ZOMEA zomea iliyoibuka wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka jana, imerejea kwa kishindo, na safari hii imeanzia mkoani hapa.
Ilikuwa katika ziara ya Waziri Mkuu, Edward Lowassa, ambako wananchi wa Makambako, waliamua kumtolea uvivu mbunge wao, Jackson Makwetta, wakisema kero zimezidi na hajafanya chochote kuwasaidia.
Mbunge huyo wa Njombe Kaskazini, ameonja joto ya jiwe akiwa na Waziri Lowassa, baada ya kuonja kali kama hiyo, akiwa na aliyekuwa mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete (sasa rais), mwaka jana wakati akimnadi.
Zomea zomea ilianzia mikoa ya kusini, ambayo kwa kawaida imekuwa haina ushindani mkubwa kisiasa, wabunge wengi wakiwa ni wa CCM. Ilikuwa mwanzoni mwa kampeni za Kikwete, ikazua maswali mengi na kuleta ugumu katika CCM, kwamba ikiwa kusini wanaikataa CCM, maeneo mengine hali ingekuwa ngumu zaidi.
Mmoja wa waliopata kuzomewa kupita kiasi, na kuonyesha kukataliwa kabisa mbele ya Rais Kikwete, ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Hawa Ghasia. Wengine waliozomewa enzi hizo ni aliyekuwa Naibu Spika wa Bunge, Juma Akukweti kabla ya zomea zomea kuhamia Kanda ya Ziwa.
Lowassa alikuwa akihutubia mkutano wa hadhara kwenye Viwanja vya Mashujaa mjini Makambako, ndipo wananchi wakawa kama vile wamelipuka, na kuanza kuzomea, wengine wakieleza kwamba wanataka mbunge wao asimame ajibu kwa nini kero zimezidi jimboni kwao.
Waziri Mkuu alitumia muda mrefu kuwatuliza wananchi hao, na pia akawa anawataka wasitumie mkutano wake kuzungumza na mbunge wao, bali wapange siku nyingine wakazungumze naye.
“Msitumie mkutano wangu kutaka kuzungumza na mbunge wenu, tafuteni muda wenu mfanye mkutano wenu,” alisema Waziri Mkuu.
Wananchi walilalamika kwamba, mbunge wao Makwetta hawatatulii kero zao, kati ya hizo zikiwa ni barabara kutokuwa na mitaro, lakini kubwa zaidi, ni kwamba hawapati taarifa za utekelezaji kutoka kwenye halmashauri, na hawaelezwi fedha zinavyotumika.
Mbaya zaidi, walisema kwamba Makwetta haonekani jimboni, isipokuwa wakati Waziri Mkuu alipokaribia kufika, alikwenda na kufanya mikutano miwili mitatu, ilhali wakati wa kampeni CCM ilitoa ahadi nyingi na mbunge aliahidi kusimamia utekelezaji wake.
Wananchi hao walipaza sauti wakisema; “msimamishe huyo atueleze.” Mmoja wa wananchi ambaye ni kiongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), alipopewa nafasi kutoa kero yake, alisema ni afadhali achaguliwe kijana wa chipukizi, kwani anaamini anaweza kufanya mambo mazuri kuliko Makwetta.
Wananchi hao pia walimshutumu Diwani wa Kata ya Makambako, Deo Sanga. Walidai kuwa diwani huyo hakai kwenye kata yao, kwani amekuwa akiishi Dar es Salaam muda wote na alirudi Makambako aliposikia kuna ujio wa Waziri Mkuu.
Walipiga kelele wakidai kuwa diwani huyo hajui lolote, kwani hakai nao. Hata hivyo, Waziri Mkuu alimtaka diwani huyo kufanya mikutano ya mara kwa mara kusikiliza kero za wananchi.
Wananchi kueleza kero zao hadharani na kutoa malalamiko dhidi ya wabunge na madiwani, kunaonyesha kuamka. Kumekuwa na harakati za kisiasa zinazoendelea hivi sasa, ambapo viongozi wakuu wamekuwa katika ziara za ndani na nje ya nchi.
Rais Kikwete amemaliza ziara ya wiki mbili nchini Marekani, wakati Lowassa amekuwa katika ziara za ndani na nje, kuhimiza utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM, na amekuwa akitoa fursa kwa wananchi kuuliza maswali, kueleza kero zao, kisha kuwataka viongozi wa ngazi husika kutoa majibu, au kufuatilia vitu vinavyolalamikiwa.
Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba, naye amekuwa akizuru mkoa mmoja baada ya mwingine, katika kukiimarisha chama chao, ikiwa ni pamoja na kupokea wanachama wapya, baadhi wakiwa viongozi wa upinzani. Haya yanafanyika ikiwa hata mwaka mmoja haujamalizika tangu Uchaguzi Mkuu ufanyike.