RAIS Jakaya Kikwete, amesema serikali yake imefikia uamuzi wa kuzirejesha baadhi ya nyumba za serikali zilizouzwa kwa watumishi wa umma baada ya kubaini kwamba zilijengwa katika mazingira nyeti.
Kikwete aliyasema hayo jana Ikulu jijini Dar es Salaam wakati alipokuwa akijibu maswali ya wahariri wakuu wa vyombo mbalimbali vya habari aliokutana nao chini ya kivuli cha utaratibu aliojipangia wa kuzungumza na wananchi kila mwishoni mwa mwezi.
“Hatukusudii kuzichukua nyumba zote…kwa mfano kuna OCD kauziwa nyumba ya OCD iliyo katika eneo la polisi, na yule OCD aliyeuziwa kahamishwa kutoka Mtwara kwenda Mafia…au kastaafu na nyumba kapangisha…Kwa kweli kuna maeneo ambayo lazima tufanye marekebisho,” alisema Kikwete.
Ingawa hakufafanua iwapo uhakiki wa nyumba zitakazorejeshwa umeshafanyika au la, na wakati hasa utakapoanza utekelezwaji wa kazi hiyo, kauli yake hiyo imehitimisha minong’ono na malumbano ambayo yamekuwapo kwa muda sasa, kuhusu suala hilo.
Hivi karibuni, Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu, John Kijazi, alikaririwa na vyombo kadhaa vya habari (si Tanzania Daima) akikanusha taarifa zilizoandikwa na gazeti moja la kila Jumapili siku kadhaa zilizopita kuhusu kuwapo kwa mpango wa serikali wa kuzirejesha nyumba hizo ambazo uuzwaji wake uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Tatu ulizusha manung’uniko makubwa.
Kwa upande mwingine, kauli ya jana ya Kikwete imeonyesha kuwapo kwa mabadiliko makubwa ya kimsimamo kwake mwenyewe, kwani siku chache baada ya kuteuliwa kuwa mgombea urais katikati ya mwaka jana, alisema akiingia madarakani hatazirejesha nyumba hizo na badala yake ataangalia mustakabali wa siku zijazo.
Kikwete katika mazungumzo yake ya kwanza na wahariri tangu achukue madaraka ya urais Desemba 21 mwaka jana, alikiri kupokea majina yaliyotumwa kwake na taasisi moja isiyo ya kiserikali ambayo iliwataja kwa majina vigogo wanaohusika na uingizaji wa dawa za kulevya hapa nchini.
Bila kuingia katika undani wa suala hilo, wala kuwataja kwa majina, Kikwete alisema ameshawasilisha katika vyombo vinavyohusika majina hayo ili uchunguzi wa kina uweze kufanyika kabla hatua hazijachukuliwa.
Rais Kikwete alisema pia kwamba, ahadi aliyoitoa katika hotuba zake kadhaa huko nyuma kuhusu kulishughulikia tatizo hilo, iko pale pale na kwamba anatarajia kuanza na vigogo wanaoingiza dawa hizo kabla ya kuanza kuwasaka wale wanaotumia.
“Suala la madawa ya kulevya nimelipa umuhimu mkubwa kama nilivyowahi kusema katika hotuba zangu nyingine huko nyuma. Nadhani katika kulishughulikia hilo hatuna budi kupambana kwanza na hawa wanaoleta,” alisema Kikwete.
Mbali ya suala hilo na la nyumba, Kikwete pia alieleza kuridhishwa na namna uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam ulivyoliendesha katika hali ya amani na utulivu zoezi la kuwahamisha wafanyabiashara ndogo ndogo, maarufu kwa jina la wamachinga kutoka katika mitaa mbalimbali ya jiji.
Kikwete alizitaka mamlaka zinazohusika kuhakikisha kwamba, maeneo yote yaliyotengwa kwa ajili ya wamachinga yanaimarishiwa miundombinu kama vyoo na maji, vyenye hadhi ya juu, ili kuwawezesha wafanyabiashara hao kuendesha shughuli zao bila matatizo.
Alisema baada ya wamachinga kupatiwa maeneo maalumu, hatua itakayofuata itakuwa ni kuandaa programu za mafunzo ya biashara, ambayo hatimaye yatawawezesha vijana hao kukopesheka na mwishowe nao kukua kibiashara na kufungua maduka, badala ya kuzeeka wakiuza mashati ya kutembeza mitaani.
Alisema atashangaa na kumuona mtu mwenye fikra finyu iwapo atasikia kuna mmachinga ambaye ataamua kurejea tena barabarani akiwa anatembeza mashati au akiuza mipira ya usukani na wakati mwingine visu.
Akizungumzia kuhusu tatizo kubwa la umeme, Rais Kikwete aliainisha mikakati mbalimbali ya muda mfupi na mrefu iliyoanza kuchukuliwa na serikali katika kukabiliana na suala hilo.
Alisema kina cha maji katika Bwawa la Mtera kimeendelea kuporomoka na kwamba hadi kufikia sasa kina cha maji ni sentimita 687.48 na kitakapofika sentimita 687 litapaswa kusimamisha uzalishaji wa umeme.
Rais alisema tayari serikali imeshafikia makubaliano na kampuni mbili za nje ambazo zitaleta mitambo miwili tofauti yenye uwezo wa kuzalisha jumla ya umeme wa megawati 140, ambayo itakuwa imekamilika kati ya mwishoni mwa mwezi Novemba na mwanzoni mwa Desemba mwaka huu.
Alisema serikali pia imeagiza mtambo mwingine wenye uwezo wa kuzalisha megawati 100 za umeme kutoka nchini Finland ambao unatarajiwa kuwa utakuwa umekamilika na kuanza kufanya kazi Julai mwakani.
Aidha, alisema kugundulika kwa gesi mkoani Mtwara ambayo ni mara mbili kwa wingi zaidi ya ile ya Songosongo na mpango wa kuongeza uzalishaji wa umeme kutoka katika makaa ya mawe ya Kiwira hadi kufikia megawati 200, ni baadhi tu ya mikakati ya serikali ya kukabiliana na tatizo hilo la umeme.
Mbali ya hayo, Rais alitumia fursa ya mkutano wake wa jana na wahariri kueleza manufaa yaliyotokana na ziara yake ndefu iliyompitisha, Hispania, Cuba na baadaye Marekani.