana na kuelezana kipi kingekuwa bora zaidi, upinzani ni sera nzuri zinazotekelezeka na kukidhi mahitaji ya wananchi kulingana na rasilimali tulizonazo. Ni sisi wa TZ tunaoelewa matatizo yetu zaidi, tunatambua rasilimali tulizo nazo. Hivyo tusikubali kupandiwa chuki na yeyoye atokaye kpopote, ndani au nje ya nchi yetu. Tuheshimu kila wazo bora linalojenga, bila kujali anayelitoa ni wachama gain. Kama kiongozi anayetuunganisha wote natutendea tunavyotaka, na wakati mwingine akikosea (maana yeye si malaika), anakosolewa kwa vyombo vyetu hivihivi, kwa kujua uongozi naye anakosoleka na kujijenga vizuri zaidi. Hatutegemei vurugu eti kwa sababu ya idikadi za kisiasa. Wapo wachochezi ila kwa upeo wa kisiasa unavyokuwa wananchi tunajua upinzani ni nini. Na tumeelimishwa zaidi na vyombo vyetu vye habari na si vingine. Tumeshuhudia habari nzuri hata za wapinzani na tunaziheshimu, na bila shaka serikali yetu inaheshimu mawazo na michango ya wapinzani. Endeleeni kuchapa kazi, tupeni elimu, msibabaishwe na mambo kama hayo. Msiangalie wao, angalieni mnachofanya ni sahihi, halafu kama wanabusara watajua makosa yao na muwape nafasi ya kujifunza. Hongereni wanahabari wetu.
     
  • Comment #3 (Posted by Lemburis Kivuyo)
    Rating
    Ningependa pia kuongezea hapo kama ifuatavyo:

    Kulambwa kwa Rais Kikwete miguu ni Kansa iliyopo katika vyombo vya habari Afrika nzima. Hakuna wa kumhukumu mwenzake kwamba ana boriti. Hata hivyo democrasia ina uhai, inazaliwa, inakuwa na kukomaa. Mimi kwa maoni yangu TZ demokrasia inakuwa. Lakini wa kukuza ni wadau wote. Vyombo vya habari, wanaharakati, taasisi zinginbe na mwananchi mmoja mmoja.

    Nirudi kwa Sunday Nation, mimi naona hapa wanajaribu kulipiza kisasi ili kupooza majeraha ya kufukuzwa nchini kwa raia na wafanyakazi wao waliokuwa wakiishi nchini kinyemela. Hawa waariri na waandishi feki wa Sunday Nation sijui kama wanawasaidia wananchi wa Kenya kama wakiendelea kutoa habari kwa chuki binafsi. Nafikiri hawa jamaa wanaturudisha nyuma kwenye hadithi za shule ya msingi "Sizitaki mbichi hizi" baada ya kuona kuwa hawakuweza kukubaliwa kuishi nchini kinyume na taratibu za nchi ndio wakaamua kuandika waliyoyaandika.

    kama nilivyosema mwanzo, demokrasia ina uhai, itahitaji kuzaliwa, na kukua. Sunday Nation wamesema ukweli lakini wameenda mbali mno. Wao wenyewe wanatambaa katika demokrasia na wanawacheka watoto wenzao wanaotambaa vivyo hivyo. kama huo sio unafiki ni nini? Nakuunga mkono kwamba hawa Sunday Nation walitakiwa kwanza watoe boriti lililoko jichoni mwao, yaani wasema udhaifu wa viongozi wao walioshindwa kuongoza nchi kabla ya kuwasema viongozi wa majirani zao.
     
  • Comment #4 (Posted by COSTA RUHETA)
    Rating
    Naungana na ukweli ukiowapa waandashi hao,kwani hata wahenga wakisema kwamba waache wafu wazikane wenyewe.maadali yetu watanzania yanawahusu nini.Hatuwezi kuiga uandishi wao utatufisha pabaya,maana "ukiiga ku...kwa tembo utapasuka msamba".keep it up.aksante.
     
  • Comment #5 (Posted by an unknown user)
    Rating
    Kaka wewe elewa tu kwamba Tanzania inaonewa wivu sana kwa sasa kwa hio dawa ni moja tu kuwa macho na meno ya wenye wivu.
     
  • Comment #6 (Posted by julio_01tz@yahoo.com)
    Rating
    Hatuna haja ya kuwashambulia sana waandishi wa habari wa Kenya, kwani aliyeleta chokochoko yote hii ya katuni ni MTANZANIA MWENZETU anayeganga njaa huko Kenya, Zamani alikuwa hapa Tanzania, huyu ni GODFREY MWAMPEMBA, mnyakyusa wa Kyela au Tukuyu. Huwa anatumia jina la kisanii la "GADO" kwenye magazeti ya Nation na East Africa katika katuni zake!
     
  • Comment #7 (Posted by Kaboka)
    Rating
    Tatizo watanzania huwa hatukubari ukweli,hakuna uwongo kwenye ile katuni,kila siku habari kwenye magazeti ni kikwete kiboko,kiwete anatisha,wakati hakuna la maana linalofanyika .sasa ni wakati wa waandishi kuandika habari siyo utoto kila siku.
     
  • Comment #8 (Posted by adam sururu)
    Rating
    actually i just want to thank you for this column,these hash and rude cartoons are just to bad and embrassing but to our side it gives us strength,keepit up and pour out more stories about kenya,they seem to know much lets learn what is best and leave the rest for themselves.it would be nice if we could also have a column to express our views in various topics you have just written.keep it up just loving you people and we expect more from you.
    adam sururu,
    DAR-ES-SALAAM.
     
  • Comment #9 (Posted by Tom Olewa)
    Rating
    Tafadhali msitutusi sisi wakenya wote eti wapumbavu kwasababu ya Catoon moja ambayo ilichorwa na Mtanzania Mwenzenu. Nilikuwa ninawaheshimu Watanzania lakini baada ya kusoma upumbavu munao andika hapa, nitafikiria mara mbili.
     
  • Comment #10 (Posted by njogu)
    Rating
    I am apalled by these myopic and xenophobic comments. I am a Kenyan who has lived in Dar for 3 years now, and though I knew there were uneasy feelings towards Kenya, I never thought they would be this bitter because honestly this is childish. FYI Gado is a Tanzanian, and in true freedom of press, i believe he draws whatever cartoons he feels like drawing. Also please note that our own leaders in Kenya are not spared this satire. Learn to have a sense of humour guys!!
     
  • Comment #11 (Posted by salema emilius)
    Rating
    Ni sahihi na ni haki kwa watu kutoa maoni yao. Lakini nilisubiri kuona jinsi gani watanzania tuta-react badala ya kuwa pro-active. Tusiangalia tutabaki watu wakuabudu viongozi ambao hawatufanyii chochote. Hatujajua jinsi ya kuwa pima viongozi wetu. Hatujajua ni nani ambaye ni kiongozi mleta maendeleo na populist. Nilazima tuwakosoe viongozi wetu. Si kuwaabudu. Tanzania hatuna upinzani! huu ni ukweli mtupu. Hivyo inabidi tuikosoe serikali sisi wenyewe. Vyombo vya habari ni lazima kuwa wakweli na kuarifu umma wa Watanzania kinachoendelea badala ya kusifia viongozi ambao hatuoni wakifanyacho. Nashukuru tunao waandishi wachache sana wanaoweza kufanya hilo. Mfano ni Hilal Sued wa IPP Media, anaonekana anakiwango kinachostahili kuwa mwanahabari. Vyombo vingi vimejaa wababaishaji. The unqualified journalists. Badala ya kuwatukana wenzetu wakenya tuangalie je kuna ukweli kwenye hilo. Binafsi nakubaliana na wakenya. Tunashindwa kuandika ukweli tunababaisha tu kwasababu tunafikiri mtu fulani ni Mungu mtu ambaye anachokifanya bado hakionekani licha ya balaa la giza linalolikumba taifa. Tunafikiri Tanzania hakuna scandal kama za Goldenberg na Anglo Leasing? Zipo lakini nani amfunge paka kengele?
     
  • Comment #12 (Posted by Patrick Mokuswane)
    Rating
    The article itself is well researched, but the message very imature. It basically suggest that to make a critical ananlysis of someone or a society, one needs to be perfect. This principle augments well in the religious sphere - where imperfect human beings are subjects of a holy God. In the world of social sciences, what the Standard did is allowed. Just imagine if we required all our MPs to be perfect before they uttered a single word to criticise government policies and measures!
     
  • Comment #13 (Posted by Proud Kenyan)
    Rating
    Jameni watanzania, jiepusheni na na chuki na hasira zisizo na msingi!

    It is all in order to be proud of who you are, and of your president (as the writer points out, Kenyans used to sing about Moi all daysome TWENTY years ago)... but take critcism in your stride.

    Salehe, in your xenophobic vitriol, you got your facts wrong. Kanu's headquaters were in KICC, not Jogooo House. The tourture chambers were in Nyayo House and Nyati House...
     
  • Comment #14 (Posted by Mbongo Marekani)
    Rating
    Mtoto akitaka wembe mpe. Sasa wakenya wmechokoza nyuki wapeni ndo ustaarabu wa sasa. Heshima ya mtu mkono wake. Tembeza mkono utaheshimika. Mwanangu hapo mwake... tena itume huko Kenya wakajifunnze na Kiswahili humo humo. Ila sio washenzi make ni wajomba zangu mwanagu. Shikilia uzi....
     
  • Comment #15 (Posted by Alustaadh Addaiy)
    Rating
    Cha kusikitisha ni pale yule tunaemramba miguu anawaramba miguu mabeberu na kuwasaliti ndugu zake.Hayo ndio aliyoyafanya muheshimiwa Kikwete alipokuwa kule marekani.Jama Watanzania wenzangu hasa waandishi wahabari mapenzi yetu yasitufanye tuwe hatuoni aibu zetu.kitendo cha RAIS Bush kumteta Rais Kibaki akiwa na Rais Kikwete ni kutaka kututilia fitina hapa Afrika ya Mashariki,na umasikini wetu usitufanye tukubali hilo.
    Ahsanteni.
     
  • Comment #16 (Posted by Loota L aiser)
    Rating
    Sijui nikuunge mkono vipi mwandishi wa habari hizi. Ni Kazi nzuri sana numefanya kuwashushua hawa madumilakuwili. Kwa ujinga wangu usio makini napenda kumuita mwandishi na mchora katuni huyo wa Kenya kuwa ni mwendawazimu kabisa ambaye hana elimu na ustadi wa uandishi wa habari. Hana maadili yoyote kabisa. Haya ndio tutakutana nayo kwenye shirikisho la Afrika Mashariki. Tuna ustaarabu wetu na hatujazoea ustaarabu wa ukabila, umkoa, wala udini. Hatutaki East Afrika Federation.
     
  • Comment #17 (Posted by mchomes)
    Rating


























































































































































































































































































































































































































































































































































    Mosi, nikupongeze mwandishi kwa makala nzuri,

    Lamsingi hapa sio la mtanzania ua mkenya aliyeleta kikaragosi cha kututukana watanzania, swali ni je,mchoraji anafanya kazi hiyo kwa masilahi ya nani, gazeti gani, nchi gani na anamfanyia nani kazi.Kwani hilo gazeti halina mhariri mkuu na alikubalije hayo yafanyike kwenye gazati lake kama hakuna muafaka?

    Haya yote yanatoa picha kidogo tu ya hali halisi ya majirani zetu walivyo jaa madharau kwa Taifa hili adhimu sana. Hivi watanzania mnaitaji kuona nini ili mjue hawa wakenya sio watu wazuri? mwone mpaka mpasuke macho?Angalia mfano mdogo tu wa maboss wachache kwenye makampuni yanayomilikiwa na wakenya wanavyo nyanyasa wa Tanzania, sio kwenye viwanda, mahoteli, insurance industy kila mahali na makelele ya waTz kwenye maeneo tajwa yamesemwa mpaka kwa mawaziri wetu, lakini wamepiga kimya kama vile hawajui nini kinaendelea.

    Tufike mahali tuseme basi, na tukatae kila aina ya udhalilishaji, unyanyasaji kwa watanzania kwa njia yeyote.wanataka kuleta ukabila hapa, WASHINDWE







     
  • Comment #18 (Posted by Abdallah Issa!!)
    Rating
    Aisee! Sitaki kuandika meengi, ila nawaomba wa TZ wenzangu kuwa makini sana na hawa wakenya, pia tusikurupuke tu kuungana nao kwenye shirikisho la Afrika Mashariki. Sababu hata huyo Museveni anaonesha ana uroho wa madaraka katika shirikisho hilo. Tukiendaga huko kwao wanatunyanyasa saana wakishajua twatoka TZ, sijui wanatuonaje?
     
  • Comment #19 (Posted by DANIEL)
    Rating
    That is very good. tell them!
     
  • Comment #20 (Posted by kasiga)
    Rating
    ukweli ubakie palepale kwani tuachane na tabia zisizo za msingi uweje ugeuke panya wakati wewe ni mamba? kamwe sitaweza kulamba miguu ya kikwete wala ya mabeberu na usishangae wala kuuliza? 9vkta9
     
  • Comment #21 (Posted by proud Nairobian)
    Rating
    We dont care where jogoo, nyati houses KICC are? Kenyans should first sort their mess out before wasting their time commenting about Tanzanianz, are your journalists have anything better to do? Hatutaki chuki na rushwa hapa. kwanza siasa ya kenya is the worst in East Africa, tribalism, nopotism, patriachical society, selfish and prejudiced yet we know 1 million Kibera residents have nothing to survive on amidst Nai, the so called capital of Kenya. Please sort your mess out first, your house is burning!!
     
Submit Comment


Article Options
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  3. Is Tanzania a safe place to invest?
  4. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
  5. Nitaendelea kugombea nafasi za kisiasa- Balozi Karume
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Linda Garner
  4. Nthelezi Nesaa
  5. Marshy Abdu
  6. Prosper Kwigize
  7. Salehe Mmoro
  8. Ramadhan Semtawa
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.