Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Operesheni wamachinga isihusishe mtandao wa wauza magazeti
Operesheni wamachinga isihusishe mtandao wa wauza magazeti
By Habari Tanzania | Published  10/1/2006 | Habari za Kitaifa | Rating:

ZOEZI la kuwaondoa wafanyabiashara ndogo ndogo, maarufu kwa jina la wamachinga limetekelezwa usiku wa kuamkia jana. Bila shaka hilo ni zoezi lililopokewa kwa hisia za namna mbili.

Wapo waliopokea zoezi hilo kwa uchungu. Kundi hili la wenye uchungu kwa namna moja ama nyingine, linajumuisha wamachinga waliohamishwa kutoka katika maeneo yao ya awali. Sababu kubwa ni moja, hali ya kibiashara katika maeneo wanayopaswa kwenda hawaifahamu, hivyo kundi hili liko katika kitendawili.

Kundi jingine ni la wakazi waliokuwa wakipata usumbufu kutokana na kuwapo kwa wamachinga katika baadhi ya maeneo ya Jiji la Dar es Salaam, hususan maeneo yaliyopangwa kubaki wazi au kutumika kwa matumizi mengine, mfano baadhi ya barabara za mitaa ya maeneo ya Kariakoo.

Kimsingi hatua inayochukuliwa na uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam si ya kupingwa. Lakini katika zoezi hili, jambo linaloweza kuzua utata ni kuwa yupi ahamishwe na yupi abaki.

Utata huo ndiyo unaohitaji maamuzi mapya. Katika viunga mbalimbali vya Jiji la Dar es Salaam, wapo wafanyabiashara ya magazeti. Kwa bahati serikali ya awamu ya nne imeunda wizara maalumu inayoshughulikia pamoja na mambo mengine, masuala ya habari.

Kigezo hicho cha serikali kuanzisha wizara mahsusi ya habari, maana yake ni kwamba inatambua umuhimu wa sekta ya habari nchini.

Katika sekta ya habari, vyombo vya habari yakiwamo magazeti hutambulika kama mhimili mkuu wa sekta nzima. Mbali na vyombo vya habari, nguzo nyingine kuu ni waandishi wa habari, na wafanyakazi wengine.

Lakini lipo kundi jingine muhimu. Hili ni kundi la wauzaji wa zao la mwisho la mwandishi wa habari. Kundi hili ni la wafanyabiashara, hasa wa magazeti.

Usiku wa kuamkia jana, wamachinga waliondolewa katika maeneo yao ya awali ya biashara. Kwa namna fulani zoezi hilo lilijumuisha hata wauza magazeti.

Tunaamini kuwa hilo ni jambo la kushangaza. Ni jambo la kushangaza kwa sababu kadhaa. Kwanza haiingii akilini kwa viongozi kuwataka wauza magazeti kukusanyika katika eneo moja la biashara. Eti wakauze magazeti gulioni!

Biashara ya magazeti ni lazima ifanyike katika kila eneo jijini kwa wakati mmoja. Hiyo ndiyo kanuni kuu ya biashara ya magazeti.

Magazeti ni biashara inayotafuta wanunuzi. Tofauti iliyopo kati ya biashara hii na nyingine ni kuwa, taifa huunganishwa kitaarifa kupitia vyombo vya habari, hususan magazeti.

Kwa sababu hiyo, tunaamini kuwa ni jambo la busara zaidi kwa wafanyabiashara ya magazeti kuendelea kutoa huduma yao katika viunga vya jiji.

Mathalani, ni jambo la kushangaza kutaka wauza magazeti kukusanyika katika soko la Mchikichini au eneo la Kigogo kwa ajili ya kuendesha biashara hiyo.

Hivi ni jambo la busara kwa mkazi wa Dar es Salaam anayeelekea ofisini asubuhi, tena akiwa katika usafiri alazimike kwenda katika gulio la Mchikichini kununua magazeti?

Hizo barabara za kuelekea huko ziko wapi? Zinatosha? Msongamano wa magari asubuhi utahifadhiwa wapi ili kuwapisha watakaokwenda kununua magazeti, ilhali wakihitajika kuwahi ofisini?

Tunaamini kuwa kuwakusanya hata wauza magazeti katika maeneo teule si jambo la busara. Wafanyabiashara hawa wanastahili kuendelea kuwapo mjini na maeneo mengine, japo katika utaratibu maalumu.

Kinyume cha hayo, Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam itakuwa ikienda kinyume cha malengo ya Serikali Kuu ya kutaka kuwa na jamii inayopashana habari kwa haraka na kwa kiwango cha juu.

Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam itakuwa ikienda kinyume cha bajeti kuu ya serikali kwa mwaka wa fedha wa 2006/2007. Katika bajeti hiyo, serikali iliamua kupunguza ushuru wa karatasi ili kutoa unafuu kwa wazalishaji wa magazeti, ili nao waweze kutoa unafuu wa bei kwa wasomaji.

Kinyume cha hapo, Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam itakuwa imefanya maamuzi makubwa bila umakini na pengine kwa kukurupuka. Serikali ya Dar es Salaam itakuwa imejikwaa kimaamuzi.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.