Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Wapinzani wamshangaa Kikwete kwa kutaka kuzirejesha nyumba
Wapinzani wamshangaa Kikwete kwa kutaka kuzirejesha nyumba
By Habari Tanzania | Published  10/4/2006 | Habari za Kitaifa | Rating:
na Martin Malera

VIONGOZI wa vyama vya siasa vya upinzani, wamesema serikali inapaswa kujilaumu yenyewe kwa uamuzi wake wa kuuza nyumba zake, na sasa kujaribu kuzirejesha.

Walikuwa wakizungumzia hatua ya Rais Jakaya Kikwete ya kuamua kurejesha baadhi ya nyumba za serikali ilizoziuza, kwa maelezo kwamba zipo kwenye maeneo nyeti.

Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP), Augustine Mrema, alisema jana kuwa, anachofanya Rais Kikwete ni kukumbuka shuka wakati tayari kumekucha, mwenyewe akidhani bado anao usiku wa kulala.

Alisema wapinzani walipinga tangu mwanzo suala la kuuza nyumba hizo, lakini Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), iliziba masikio. Enzi hizo ilikuwa utawala wa awamu ya tatu.

“Sisi tulizungumza, tukaonekana wajinga, lakini leo rais anakumbuka kujifunika shuka wakati kumekucha. Suala hilo litamletea mgogoro mkubwa na vigogo wenzake, haiwezekani,” alisema Mrema.

Mwenyekiti huyo alisisitiza kuwa ni vigumu kwa Rais Kikwete kurejesha nyumba hizo, kwani serikali iliuza yenyewe kwa hiari yake, sheria zipo na mahakama zipo, na kwa kuwa sheria zilizotumika kuuza hazijafutwa, wengi watakimbilia mahakamani kudai haki.

“Waliouziwa mikataba wanayo, hawakupora nyumba hizo na sheria zipo hazijafutwa. Tuliwaambia, mkatuona sisi tuna wivu,” alisema Mrema.

Akizungumza na Tanzania Daima kwa simu jana, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Wilbroad Slaa alimshauri Rais Kikwete aunde tume kuchunguza suala zima la uuzaji wa nyumba hizo, akisema limegubikwa na rushwa.

Alisema umuhimu wa kuunda tume pia utasaidia kujua thamani halisi ya nyumba hizo tangu ziliponunuliwa na hata baada ya kufanyiwa ukarabati, kwani kuna baadhi ya nyumba zimenunuliwa kwa sh milioni 40 na kukarabatiwa kwa sh milioni 100.

“Kwanza nampongeza Rais Kikwete kwa kutambua kuwa kuna matatizo katika suala la uuzaji wa nyumba hizo, matatizo ambayo tungeweza kuyaepuka kama tungekuwa wasikivu,” alisema Dk. Slaa.

Alimtaka Rais Kikwete kuangalia pia nyumba zilizouzwa kwenye halmashauri za wilaya, badala ya kuangalia nyumba zilizopo Serikali Kuu.

Kuhusu suala la Zanzibar, Dk. Slaa alimtaka Rais Kikwete kuacha maneno, kwani mara kadhaa amezungumzia kushughulikia tatizo la Zanzibar, lakini hajaanza kufanya hivyo.

Hata hivyo, alipendekeza kuwa, suluhisho la mgogoro wa kisiasa Zanzibar ni kuanzisha serikali ya mseto. Alisema serikali iache dhana ya kuwa na muafaka wa tatu, wa nne na zaidi, na sasa iangalie muafaka wa kudumu.

Pia alisema mgogoro wa Zanzibar sasa usichukuliwe kama suala la Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF), bali liwe suala la Watanzania wote.

Juzi, Rais Kikwete, katika mkutano wake wa kwanza na wahariri wakuu wa vyombo vya habari nchini, alizungumzia kwa mara ya kwanza hadharani suala la kurejesha baadhi ya nyumba alizosema zipo kwenye maeneo nyeti.

Pia alisema ameshaanza kushughulikia suala la mgogoro wa kisiasa Zanzibar kama alivyoahidi wakati akihutubia Bunge kwa mara ya kwanza mwishoni mwa mwaka jana, mjini Dodoma, akisema kwamba amefikia pazuri.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments
  • Comment #1 (Posted by Juma M Juma)
    Rating
    Kikwete is a charlatan. Hana jipya zaidi ya kutaka sifa.Mbona yeye alikuwepo wakati zinauzwa na alinunua?
    Huu ni unafiki wa watawala wetu.Hata hivyo hana makosa. Huo ndiyo uzuri wake wa sura uliomuwezesha kuchaguliwa katika rushwa kubwa na inayonuka. Anatudanganya harejeshi nyumba hata moja ng'o
     
Submit Comment


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.