WAKATI mfungo wa Ramadhan ukiingia siku ya nane leo, tafrani imezuka Zanzibar baada ya mfanyabiashara mmoja kukamatwa na kufunguliwa mashitaka ya kuuza vyakula katika kipindi cha mfungo huo nyakati za mchana.
Mfanyabiashara huyo, James John Sakubu (28) amekamatwa katika eneo la biashara la Malindi na kufikishwa mahakamani kwa kosa la kuuza chakula ndani ya mwezi wa Ramadhan.
Hata hivyo, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Omar Makungu, amefafanua mwelekeo wa maamuzi kuhusu tafrani hiyo akisema, hakuna sheria inayozuia mtu yeyote kuuza chakula katika kipindi cha mwezi wa Ramadhan.
Akihojiwa kuhusu suala hilo, Makungu alisema kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, kila mtu ana haki ya kufanya kazi ili aweze kupata mahitaji yake.
“Hakuna sheria inayomzuia mtu asiuze chakula mwezi wa Ramadhan, na kama ipo basi wengi wangekamatwa ikiwemo, wauza mikate na maandazi,” alisema Naibu Mwanasheria Mkuu.
Alieleza kwamba anavyofahamu yeye yapo matoleo yanayozuia mtu kula hadharani huku watu wengine wakiwa wamefunga, lakini sio kuzuia mtu kuuza chakula,” alisema.
Makungu alisema kwamba matoleo hayo yalikuwa yakitumika siku za nyuma ili kuweka nidhamu katika mwezi mtukufu wa Ramadhan, hasa kwa kuzingatia idadi kubwa ya wakazi wa Zanzibar wanafunga.
Alisema hafahamu ni sheria gani imetumiwa na Baraza la Manispaa kumfungulia mashitaka mfanyabiashara huyo na kuahidi kuwa atachunguza zaidi suala hilo.
Aidha, alisema hawezi kusema kwanini mfanyabiashara huyo amekamatwa ilhali wapo wengine wanaoendesha biashara za chakula na hata huduma za baa tangu kuanza kwa mwezi wa Ramadhan.
Mwanasheria wa siku nyingi Zanzibar, Salum Taufiq, aliunga mkono kauli ya Naibu Mwanasheria Mkuu huyo na kusema iwapo sheria hiyo ingekuwepo wakazi wengi wangekamatwa Zanzibar.
Alisema sheria iliyopo ni ya kuzuia kufanya biashara katika maeneo ya wazi bila ya kuwa na leseni za manispaa.
“Hakuna sheria inayozuia mtu kuuza chakula na kama sheria hiyo ipo, basi maduka ya nyama na wauza mikate wangetakiwa wasiuze,” alisema mwanasheria huyo ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria Zanzibar.
Alisema suala hilo linaweza kufungua mjadala mkubwa kwa wanasheria na wanaharakati wa haki za binadamu kutokana na uzito wake.
Meya wa Manispaa ya Zanzibar, Mahboub Juma, alipoulizwa kuhusu tafrani hiyo, alisema hafahamu ni sheria gani imetumika dhidi ya mfanyabiashara huyo.
“Naomba watafute watu wa kamati ya sheria na uongozi wa Baraza, inawezekana wao ndio wanafahamu sheria iliyotumika kumkamata kijana huyo na kumshitaki,” alisema.
James alisomewa mashitaka yake na Mwendesha Mashitaka wa Baraza la Manispaa, Ali Abdallah Haji kuwa alitenda kosa hilo katika mtaa wa kibiashara wa Malindi juzi saa 4:00 asubuhi.
Ilidawa mahakamani hapo kuwa, siku ya tukio, James alikamatwa na masufuria yakiwa na maharage, maandazi na chai akiwauzia wateja wake, kinyume cha sheria za mitaa na maeneo ya wazi ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
James ameamriwa kwenda rumande na hakimu Ndame Ali wa Mahakama ya Mwanzo Mwanakwerekwe baada ya kushindwa masharti ya dhamana.
Baadhi ya wananchi wamesema kesi hiyo itaweka msingi mzuri kwa siku za baadaye, juu ya mambo ya kufuatwa katika mwezi wa Ramadhan, lakini wengine walisema inaiweka pabaya serikali katika medani za haki za binadamu.