Na Mwandishi Wetu
MAMA wa Mfalme wa Swaziland, amewasili nchini jana kwa ziara ya siku tano, akiwa ni mgeni wa serikali.
Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa, Mama wa Mfalme alipokelewa na mke wa Rais, Mama Salma Kikwete. Akiwa uwanjani hapo, alikagua vikundi mbalimbali vya utamaduni vilivyoandaliwa kwa heshima yake.
Mama wa Mfalme kesho atakwenda Kisiwani Zanzibar ambako atapokelewa na mke wa Rais wa Zanzibar, Mama Shadya Karume na kutembelea maeneo mbalimbali ya visiwa hivyo, yakiwamo maeneo ya kihistoria.
Jumatano, Mama wa Mfalme ataondoka Zanzibar kwenda Mkoani Manyara ambako atatembelea kreta ya Ngorongoro.Mgeni huyo amewasili nchini huku vumbi la lawama za wanaharakati wa haki za binadamu na masuala ya jinsia kuhusiana na Mama Kikwete kuhudhuria sherehe za kimila nchini Swazland, likiwa halijatua.
Juzi wanaharakati hao walisema haikuwa sahihi hata kidogo kwa mke huyo wa Rais kuhudhuria sherehe hizo.Katika hatua nyingine, Lilian Lucas,anaripoti kutoka Mvomero, Morogoro kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani humo kimepingana na msimamo wa wanaharakati hao na kumtetea Mama Kikwete kuwa alikuwa sahihi kuhudhuria sherehe hizo.
Katibu wa CCM Wilaya ya Mvomero, Deogratias Rutagumilwa, alitoa tamko hilo jana wakati wa maadhimisho ya wiki ya Jumuiya ya Wanawake wa CCM (UWT) iliyofanyika katika Kijiji cha Melela wilayani humo.Alisema nchi ya Swaziland ni nchi huru ambayo inaheshimu mila zake kama ilivyo Tanzania na kwamba mke wa Rais alikuwa na mwaliko wa kutembelea nchi hiyo na kuhudhuria ngoma hizo bila kikwazo kwani kukataa kwake ni kukataa mwaliko wa Tanzania katika nchi hiyo.
Alisema Waswazi wanaheshimu mila zao na tamaduni zao na ngoma aliyohudhuria Mama Kikwete ni sehemu ya tamaduni zao ambazo Tanzania haina mamlaka ya kuzipinga na yeye (mama Kikwete) asingeweza kukataa mwaliko huo, kwani kufanya hivyo ni kuijengea uhasama nchi yetu na Swaziland.