TUME ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imesema kwamba watendaji wakuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) walikuwa wakiingilia utendaji wa tume hiyo wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka jana.
Hayo yameelezwa katika ripoti ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari mjini hapa.
Ripoti hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa ZEC, Masauni Yussuf Masauni, na imesema pia viongozi wa serikali za mitaa na masheha wamekuwa wakiingilia kazi za uandikishaji wapiga kura, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Imeelezwa kwamba maofisa wa ZEC walikuwa wakijitahidi kutoa maelekezo, lakini viongozi hao waliyakataa, hivyo kusababisha malalamiko kutoka kwa wananchi.
“Watendaji wakuu wa serikali baadhi ya nyakati waliingilia maamuzi ya tume kinyume cha taratibu na sheria,” ilisema ripoti hiyo na kuongeza kwamba, katika Kisiwa cha Pemba kulifanyika udanganyifu mkubwa, kwa baadhi ya watu kujiandikisha zaidi ya mara moja.
Aidha, alieleza kwamba baadhi ya watoto ambao hawajafikia umri wa kupiga kura, waliandikishwa kisiwani humo baada ya kughushi vyeti vya kuzaliwa.
“Pemba kulijitokeza vitendo vya baadhi ya watu kujiandikisha zaidi ya mara moja au zaidi ya kituo kimoja, na watoto wenye umri mdogo waliojiandikisha walikuwa na vyeti vya kughushi,” ilisema ripoti hiyo.
Katika uchaguzi uliopita, Chama cha Wananchi (CUF) kilipata viti vyote 18 vya ubunge na uwakilishi kisiwani humo, wakati CCM walipata viti 31 kisiwani Unguja na kimoja kunyakuliwa na CUF katika Jimbo la Mji Mkongwe.
Aidha, ilisema kwamba, vyama vya siasa na wahisani, nyakati fulani walikuwa wakiingilia uamuzi wa ZEC, vitendo ambavyo ni kinyume cha sheria. Ilisema kwamba, vitendo hivyo vilijitokeza zaidi wakati wa uandikishaji na upigaji kura.
ZEC imewashutumu waangalizi wa uchaguzi kutoka ndani na nje, ambao walionyesha upendeleo katika shughuli zao za kiutendaji na kufikia hatua ya kuzozana na maofisa wake, jambo ambalo ni kinyume cha maadili.
“Wengine walilazimisha kupewa taarifa za uchaguzi kutoka katika kila kituo, kitendo ambacho ni kinyume na maadiili ya uchaguzi,” ilisema ripoti hiyo ya kurasa 145.
Hata hivyo, ripoti hiyo imeeleza kwamba, pamoja na matatizo hayo yaliyojitokeza, kwa ujumla uchaguzi huo ulifanyika katika mazingira ya uwazi, amani na utulivu na ulikuwa huru na wa haki.
Ripoti hiyo imesema ni kikundi kimoja cha waangalizi, Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu kilichosema uchaguzi huo haukuwa huru na wa haki na hivyo kushauri urudiwe na usimamiwe na jumuiya za kimataifa.
Kuhusu zoezi la ugawaji majimbo, ZEC imependekeza kifungu 120 (2) cha Katiba ya Zanzibar kifanyiwe marekebisho ili Baraza la Wawakilishi lisiwe na mamlaka ya kupunguza au kuongeza idadi ya majimbo ya uchaguzi. Alitaka jukumu hilo libakie kwa ZEC.
Aidha, ripoti hiyo iliyoandaliwa na makamishna wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na CUF imependekeza kifungu cha sheria 119 (13) 72 (1) na 24 (2) vya Katiba ya Zanzibar vifanyiwe marekebisho ili kuondoa mvutano wa kisheria.
Ripoti hiyo imesema vifungu hivyo vinaruhusu mwananchi ambaye hakutendewa haki kuidai mahakamani, lakini ibara ya 119 (13) inasema hakuna mahakama yoyote itakayokuwa na mamlaka ya kuchunguza jambo lolote lililotendwa na Tume ya Uchaguzi katika kutekeleza madaraka yake.
Wakati ripoti hiyo ilipowasilishwa kwa Rais wa Zanzibar, alisifu Tume ya Uchaguzi kwa kufanikisha uchaguzi huo na kuwataka kushughulikia kasoro zilizojitokeza ili uchaguzi ujao uwe mzuri zaidi.
Alisema vyama vya siasa ni utamaduni wao kulalamika juu ya matokeo ya uchaguzi, hasa pale wanaposhindwa kufikia malengo ya kisiasa.
Katika Uchaguzi Mkuu uliopita Zanzibar Oktoba 30 mwaka jana, Rais Karume aliibuka mshindi kwa kupata asilimia 53.2 ya kura na mpinzani wake mkubwa, Seif Shariff Hamad wa CUF kupata asilimia 46.