WAZIRI Mkuu, Edward Lowassa, amesema Tanzania itaangalia uwezekano wa kufanya biashara na Lesotho, kutumia fursa ya uelewano mzuri wa kisiasa uliopo baina ya nchi hizo.
Lowassa ambaye amekuwapo Lesotho kumwakilisha Rais Jakaya Kikwete kwenye maadhimisho ya miaka 40 ya uhuru wa nchi hii, alikuwa akitoa maelezo kuhusu uhusiano wa Tanzania na Lesotho kwa Balozi wa Tanzania nchini hapa, Emmanuel Mwambulukutu.
Balozi Mwambulukutu ambaye ofisi yake iko Afrika Kusini, alimweleza Waziri Mkuu Lowassa kuwa kuna nafasi ya kufanya biashara na nchi hiyo kwa vile kuna vitu Tanzania inatengeneza kwa wingi na Lesotho soko lipo kwa kuwa inavihitaji.
“Kuna vitu vidogo vidogo vya matumizi ya nyumbani kama ndoo, vifaa vya plastiki ambavyo vinahitajika sana na wananchi wa kawaida wa Lesotho. Sasa hivi kuna Watanzania wanaingiza vitu hivyo lakini kwa uchache tu na si biashara kamili,” alisema.
Waziri Mkuu Lowassa alijibu kuwa serikali itaangalia uwezekano wa kufanya biashara na Lesotho kwa vile Watanzania sasa wanaanza kuchacharika kufanya biashara na nchi mbalimbali duniani kutokana na fursa zilizopo.
Juzi Waziri Mkuu Lowassa, akiwa miongoni mwa viongozi waalikwa kutoka nchi mbalimbali za Afrika, alishiriki kuangalia gwaride rasmi la kitaifa kwenye uwanja wa michezo wa Setsoto mjini hapa.
Mfalme Letsie III (wa tatu) wa Lesotho alikagua gwaride hilo lililofanywa na jeshi la nchi hii na kupokea saluti kabla ya kulihutubia taifa kwa kuwashukuru wananchi wa Lesotho kwa utulivu wao hivi sasa na kuwataka waendelee kuijenga nchi yao. Wananchi pia waliandamana kupita mbele ya mfalme wakati wa gwaride hilo.
Naye kiongozi wa Serikali ya Lesotho, Waziri Mkuu, Pakalitha Mosilili, aliwashukuru viongozi mbalimbali wa nchi za Afrika na wawakilishi wa nchi mbalimbali duniani kwa kushirikiana na wananchi wa Lesotho katika maadhimisho hayo