Uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni umetoa agizo kwa wakazi wa mitaa ya Ndugumbi na Vigaeni Jijini Dar es Salaam, kushiriki vyema katika zoezi la kuangamiza wadudu waletao magonjwa ya mlipuko bila kuleta usumbufu kwa wafanyakazi wa Serikali watakaopuliza dawa hizo.
Agizo hilo limetolewa na uongozi huo kupitia Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa huo, Bi. Amina Zuberi Mtemvu.
Amesema kila mkazi anatakiwa kutekeleza agizo hilo bila kipingamizi kwa kushirikiana na wafanyakazi wa Serikali.
”Wafanyakazi halali wa Serikali wenye vitambulisho na sare za kazi watafika kupuliza dawa za kuangamiza wadudu waletao magonjwa ya mlipuko mtaani kwetu, hivyo kutokana na gharama za uendeshaji wa zoezi hilo kila nyumba inatakiwa kuchangia kiasi cha Sh. 1,000 kwa choo cha shimo na mtapewa risiti baada ya kupewa huduma hiyo,” akasema Bi. Mtemvu.
Kadhalika kiongozi huyo amebainisha kuwa utafiti umeonyesha kuwa magonjwa ya matumbo ya kuhara, kichocho, malaria, kipindupindu yanayosababishwa na wadudu waenezao uchafu yamepungua tangu dawa hizo zilipopulizwa miezi iliyopita.
Amesema ukiachia eneo la choo, maeneo mengine yote ya kwenye mifereji, madimbwi na sehemu zote zenye mazalia ya mbu yatapulizwa bure bila kulipiwa kwakuwa ni ya wazi.
Mbali na hilo, Bi. Mtemvu amesisitiza kuwa, wakazi wote wanatakiwa kuhakikisha dawa imepuliziwa katika eneo lao kwani ulinzi wa afya zao hutegemea sana usafi wa eneo wanaloishi