Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Asema amefika pazuri katika mpasuko Zanzibar
Asema amefika pazuri katika mpasuko Zanzibar
By Habari Tanzania | Published  10/3/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Mwandishi Wetu

RAIS Jakaya Kikwete amesema ameshaanza kulishughulikia tatizo la kisiasa la Zanzibar kama alivyoahidi wakati alipolihutubia Bunge kwa mara ya kwanza mwishoni mwa mwaka jana.

Akizungumza na wahariri wakuu wa vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini jana, Rais Kikwete bila ya kuingia katika undani, alisema tayari ameshafika mahali pazuri katika juhudi zake za kuhakikisha kile alichokiita mpasuko wa kisiasa wa Zanzibar kinapatiwa ufumbuzi.

“Kama nilivyosema wakati ule, ni kwamba naamini kule Zanzibar lipo tatizo ambalo lazima lipatiwe ufumbuzi… kulikuwa na mambo maeneo mengi ya kushughulikia, nikianzia ndani ya chama changu…nadhani nimefika mahali pazuri,” alisema Kikwete.

Kauli hiyo ya Kikwete kwa upande mwingine huenda ikawa imefungua ukurasa mpya katika kulipatia ufumbuzi tatizo hilo ambalo limedumu kwa takriban miaka 11 sasa, kutokana na kuwapo kwa mvutano mkali kati ya vyama vikuu viwili shindani visiwani humo, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF).

Mvutano huo ambao mwaka 2001 ulisababisha mtafaruku mkubwa hata maisha ya watu zaidi ya 20 kupotea huku wengine kadhaa wakijeruhiwa, umekuwa ukitokea katika chaguzi zote tatu za vyama vingi za mwaka 1995, 2000 na 2005, ambapo CUF wamekuwa wakipinga matokeo ya uchaguzi yanayowapa ushindi CCM.

Kwa upande mwingine, kauli hiyo ya Kikwete inaonyesha kwamba, pamoja na kuonekana akiwa kimya katika kipindi chote cha miezi tisa tangu atoe ahadi ya kulishughulikia suala hilo, amekuwa akiendesha kampeni zake chini chini ama ndani ya chama chake au pengine akikutana na viongozi wa CUF au wawakilishi wao.

Kauli hiyo ya Rais Kikwete ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa Taifa wa CCM imekuja siku chache tu baada ya Mwenyekiti wa Taifa wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, kumtaka awe ameanza kulishughulikia tatizo hilo kabla ya kuanza kwa mwezi Mtukufu wa Ramadhan ambao ulianza takriban siku tisa zilizopita.

Akizungumza na Tanzania Daima kwa simu jana, Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa CUF, Jussa Ismael Jussa, ambaye ni mmoja wa viongozi wa chama hicho walio karibu sana kikazi na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, alisema hajaona kuwapo kwa jambo lolote jipya katika kauli hiyo ya Kikwete.

Hata hivyo, alipotakiwa kueleza iwapo kumeshakuwapo mawasiliano ya chini kwa chini kati ya chama hicho na Rais Kikwete au mwakilishi wake, Jussa hakuwa tayari kueleza lolote zaidi ya kumtaka mwandishi wa gazeti hili kuwasiliana na Maalim Seif. Maalim mwenyewe hakuweza kupatikana alipotafutwa kwa njia ya simu.

CUF imekuwa ikizoa viti karibu vyote kisiwani Pemba, na CCM ikijiliwaza kwa kuiteka Unguja, na wakati mwingine hufikia kukaribiana kufungana. Hata hivyo, kwa kuwa Unguja ina majimbo mengi zaidi (yakiwamo yaliyogawanywa), CCM imekuwa na wawakilishi wengi zaidi.

Rais Kikwete amepata kuonya juu ya kuendeleza mpasuko huo, akisema kila kitu kina mwisho, na kwamba lazima Wazanzibari waishi kama ndugu.

Kuhusu kile kinachoonekana kuwa ni harakati za Chama cha CUF kujaribu kumlazimisha aanze kuushughulikia mgogoro huo, Kikwete alisema kama wanasiasa, wanayo haki ya kujitafutia ajenda ili kukabiliana na maadui wao wa kisiasa.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.