WAZIRI wa Ulinzi wa Marekani, Donald Rumsfeld, ameridhia ofa ya kununua tumbaku ya Venezuela lakini ameikoromea serikali ya Rais Hugo Chavez kwa kujijenga kijeshi.
“Katika sayari hii sijasikia mtu yeyote anayeitishia Venezuela, hivyo sioni sababu ya kujijenga namna hiyo kijeshi,” alisema Rumsfeld, ambaye anahudhuria mkutano wa mawaziri wa ulinzi wa nchi zilizo katika kizio cha magharibi, ambao wengi wao walisikitishwa na silaha, ndege za kivita na helikopta anazonunua Chavez.
Nchi nyingine za eneo hilo zimeonyesha wasiwasi kwamba silaha hizo zinaweza kuishia katika mikono ya magaidi, Rumsfeld aliwaambia waandishi wa habari juzi na kuongeza kwamba anaelewa sababu za nchi jirani kuwa na wasiwasi.
Wakati akihoji suala la kujijenga kijeshi, Rumsfeld pia alisalimiana na waziri wa ulinzi wa Venezuela, Jenerali Raul Isaias Baduel, ambaye pia anahudhuria mkutano huo.
“Nimezungumza na Rumsfeld kumhakikishia ubora wa tumbaku ya Venezuela, na nilimtaka ajaribu kuivuta,” Baduel aliliambia Shirika la Habari la Associated Press.
Hata hivyo alisema kwamba Rumsfeld alimweleza kuwa havuti tumbaku na mke wake hangekuwa tayari kumuona akivuta.
Baduel, alisema kwamba hakukutana na Rumsfeld wakiwa peke yao, pia alisema kwamba operesheni ya hivi karibuni ya nchi yake kujijenga kijeshi si mashindano ya silaha kama Marekani inavyodai.
Rumsfeld pia hakukutana na Chavez, ambaye amekuwa akisisitiza kwamba Marekani inapanga kuivamia nchi yake, madai ambayo maofisa wa Marekani wameyatupilia mbali.
Chavez alitawala vichwa vya habari hivi karibuni baada ya kumwita Rais George Bush ‘shetani’ na kuwakoromea viongozi wa Marerkani kujaribu kukwamisha juhudi za nchi yake kuingia katika Baraza la Usalama la UN.
Rumsfeld yuko katika ziara ndefu ya masuala ya kijeshi katika nchi mbalimbali, ziara ambazo zimemweka mbali na kelele za vyombo vya habari huku mjadala unaomtaka ajiuzulu kutokana na vita ya Iraq ukiibuka upya.
Rumsfeld ameshaweka wazi kwamba hatajiuzulu na wala hatasoma kitabu kilichotolewa hivi karibuni kinachokosoa utendaji wake ‘State of Denial’ kilichoandikwa na Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Washington Post, Bob Woodward.
AP