Kauli kwamba sangara wa Ziwa Victoria huuzwa Ulaya na kuacha mifupa, kwa kuwa siyo chaguo la kwanza la wakazi wa eneo hilo, ni uongo mtupu, upuuzi na unafiki uliopea.
Kama ni hivyo, kwa nini sasa wale vichwa vinavyoitwa mapanki? Wengine wanasema eti mapanki yanatengeneza supu; kwamba supu ya mapanki ni tamu kuliko ya sangara mwenyewe! Unafiki na uzandiki!
Ninakubaliana na ukweli kwamba sangara alipoanza kuonekana ziwa Victoria mwishoni mwa miaka ya 70, hakuwa na walaji wengi. Kulikuwa na samaki wengine kama sato, furu, gogogo, ningu, kuyu n.k.
Lakini kadiri miaka ilivyokwenda, sangara huyu aliyegeuka “Nightmare” leo, akawameza samaki wadogo wote, na kusalia yeye. Wananchi wakakosa chaguo lingine. Wakamtegemea yeye sangara kuwa chakula chao.
Ingawa wengi walianza kushindwa bei yake baada ya kuanza kusafirishwa Ulaya, waliendelea kula watoto wake waitwao,Serena, bodo, degere au hata Ng’arata ama Jing’arata, kwa Kijita.
Hawa Ng’arata au degere ndiyo chakula kikuu leo katika mwambao wa Ziwa Victoria. Tena hawa wanategemewa au wanapendwa na siyo watu fukara tu, bali hata wenye uwezo wa kati. Wanaliwa badala ya furu ambao hawapatinani kwa wingi kama zamani, kwa sababu waliliwa na huyohuyo,Nightmare, sangara!
Mahali hawa degere wanapopatikana, ama hukaushwa na kusafirishwa ndani ya magunia, au huuzwa na kuliwa wabichi, na ni watamu kuliko Perege wa Bwawa la Nyumba ya Mungu.
Bei ya fungu moja dogo ni kati ya sh. 500 hadi 1500 kutegemea umbali toka ziwani. Baadhi ya wananchi waliokuwa wakiwakataa walijikuta wakilazimika kuwala, kufuatia uhaba wa samaki wengine au hata nyama, na mboga za majani, ambazo huwa adimu nyakati za kiangazi.
Hata hao sangara wadogo hukaushwa kwa njia duni sana. Yaani hutupwa mchangani na kuoza, kisha wanapokauka kuchukuliwa na kuuzwa! Kwa wale wanaowajua hawa degere wakavu, hutoa riha mbaya mithili ya kidonda kilichovunda, lakini wakipikwa huwa watamu mithili ya sato wakavu!
Akitokea Sauper, akapiga picha jinsi wanavyokaushwa hawa degere kwa jua, watu watasema katudhalilisha! Vivyo hivyo, hata mapanki yanapotolewa viwandani hutoa riha mbaya. Riha mbaya huja baada ya mapanki hayo kuoza na kutoa mafunza na si vinginevyo!
Kama yalivyo madegere, mapanki nayo yakishakaushwa kwa moto ili kuua mabuu na mafunza, huonekana mazuri. Mengine hukaangwa na kuuzwa sokoni; kiasi kwamba mtu aliyeyaona yakitolewa kiwandani, hatajua kuwa ndio yale yaliyokuwa yakitoa uvundo!
Hapa hoja dhaifu inayotolewa na serikali kwamba sangara si chaguo la wenyeji wa Kanda ya Ziwa, kwa kweli ni upuuzi na kuwafanya watu kuwa wajinga! Kama si chaguo lao, wanakula madegere ya nini; na mapanki ya kazi gani?
Tuambizane ukweli kwamba, huyu Nightmare (Jinamizi) sangara, ndiye aliyeleta matatizo ziwa Victoria. Aliwala sato wote wazuri;akawafyeka gogogo, ningu labda na mumi au kamabale, na kusababisha watu kumtegemea yeye.
Baada ya kuanza kuuzwa Ulaya, sangara wote wakubwa waliadimika sokoni.Wakabaki watoto wao wanaovuliwa siku mbili tu baada ya kuanguliwa! Pia Mamlaka ikapiga marufuku uvuvi huu haramu! Sasa wananchi wale nini kama si mapanki?
Si sangara wadogo pekee wanaopigwa marufuku kuvuliwa, kufuatia kinachoitwa uvuvi endelevu. Hata dagaa wamewekewa masharti kwamba wavuliwe wanene!
Nyavu za kuvulia dagaa leo ni mgogoro unaofukuta. Maofisa wa Uvuvi, polisi na Maliasili, wanawageuza wavuvi kuwa “Hela ya mboga” kila kunapokucha, kufuatia jinamizi hilo la uvuvi haramu! Ajabu ni kwamba nyavu zenye matundu madogo, hazikamatwi huko viwandani na madukani…wahusika husubiri zifike ziwani, ambako huzipora na kwenda kuziuza kwa njia haramu eneo lingine, na chache huchomwa moto, ili kuhalalisha unyama wao!
Ninasema, ulaji wa mapanki huchochewa na vitu vimgi ikiwemo rushwa, tamaa, kukurupuka, mipango mibovu na kwa ujumla njaa tu! Utawazuiaje wavuvi kuvua dagaa, sangara wadogo n.k bila kuwawezesha nyenzo za uvuvi endelevu?
Wale nini; mawe siyo? Halafu wakila mapanki mbele ya kamera za kina Hubert Sauper, mnakataa kuwa ni uongo! Acheni unafiki!
Kwa upande mwingine, hakuna mwananchi wa kijijini anayeweza kununua mnofu wa sangara, hata kama watauzwa katika maduka! Kwani nyama haziozei buchani, kwa kukosa wanunuzi?
Hoja hapa ni kuwawezesha wananchi kiuchumi; ili waweze kuepuka kula chakula cha ovyoovyo, kinachodhalilisha, basi! Kama alivyosema rais Kikwete juzi, Watanzania ni watu wanaojipenda…wanakula mapanki kwa shida. Shime rasilimali zetu zinazovunwa na Wazungu ziwawezeshe kuinuka kiuchumi.
Kuna uongo wa kinafiki, kwamba mapato ya sangara yamewanufaisha sana wananchi wa Kanda ya Ziwa tangu waliopoanza kuuzwa Ulaya! Wamenufaika vipi wakati wanakula uvundo? Si kweli kwamba sasa biashara hiyo imeondoka mikononi mwa watu wa kawaida, badala yake wanaonufaika ni wageni: Wahindi, Wazungu, Wakenya na watu wengine?
Siyo haohao wanaotuzuia kuvua, na badala yake wanavua wao wenyewe na kutuacha kula degere, ng’arata na mapanki bila uwezo wa kununua nyama au samaki wengine? Mkulima wa Misungwi au hata Bugoji na Nyambono, anao uwezo wa kununua fillet ya sangara? Kama jibu ni hapana; ale nini kama siyo panki? Kumbuka degere nao hutokana na uvuvi haramu!
Mkoani Mara wakazi wengi wa vijijini walizoea kula wanyamapori, hususan nykati za kiangazi ambazo husababisha mboga-mboga na samaki wengine kuwa adimu.Leo ukionekana na nyama ya pundamilia (nyara za serikali) ni kifungo cha miaka 30 jela; wale nini kama siyo panki? Wale senene, kumbikumbi na wadudu wengine? Nao hupatikana nyakati za masika tu…
Kabla ya kukanusha kuwa wananchi waliowemgi hawali mapanki, tunaomba utafiti wa kisayansi. Tena wengine husema mapanki yanayoliwa hayajaoza! Sangara anapotolewa kwenye barafu, baada ya kuondolewa minofu kiwandani, huoza baada ya saa ngapi, kama si chache tu?
Kwa kifupi, Darwin’s Nighmare inatuzindua Watanzania usingizini. Tuache kulala. Tutumie vizuri rasilimali zetu kuondoa wananchi katika ufukara. Hapa hoja si kuzuia sangara kuuzwa Ulaya kwa pesa nyingi. Ni kutumia mauzo ya sangara kuboresha maisha ya wote.
Ahadi ya rais wetu ni maisha bora kwa kila Mtanzania; si kwa welio wengi; ili wanaobaki wale mapanki, halafu tukatae ukweli kwamba hatuli panki! Tena ni aibu kusema kuwa wavuvi wamefaidika, wakati sasa hawana kitu, nyumba walizojenga kabla ya matapeli kuja, tayari zimeuzwa!
Wengine wamewatapeli wavuvi na kuuza viwanda! Tena bei wanayowalipa wavuvi ni ya kitapeli, wakati wao wanivuna Euro. Haya yote Sauper hajayasema? Viwandani; wageni wanalipwa mishahara mizuri kuliko wazawa. Ni hadithi tu kwamba tumepata mabilioni…mrahaba uliopatikana ni shilingi ngapi, na zimefanya nini?
Tuwe wakweli. Badala ya kuandamana kumpinga Sauper, tukae chini kuondoa tongotongo tulizoona katika Darwin’s Nighmare. Wananchi wengi wanajua haya, wala si mabango yaliyochorwa juzi kulaani baadhi ya vyombo vya habari na wahusika wengine.