MAMA wa Mfalme Mswati III wa Swaziland, Ntobi Indlovukazi, aliyepo nchini kwa ziara ya siku tano amesema, sherehe za kimila za nchi hiyo zinazowahusisha mabinti mabikira, zinalenga kuwafundisha wasichana hao maadili mema na si vinginevyo.
Akizungumza Ikulu jijini Dar es Salaam katika hafla ya chakula cha usiku iliyoandaliwa kwa heshima yake na Mama Salma juzi, Ntobi alisema sherehe hizo za kila mwaka za kimila (Read Dance) ambazo mwaka huu zilihudhuriwa na mke huyo wa Kikwete hulenga kuwafundisha vijana wa kike namna ya kujitunza.
Alibainisha kuwa katika kipindi cha sherehe hizo, vijana hao wa kike wa rika mbalimbali hufundishwa mambo muhimu yanayohusu kulinda na kutunza ujana wao, majukumu ya mwanamke katika familia, ukakamavu, nidhamu na kubwa zaidi ni katika kujiepusha na janga la Upungufu wa Kinga Mwilini (UKIMWI).
“Tunawafundisha vijana wetu wa kike namna ya kujitunza ili kuepusha maambukizi ya UKIMWI. Namshukuru sana Mama Kikwete kuitikia mwaliko wangu ambao licha ya kuutoa katika muda mfupi, aliweza kufika na kuhudhuria tukio hilo muhimu katika nchi yetu, naamini kuna mengi aliyojifunza,” akasema mama wa Mfalme Mswati.
Kauli hiyo ya mama wa Mfalme Mswati imekuja wakati kukiwa na shinikizo kubwa la wanaharakati wa haki za binadamu na watetezi wa masuala ya kijinsia kupinga kitendo cha Mama Salma kuhudhuria sherehe za mwaka huu, ambazo kiongozi huyo alioa mke mwingine.
Hata hivyo, taarifa ya Ikulu iliyomkariri mama huyo wa mfalme haikueleza iwapo alizungumza lolote kuhusu hulka ya mwanawe, Mfalme Mswati III kuchagua mke karibu katika kila sherehe, jambo ambalo limekuwa likipigiwa sana kelele na wanaharakati wa masuala ya kijinsia duniani.
Tangu wanaharakati hao wamshambulie Mama Salma, hakuna kiongozi yeyote wa kiserikali ambaye ameibuka na kutoa majibu kuhusu ziara hiyo ya mke wa Rais Swaziland, ingawa makala ziliandikwa na baadhi ya vyombo vya habari zikihoji uhalali wa hoja za wanaharati kuhoji utamaduni wa taifa jingine.
Mbali ya suala hilo, Ntobi alisema katika nchi yake kuna juhudi za wanawake katika kuwaendeleza wanawake wenzao kiuchumi, na kwamba wanawake wa Swaziland wana mengi ya kujifunza kutoka kwa wanawake wa Tanzania.
Alisema kuwa, ziara yake nchini itampa fursa ya kubadilishana mawazo, mbinu na mikakati ambayo wanawake wa Tanzania wanatumia katika kuwainua wenzao kiuchumi, lakini zaidi katika kukabiliana na tatizo la ugonjwa wa UKIMWI.
“Sisi wanawake wa Swaziland, Tanzania na Afrika tukikuna vichwa vyetu na kwa pamoja tukikusanya nguvu zetu, tunaweza kabisa kuwakwamua kiuchumi wanawake wenzetu, hasa wa vijijini na kuokoa maisha ya vijana wetu wengi wasiangamie na UKIMWI,” alisema Ntobi.
Aliongeza kwamba, pamoja na mafanikio makubwa ya kiuchumi yaliyopatikana katika nchi hizi mbili, bado wananchi wa nchi hizo wanakabiliwa na matatizo ya umaskini, maradhi, UKIMWI, ukame na ukosefu wa ajira.
Alisema kuwa, Swaziland na Tanzania zinatakiwa kuunganisha nguvu zao katika kuhamasisha kinga dhidi ya UKIMWI, kufanya utafiti wa tiba ya ugonjwa huo na kuweka mipango madhubuti ya kuwasaidia watoto yatima.
Mama Salma kwa upande wake, alisema zinatakiwa nguvu za ziada katika kuwapatia wajawazito wenye virusi vya UKIMWI dawa zitakazowawezesha watoto wao kuzaliwa bila kuambukizwa.
Alimtaka mama wa Mfalme awe balozi mzuri wa kutangaza vivutio vizuri vya utalii vilivyopo hapa Tanzania na pia awashawishi wafanyabiashara wenye uwezo wa kifedha kuja kuwekeza nchini Tanzania.
Baadhi ya wageni walioalikwa kwa chakula hicho ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dk. Asha – Rose Migiro; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Hawa Ghasia; Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Anna Abdallah na wabunge.