Habari Tanzania - http://www.habaritanzania.com
Majambazi yateka machimbo
http://www.habaritanzania.com/articles/12/1/Majambazi-yateka-machimbo
By Habari Tanzania
Published on 05/14/2006
 
Watu wanane wanaosadikiwa kuwa majambazi yakiwa na silaha yameyateka kwa muda wa saa saba, machimbo ya dhahabu ya Nyakahula, wilayani Biharamulo mkoani Kagera.

Watu wanane wanaosadikiwa kuwa majambazi yakiwa na silaha yameyateka kwa muda wa saa saba, machimbo ya dhahabu ya Nyakahula, wilayani Biharamulo mkoani Kagera.

Katika purukshani hizo, yalifanikiwa kupora maelfu ya fedha baada ya kuwapiga wachimbaji na kuwabaka wanawake hadharani na kutokomea bila upinzani wo wote.

Afisa tarafa ya Lusahunga, Bw. Julius Kigongo, alithibitisha kuwepo kwa tukio hilo lililofanyika Jumatatu usiku na kueleza hiyo ni mara ya nne kuvamia na majambazi, katika kipindi kisichozidi miezi minne. Hata hivyo alisema machimbo hayo si rasmi na yanaendeshwa na wachimbaji wadogo.

Bw. Kigongo, alisema kwa mujibu wa taarifa rasmi zilizopo ofisini kwake, watu wanane wanaodaiwa kuwa na bunduki aina ya SMG walivamia machimbo hayo na kisha kuwaweka chini ya ulinzi mamia ya wananchi kwa zaidi ya saa saba, huku yakifyatua risasi juu ili kuwafanya wasalimu amri.

Tukio hilo limetokea kati ya saa 4 usiku na saa 11 alfajiri, walipoondoka baada ya kufanya ukatili wa aina yake, ambapo baadhi ya wanawake wanaoendesha biashara za kuuza vinywaji baridi, bia na mama lishe, walibakwa hadharani kwenye sebule za vibanda vyao mbele ya wateja.

Uporaji huo umetokea siku nane tu baada ya majambazi wengine wenye silaha kuvamia machimbo hayo Mei Mosi na kupora fedha na kuwabaka baadhi ya wanawake. Machimbo hayo yamevamiwa mara nne katika katika kipindi kisichozidi miezi minne.

Afisa Tarafa huyo, alisema taarifa ya tukio hilo iitolewa polisi ambapo walifika eneo la tukio na bado wanaendelea na upelelezi.

?Wakizungumza na mwandishi wa habari wa PST juzi alipotembelea eneo hilo, baadhi ya waathirika akiwemo mwanamke aliyejitambulisha kwa jina la mama Said huku akijikongoja kwa kutumia fimbo kutokana na majeraha aliyoyapata kutokana na kipigo amedai alinyang’anywa Sh. 136,000 za mauzo ya bia.

Ingawa yeye alisema hakubakwa, lakini aliwasikitikia waliobakwa na majambazi hayo kwa zamu huku yakipiga kelele yakidai kila mambo sasa yanakwenda kwa ari mpya, kasi mpya na nguvu mpya yakisisitiza hayatapenda kuua iwapo watafuata maelekezo yao.

Kijana mmoja anayedai kuporwa Sh. 8,000 alizopata kwa kusafirisha abiria kwa kutumia baiskeli, aliyeomba kuficha jina lake, amedai baada ya kusalimisha fedha alizokuwa nazo kwa majambazi hayo, kama alivyokuwa ameamriwa, alishuhudia jirani yake mwanamke aliyemhifadhi jina lake akibakwa kwa zamu.

Kufuatia kuwepo mlolongo wa matukio katika machimbo hayo, imeelezwa kuwa uhalifu unachangiwa na wakimbizi wakishirikiana na baadhi ya wananchi wasio waadilifu.

?Juhudi za kuwapata Kamanda wa polisi wa mkoa wa Kagera na mkuu wa wilaya ya Biharamulo, kuzungumzia matukio hayo hazikufanikiwa baada ya simu ya mkononi ya RPC Ignas Mbinga kutopatikana wakati wasaidizi katika ofisi ya mkuu wa wilaya walidai alikuwepo kwenye ziara maalumu ya kuhamasisha usalimishaji silaha.

  • SOURCE: Nipashe