Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Mkakati wa Magufuli wabaini matapeli 30 wa viwanja hewa
Mkakati wa Magufuli wabaini matapeli 30 wa viwanja hewa
By Habari Tanzania | Published  10/3/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Kulwa Karedia

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, John Pombe Magufuli, ametangaza kunaswa kwa mtandao wa matapeli 30 wanaojihusisha na utengenezaji wa hati bandia ambazo huzitumia kugawa viwanja nchini kinyume cha sheria.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Dar es Salaam jana, Magufuli alisema katika mtandao huo tayari watu wanne wamekamatwa, mmoja kati yao ni mwenye asili ya Kiasia.

“Tumefanikiwa kukamata mtandao wa matapeli 30 ambapo kati ya hao tayari wanne wako mikononi mwa Jeshi la Polisi, mmojawapo ni mwenye asili ya Kiasia. Hawa wamekuwa mabingwa wa kutengeneza hati bandia ambazo huzitumia kugawa viwanja,” alisema Waziri Magufuli.

Aliongeza kuwa, zoezi hilo limeanza nchi nzima kwa wizara yake kushirikiana na Jeshi la Polisi na Taasisi ya Kuzuia Rushwa (PCB), linaonekana kuwa na manufaa zaidi.

“Nawaomba wananchi wasikubali kutapeliwa na watu hawa, watoe taarifa zao kwetu na sisi tutawashughulikia kwa mujibu wa sheria zilizopo, ili tuhakikishe kila Mtanzania anayestahili kupata kiwanja anapata kwa njia iliyo halali,” alisema Waziri Magufuli.

Kumekuwapo malalamiko kutoka kwa wananchi, juu ya kiwanja kimoja kugawiwa kwa zaidi ya mtu mmoja. Hata Rais Jakaya Kikwete alipata kukemea hilo, na akataka wahusika washughulikiwe. Imekuwa ikichukuliwa kwamba, hati zote hizo hutolewa na maofisa ardhi, hadi mtandao huu unapobainika.

Katika hatua nyingine, Waziri Magufuli amepiga marufuku halmashauri zote za wilaya kutuma maombi makao makuu ya wizara hiyo ya kutaka kuruhusiwa kutumia viwanja vilivyo wazi, wakati ukweli ni kwamba maeneo hayo yanatakiwa kubaki wazi.

Alisema hatua hiyo inatokana na halmashauri nyingi kutumia maeneo ya wazi kugawa kwa watu, kisha kusababisha matatizo makubwa kwa wale wanaopewa viwanja hivyo.

“Naagiza kuanzia sasa sitapokea maombi kutoka halmashauri yoyote ili nitoe kibali cha kugawa viwanja… hawa wamekuwa na tabia ya kugawa maeneo ya wazi kisha kuleta migongano isiyokuwa ya lazima katika jamii,” alisema Waziri Magufuli.

Alisema yeyote atakayekiuka agizo hilo, atamchukua yeye na maombi yake hadi kwa Rais Jakaya Kikwete ili liwe funzo tosha kwa viongozi wenye tabia ya namna hiyo.

“Yeyote atakayekiuka agizo hili, akija wizarani kwangu namchukua yeye na maombi yake moja kwa moja nampeleka kwa Rais Jakaya Kikwete ili akajibu tuhuma zake vizuri, maana suala hili Rais amekuwa akilipigia kelele kila siku,” alisema.

Magufuli alikuwa akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Makazi Duniani ambayo huadhimishwa Oktoba 2 ya kila mwaka.

Katika maadhimisho hayo, Waziri Magufuli amewataka Watanzania, hasa wale wanaoishi maeneo ya mijini, wakubali kupima viwanja vyao, ili kuepuka tatizo la kubomolewa nyumba zao.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Martin Madekwe, alizitaka taasisi za fedha, zikiwamo benki, kutoa mikopo katika sekta ya nyumba ili kusaidia kuondoa uhaba wa nyumba uliopo hivi sasa.

“Tunaziomba taasisi za fedha, kampuni, mashirika ya umma na mabenki kutoa mikopo kwa sekta hii, ili tuweze kujenga nyumba nyingi na kupunguza tatizo hili kwa Watanzania,” alisema Madekwe.

Ujumbe wa mwaka huu wa maadhimisho ya Siku ya Makazi Duniani ni ‘Miji, Matumaini ya Maendeleo’ ambapo inatarajiwa ifikapo mwaka 2050 watu bilioni sita watakuwa wanaishi mijini.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.